Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuboresha mfumo wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma

Waziri Mkuu Dk, Mwigulu Nchemba akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo la Kalenga katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumamosi Juni 6, 2026 eneo Ifunda wilayani Iringa mkoani Iringa.

Muktasari:

  • Asema mfumo wa ufuatiliaji uliopo sasa unaruhusu uwepo wa watu wanaofanya upigaji bila kuguswa huku wengine wakiwa kwenye maeneo yenye ukame wa fursa na ufuatiliaji mkali zaidi wa kiutendaji, jambo ambalo linahitaji marekebisho ya mfumo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itafanya maboresho ya sheria ili kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika ngazi zote ili kuwabana wale ambao hawaguswi na mifumo ya uwajibikaji.

Hatua hiyo inatokana na kutoridhishwa kwake na mifumo ya uwajibikaji ikiwemo inayofanywa na  Sekretarieti ya Maadili ambayo kwa kiasi kikubwa inashughulika na ufuatiliaji wa viongozi kwa kuwataka kuwasilisha fomu za maadili na kutaja mali zao.

Akizungumza leo Juni 6, 2026 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Iringa, Dk Mwigulu amesema taasisi hiyo kwa kiasi kikubwa inashughulika na ufuatiliaji wa viongozi kuwasilisha fomu za maadili na kutaja mali zao huku ikiwaacha watu walio kwenye mirija ya kujilimbikizia fedha.

Amesema mfumo wa ufuatiliaji uliopo sasa unaruhusu uwepo wa watu wanaofanya upigaji bila kuguswa huku wengine wakiwa kwenye maeneo yenye ukame wa fursa na ufuatiliaji mkali zaidi wa kiutendaji, jambo ambalo amesema linahitaji marekebisho ya mfumo.

“Tuna sekretarieti yetu ya maadili, na nilishawaelekeza. Kwa kiwango kikubwa wanashughulika na kumulika wanasiasa wajaze fomu za maadili, wataje mali walizo nazo. Sio kwamba hatupingi wajaze, lakini…

“Kuna watu wengine wamekaa pazuri, wametegesha rada zao wanavuna hawaonekani, halafu kuna wengine ambao wako kwenye ukame, ndiko ambako tochi zimeelekezwa za kulia, ndiko mitego ilivyopo. Sasa haya na yenyewe tumesema lazima tuyasimamishe,” amesema Dk Mwigulu.

Wananchi wa Jimbo la Kalenga wakimsikiliza Waziri Mkuu Dk, Mwigulu Nchemba katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumamosi Juni 6, 2026 eneo Ifunda wilayani Iringa mkoani Iringa.

Amesema hali hiyo imeifanya Serikali kuanza maboresho ya mifumo ya uwajibikaji kupitia sekretarieti ya maadili, kwa lengo la kufanya ulinganifu wa kiutendaji ili kubaini maeneo yenye hatari kubwa ya upotevu wa rasilimali, akitolea mfano sekta zinazokusanya mapato na kutoa leseni.

“Mimi nimekulia ndani ya serikali na naijua. Hivi kati ya diwani wa kata na ofisa aliyeko bandarini anayekusanya mapato, ni yupi yuko kwenye bomba? Na ofisa wa mamlaka anayekadiria mapato, yupi yuko kwenye bomba? Hivi mmewaona madiwani wangapi wana nyumba za gorofa?” amehoji.

Amesema maeneo yenye usimamizi wa moja kwa moja wa fedha na rasilimali za umma ndiyo yanapaswa kupewa kipaumbele zaidi katika ufuatiliaji wa maadili na uwajibikaji.

Ameongeza kuwa hata katika utoaji wa leseni na mikataba, bado kuna changamoto ya uwiano wa uwajibikaji, akibainisha kuwa baadhi ya nafasi muhimu zinahitaji uangalizi zaidi kuliko zilivyo sasa.

“Hivi, mbunge anasaini mkataba gani? Unamwacha anayetoa leseni za madini, yeye anaambiwa ajaze tu ahadi ya uaminifu,” amesema Dk Mwigulu.

Ameeleza kuwa mfumo wa sasa unahitaji marekebisho kwa sababu baadhi ya maeneo yenye hatari kubwa ya rushwa hayapewi uzito unaostahili katika ufuatiliaji wa maadili.

“Nimewaambia hizi fomu zibadilishwe. Namba moja iwe kwenye maeneo yaliyo na vishawishi vingi vya rushwa, sio hii ya business as usual,” amesema.

Waziri Mkuu Dk, Mwigulu Nchemba akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo la Kalenga katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumamosi Juni 6, 2026 eneo Ifunda wilayani Iringa mkoani Iringa.

Amesema Serikali itaachana na utaratibu wa kawaida wa kukamilisha karatasi bila ufuatiliaji wa kina, na badala yake itajielekeza kwenye maeneo halisi yenye changamoto za kiutendaji.

“Tunamaliza karatasi za bure, twende kwenye eneo ambalo tunalijua. Ufuatiliaji ufanyike zaidi kwenye maeneo hayo ili keki hii iwanufaishe kila mtu,” amesema.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa dawa hospitalini, akibainisha kushangazwa na hali ya baadhi ya wagonjwa kuandikiwa kununua dawa nje ya vituo vya afya licha ya Serikali kuwekeza zaidi ya asilimia 90 ya upatikanaji wa dawa.

“Dawa ni zaidi ya asilimia 90, lakini bado mgonjwa anaambiwa aende kununua mtaani. Hii inatoka wapi?” amehoji Waziri Mkuu.

Amesema Serikali, pia, inachunguza mifumo ya usambazaji wa dawa na taarifa za baadhi ya dawa kuhitajika kuteketezwa baada ya muda wake kuisha, akibainisha kuwepo kwa sintofahamu inayohitaji ufafanuzi wa kina.

“Zime-expire (kwisha muda) zipi kama watu walikuwa wanaambiwa dawa hamna wakanunue mtaani? Haya yote tunayafanyia kazi,” amesema Dk Mwigulu.