Rais Magufuli asema umasikini wa chakula Tanzania umepungua

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema Tanzania inaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya  kukabiliana na umasikini, akibainisha kuwa kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umasikini wa chakula nchini umepungua.

Dar es Salaam.  Rais John Magufuli amesema Tanzania inaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya  kukabiliana na umasikini, akibainisha kuwa kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umasikini wa chakula nchini umepungua.

Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf)ni kati ya mikakati iliyobuniwa ili kuziendeleza kaya masikini kujikwamua kiuchumi.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatatu  Februari 17, 2020 wakati akizindua kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf jijini Dar es Salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Rais Magufuli amesema tatizo la umaskini hususani mahitaji ya msingi ikiwamo kipato na chakula ni moja ya changamoto inayozikabili nchi nyingi duniani hasa za barani Afrika.

Amesema kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) mwaka 2015 takribani watu milioni 736 walikuwa wakiishi kwenye umasikini uliokithiri.

“Cha kusikitisha zaidi ni kwamba zaidi ya nusu ya masikini wote duniani wanaishi bara la Afrika, hii inamaanisha kwamba kwenye kila watu watatu mmoja ni masikini,” amesema Rais Magufuli.

Amesema kwa mujibu wa Benki ya Dunia ikiwa jitihada za makusudi hazitachukuliwa, ikifika mwaka 2030 asilimia 90 ya masikini wote duniani watakuwa kwenye Bara la Afrika.

“Ndugu zangu Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kukabiliwa na tatizo la umasikini, baba wa Taifa Mwalimu Nyerere (Julius) aliuita umasikini kama adui wa Taifa letu,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo,  amesema kutokana na jitihada za kupambana na umaskini zilizofanywa, hali hiyo nchini inapungua.

Rais Magufuli amesema kulingana Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 18.7 mwaka 2001 mpaka asilimia 9.5 mwaka 2017/2018.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amempongeza Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuanzisha mfuko wa Tasaf na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuendeleza.

Amesema katika kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji wa mpango huo kumekuwa na mafanikio mengi kwa jamii.

“Kupitia miradi hiyo wananchi wamenufaika kwa kupata barabara za vijijini, madarasa, nyumba za walimu, madawati, zahanati na mingine,” amesema Rais Magufuli.