Mwanyika atakiwa kwenda kwa DPP

Muktasari:

Serikali ya Tanzania  imeutaka upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Deogratius Mwanyika kwenda kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kufuatilia makubaliano waliyoingia baina ya Serikali na kampuni ya madini ya Barrick.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imeutaka upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Deogratius Mwanyika kwenda kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kufuatilia makubaliano waliyoingia baina ya Serikali na kampuni ya madini ya Barrick.

Hatua hiyo inatokana na upande wa utetezi kuuomba upande wa mashtaka kufuatilia na kujua kama makubaliano waliyoingia kati ya Serikali na kampuni hiyo yatasaidia kuiondoa kesi hiyo mahakamani.

Mwanyika ambaye alikuwa Rais wa migodi ya Pangea, North Mara Exploration na Bulyanhulu na wenzake sita wanakabiliwa na mashtaka 39 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi ya zaidi ya dola za Marekani 112 milioni.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Februari 14, 2020 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Godfrey Isaya kuwa wajibu wa kufuatilia makubaliano hayo ni wa upande wa utetezi na sio upande wa mashtaka.

"Upelelezi wa kesi hii haujakamilika na niseme tu upande wa utetezi ndio wenye jukumu la kufuatilia makubaliano hayo yaliyoingiwa baina ya Serikali na kampuni ya Barrick kwa DPP na sio sisi,” amedai wakili Simon.

Awali, wakili wa utetezi, Lwekama Rwekiza amedai mahakamani hapo kuwa yapo mazungumzo baina ya Serikali na kampuni ya Barrick yanayosimamia kampuni ambayo wateja wao ni waajiriwa.

Amedai shauri hilo linahusiana na makubaliano yaliyotiwa saini hivi karibuni baina ya Serikali na Barrick kuashiria kumalizika kwa mgogoro uliokuwepo awali.

"Shauri  hili lina uhusiano na makubaliano yaliyosainiwa baina ya Serikali na kampuni ya Barrick, na vyombo vya habari vimeripoti kumalizika kwa mgogoro baina ya Serikali na kampuni hizi kwa kuanzishwa kampuni ya Twiga ambayo Serikali ni mbia, naiomba mahakama yako ielekeze upande wa mashtaka kufuatilia na kuona namna ya kufuta shauri hili," amedai Rwekiza.

Hakimu Isaya baada ya kusikiliza hoja za upande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, 2020 itakapotajwa.

Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Mwanyika , washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 77/2018 ni meneja uhusiano wa mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo;  mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo; kampuni ya mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration Du Nord LTEE na Bulyanhulu.

Kati ya mashtaka hayo 39 yanayowakabili;  mashtaka 17 ni ya utakatishaji fedha, mashtaka nane ya ukwepaji kodi, saba ya kughushi nyaraka,  matatu ya kula njama na shtaka moja la kusaidia kuongoza uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutoa rushwa.

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Aprili 11,  2008 na Juni 30, 2017 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,  Kahama, Tarime na Biharamulo pamoja na maeneo mbalimbali ya mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini, mjini wa Toronto nchini Canada na visiwa vya Barbados na nchini Uingereza walikula njama ya kutenda makosa hayo.

Miongoni mwa mashtaka ni  kutoa rushwa ambapo Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kutoa Sh718 milioni kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Shinyanga,  Hussein Kashindye kwa lengo la kumshawishi aachane na  uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kukwepa kodi, inadaiwa kati ya Mei 16, 2008 na Desemba 31, 2008 katika maeneo hayo wakiwa na nia dhahiri, walitoa tamko la uongo kwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kukwepa kodi ya dola za kimarekani 9 milioni  ambayo ilikuwa ni kodi iliyotakiwa kulipwa TRA.