Mwinyi awapa somo wasomi Tanzania

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa  cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Muktasari:

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa  cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amewataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi wanaoupata kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya nchi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa  cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amewataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi wanaoupata kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya nchi.

Amesema kasi ya maendeleo katika uchumi wa nchi yoyote duniani hutegemea uwekezaji wa maarifa na ujuzi.

Mwinyi ametoa rai hiyo leo Alhamisi Desemba 12, 2019 katika mahafali ya pili ya KIUT. Wanafunzi 1148 wamehitimu masomo yao katika kozi mbalimbali.

“Pamoja na kujiendeleza kwa masomo ya juu zaidi napenda kuwahimiza  mkatilie maanani uaminifu kazini, mkakiwakilishe vyema chuo chetu kwa kuwa waadilifu na kutoshiriki kwa namna yoyote ile katika matendo ya kifisadi.

“Nawaalika wanajumuiya ya KIUT pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, tumuunge mkono Rais wetu (John Magufulj) kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake na kufanya kazi kwa bidii ili maisha bora yawe na tafsiri kwetu sote pamoja na vizazi vyetu,” amesema Mwinyi.

Ameongeza, “kwa mfano ni kwa kiasi gani elimu na huduma tutoazo zitasaidia Tanzania kufikia uchumi wa viwanda.”

Makamu mkuu wa chuo hicho, Jamidu Katima amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa kujitolea ili wapate uzoefu.