Polisi: Mangula ana sumu mwilini

Muktasari:

Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema baada ya kufanya uchunguzi limebaini makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula ana sumu mwilini.

Dar es Salaam. Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema baada ya kufanya uchunguzi limebaini makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula ana sumu mwilini.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Machi 9, 2020 na Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema polisi wameanza uchunguzi  kubaini namna sumu hiyo ilivyoingia mwilini mwake na litachukua hatua kali kwa atakayebainika kupanga au kuratibu jambo hilo.

Jumamosi ya  Februari 29, 2020  Rais wa Tanzania, John Magufuli alimjulia hali Mangula aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuanguka ghafla Ijumaa Februari 28, 2020.

Taarifa ya Mangula kuugua ilitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa huku video zikimuonyesha Magufuli akizungumza naye, baadaye kusali pamoja.

Mangula alionekana akiwa amelala kitandani huku akiwa na plasta juu ya jicho lake la kushoto.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Mangula ambaye  alishiriki kikao cha kamati kuu ya chama hicho sambamba na Magufuli  kilichofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba Februari 28, 2020, baada ya kuanguka alilazwa chumba cha uangalizi maalum (ICU).

“Mangula aliugua ghafla jana na kisha kukimbizwa hospitali kwa matibabu,” inaeleza taarifa hiyo.

“Utapona na Mungu atakusimamia katika tatizo hili, sisi tulipoona jana (Ijumaa Februari 28, 2020)  umeanguka ilitushtua,” amesema Magufuli na Mangula kujibu, “sijui nimeangukaje.”

 “Huwezi  ukajua ila sisi tunamkabidhi Mungu na Mungu atakusimamia, Mungu akujalie sana,” amesema Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi