VIDEO: Mwenyekiti wa zamani bodi ya MCL aweka wazi alichoelezwa na Mufuruki

Muktasari:

Mkurugenzi  mkuu wa kampuni ya Lindam Group Limited, Zuhura Muro ameeleza namna mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki alivyomuaga kabla ya kukutwa na umauti  Desemba 8, 2019.

Dar es Salaam. Mkurugenzi  mkuu wa kampuni ya Lindam Group Limited, Zuhura Muro ameeleza namna mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki alivyomuaga kabla ya kukutwa na umauti  Desemba 8, 2019.

Muro, mwenyekiti wa bodi mstaafu wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 10, 2019 wakati akitoa salamu za rambirambi katika shughuli  ya kumuaga Mufuruki kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Mufuruki aliyefariki dunia Desemba 8, 2019 katika jiji la Johannesburg,  Afrika Kusini alishiriki kwa uwezo wake kuijenga MCL na waandishi wake ambao wengine  wamekwenda kuajiriwa maeneo mengine.

Enzi za uhai wake, Mufuruki aliwahi kuwa mwenyekiti wa MCL, ambayo ni kampuni tanzu ya Nation Media Group (NMG ) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mitandao yake ya kijamii ikiwamo MCL Digital.

Katika salamu zake za rambirambi, Muro amesema alipopata taarifa za Mufuruki kuwa mgonjwa  alikwenda kumjulia hali katika Hospitali ya Aga Khan  alikokuwa akipatiwa matibabu kabla ya kusafirishwa kwenda Afrika Kusini.

“Tulikuwa katika harakati za kumsafirisha kwenda Afrika Kusini  kutibiwa, nilizoea kumuona  akiwa mcheshi lakini siku hiyo niligundua kuwa rafiki yangu anaumwa.”

“Nilimsogelea kisha akafungua macho yake akaniita jina langu  akaniambia ‘nakufa’ nikamwambia hapana huwezi kufa umepambana vita nyingi nina amini na hivi utashinda,” amesema Muro.

Amesema amejifunza mengi kutoka kwa Mufuruki lakini kikubwa  ni upendo, uadilifu na uchapakazi.