VIDEO: Polisi waeleza mabilioni ya NBC yalivyoibwa Dar, wanne mbaroni

Tuesday February 25 2020

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne, wakiwemo waliokuwa  wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya G4S kwa tuhuma za kuiba Sh1.2 bilioni, Dola 402,000 za Kimarekani na Euro 27,700 walizokuwa wakizipeleka makao makuu ya Benki ya NBC kutoka katika matawi ya benki hiyo.

Akizungumza leo Jumanne Februari 25, 2020 Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Christopher Rugemalila, Mohamedi Ramadhani, Ibrahimu Maunga na Salumu Shamte.

Mambosasa amesema wizi huo umefanyika Februari 7, 2020 siku ambayo Rugemalila, Ramadhani na Maunga walikuwa katika gari aina ya Toyota Nissan mali ya kampuni ya G4S wakisindikiza  fedha walizokabidhiwa kutoka tawi la Samora na Kariakoo.

Amesema hawakufikisha fedha hizo makao makuu na walipanga njama za kuzipeleka Temeke kugawana.

“Walipanga njama na kuelekea maeneo ya Temeke Maduka mawili karibu na kituo cha mafuta cha Camel. Walichukua fedha zote za kuziweka kwenye gari ndogo aina ya Toyota IST iliyokuwa ikiendeshwa na Shamte.”

“Watuhumiwa hao baada ya kufanikisha uhalifu huo walitelekeza gari la kampuni ya G4S, silaha mbili mali ya G4S ikiwemo bastola moja, pia mashine ya kuhesabia fedha na muhuri wa Benki ya CBA kisha kuondoka kusikojulikana,” amesema.

Advertisement

Amebainisha baada ya kufuatilia Februari 17, 2020  walianza kumkamata  Rugemalila ambaye baada ya kupekuliwa alikutwa na Sh110 milioni, Dola 19,000 za Kimarekani na magari matano.

Mambosasa ameyataja magari hayo ni BMW ya Sh15 milioni, Toyota Runx (Sh13 milioni) na Toyota  IST tatu za Sh11 milioni kila moja.

“Mtuhumiwa baada ya kuendelea kuhojiwa alikiri tayari ameshanunua nyumba mbili na kiwanja kimoja kwa Sh107 milioni, samani za ndani za Sh5 milioni. Kwa vitu hivyo alikuwa ametumia Sh297 milioni na Dola 21,000 za Kimarekani,” amesema Mambosasa.

Amesema polisi waliendelea na upelelezi na Februari 21, 2020  waliwakamata Shamte na  Ramadhan maeneo ya Mbagala na walipokaguliwa walikutwa na Sh332 milioni, Dola 50,000 za Kimarekani, Euro 5,010 na gari aina ya IST iliyotumika kubeba fedha walizoiba.

“Watuhumiwa wote wawili baada ya mahojiano walikiri kununua viwanja viwili maeneo ya Kisemvule na Kivule kwa Sh25 milioni na kufanya jumla kuu ya mali na fedha walizotumia kuwa Sh357 milioni, dola 50,000  za Kimarekani na Euro 5010,” amesema Mambosasa

Mambosasa amesema Maunga alikamatwa Februari 24, 2020 akiwa na Sh197 milioni.

Amesema mtuhumiwa huyo alinunua nyumba Kibaha mkoani Pwani kwa Sh30 milioni na samani za ndani za Sh10 milioni, “alitumia Sh253 milioni.”

Advertisement