Simba 19 wakamatwa Serengeti kutokana na kula mifugo ya wananchi

Muktasari:

  • Simba 19 waliokuwa wanaendelea kula mifugo ya wananchi wamekamatwa na kufanya jumla yao kufikia 36 waliokwishakamatwa maeneo ya wananchi wilayani Serengeti

Serengeti. Simba 19 waliokuwa tishio kwa wananchi na kula mifugo wamekamatwa na kikosi maalum kilichokuwa kinawasaka katika maeneo ya Nyichoka na Bukore wilayani Serengeti.
Kukamatwa kwa simba hao kunafanya jumla ya simba 36 kukamatwa katika maeneo hayo kwa mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu akizungumza leo Alhamisi Machi 26, 2020 amesema kuwa simba wa mwisho wamekamatwa jana na kufikia 19 na kuwa hakuna waliobaki eneo hilo.
"Toka mwaka jana Novemba mpaka juzi tulikuwa katika wakati mgumu sana maana kila kukicha wananchi wanapiga kelele kuwa wanyama hao wameonekana au wamekula mifugo, kwa ujumla hili ni tukio la kwanza toka historia ya uhifadhi simba 36 kuhama hifadhi na kuhamia maeneo ya wananchi," amesema.

Amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya tathimini ya mifugo iliyoliwa katika vijiji vya Robanda, Parknyigoti, Nyichoka, Bukore, Miseke, Rwamchanga, Makundusi, Nyanungu na Kwitete ili kujua idadi na kuandaa taratibu za malipo ya kifuta machozi.
Simba 17 waliokamatwa awali walipelekwa hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato na hao utaratibu unaandaliwa mahali pa kuwapeleka.