Profesa Lipumba awataka waliohama CUF kurejea

Wanachama na viongozi wa chama cha wananchi cuf Wilaya ya Bukoba Mjini wakiwa katika kongamano lililoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahimu Lipumba wakati wa ziara ya uimarishwaji chama hicho.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amewakumbuka waliohama chama hicho akiwemo mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kuwataka kurejea.

Kagera. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amewakumbuka waliohama chama hicho akiwemo mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kuwataka kurejea.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 23, 2019 katika kongamano lililohusisha viongozi wa wilaya,  kata, matawi na wagombea wa serikali za mitaa kutoka wilaya ya Bukoba Mjini.

"Lwakatare ni kijana wangu wa siku nyingi nilisikitika sana alivyohamia Chadema lakini bado tunaheshimiana na kuzungumza na kama akitaka kurudi CUF maamuzi ni yake.”

"Nazungumza kwa ujumla wote waliohama CUF kwa sababu moja au nyingine na kwenda vyama vingine warejee kwenye chama chao,” amesema Profesa Lipumba.

Huku akieleza jinis CUF ilivyojengwa katika msingi wa haki na usawa, Profesa Lipumba amesema, “kwa misingi hiyo tunaomba wanachama wote warejee. Tunawakaribisha  watakuwa na haki kama wanachama wengine.”

Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF,  Abdul Kambaya amesema kama kuna Mkoa ulioathirika na propaganda ni Kagera.

"Wengi hamfanyi maamuzi sahihi kwa kuwa mmekuwa mkiangalia propaganda za vyama vya siasa  na kusababisha wengi wenu kuhama bila kuelewa,” amesema Kambaya.