Rais Magufuli azungumzia kuachiwa ndege ya Bombadier

Saturday December 14 2019

 

By Jesse Mikofu na Sada Amir, Mwananchi

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema jitihada za Serikali ya nchi hiyo ndiyo zimeifanya ndege ya aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imeshikiliwa nchini Canada kuachiwa.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumamosi Desemba 14, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza kunakofanyika shughuli ya kuipokea ndege hiyo iliyoshikiliwa tangu Novemba 2019.

"Ndege hii ilipangwa kuwasili Novemba lakini walifungua kesi ikazuiliwa," amesema Rais Magufuli

Amesema ndege hiyo ilitoka Canada usiku wa kuamkia jana Ijumaa mpaka Island ikatua kisha ikapita Jamhuri ya  Czech, Misri hadi Adis Ababa nchini Ethiopia.

"Nimeambiwa itatua hapa kwenye saa moja na ujio wa ndege hii ni dhahiri kwamba Mungu yupo nasi, tuendelee kumuomba Mungu, usafiri wa anga ni kichocheo kikubwa cha uchumi duniani kote,” amesema Rasi Magufuli huku akishangiliwa

Awali, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema wanyonyaji waliokuwa wakiibia nchi hiyo ni dhahiri wameshindwa badala yake wameanza kushika ndege.

Advertisement

Aliyesababisha Bombardier kukamatwa ni Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya dola 33 milioni.

Kesi hiyo ilisababisha Mahakama hiyo kuizuia ndege ya Tanzania aina ya  Airbus A220-300 kuondoka nchini humo Agosti, 2019.

Steyn, anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980. Hata hivyo, Septemba 3, 2019 mahakama hiyo iliamuru ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuachiwa baada ya Serikali kushinda kesi bila kutoa fedha yoyote.

 

Advertisement