Tatizo la ukosefu wa ajira lamtisha Mkapa

Dar es Salaam. Serikali ya Awamu ya Tano iko kwenye mkakati mkubwa wa kuhakikisha uchumi wa nchi unategemea viwanda ifikapo mwaka 2025 na imeanza na miradi mikubwa ya kujenga msingi imara wa viwanda.

Ujenzi wa bwawa la Stigler’s Gorge kwa ajili ya nishati muhimu ya umeme, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kurekebisha sheria ili kuondoa urasimu katika uwekezaji, ununuzi wa ndege ili kurahisisha usafiri wa ndani na nje na mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma.

Mengine ni ununuzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu, ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi na kutenga maeneo maalum ya kiuchumi.

Matatarajio katika matokeo ya hayo yote ni pamoja na ongezeko la ajira, tatizo ambalo linaonekana kukua kadri idadi ya watu inavyoongezeka.

Na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameonyesha hofu pia ya tatizo hilo hasa kwa vijana ambao wengi wanazagaa mitaani bila ya kuwa na shughuli maalum.

“Ninatishika kwa kweli ninavyoona vijana wengi wakiwa mitaani bila ya kuwa na shughuli ya kufanya na kibaya zaidi hakuna mipango ya haraka ya kukabili tatizo lao la ajira,” anasema Mkapa katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” alichozindua mapema wiki hii.

Mkapa anasema nchi lazima ije na mipango endelevu kukabili tatizo la ajira kwa vijana na hasa wale wanaohitimu vyuo na shule mbalimbali.

Mkapa anasema kuwa aligundua ukubwa wa tatizo hilo katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuonya kuwa litakuwa ajenda kubwa ya mustakabali wa taifa katika chaguzi zijazo kutokana na ongezeko la idadi ya vijana.

Mkapa anasimulia kwenye kitabu chake kuwa kwa macho yake alishuhudia vijana wengi zaidi kwenye mikutano ya kampeni mwaka 2015 ukilinganisha na wazee.

“Hii maana yake ni kuwa vijana ndio watakuwa na sauti katika chaguzi zijazo. Ajenda zao kama zile za tatizo la ajira lazima zifanyiwe kazi na kupata majawabu,” anasema Mkapa.

Takwimu za ongezeko la vijana

Akiweka hoja yake katika takwimu, Mkapa anasema wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 vijana wenye umri kati ya 15 na 34 walikuwa milioni 16.

“Idadi hiyo ya vijana milioni 16 inakadiriwa kuwa mara mbili ya idadi ya watu wazima,” anasema Mkapa ambaye wakati huo alihutubia katika ufunguzi wa kampeni za mgombea wa CCM, John Magufuli.

Mkapa anasema inakadiriwa kutakuwa na vijana milioni 23 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 ifikapo mwaka 2025.

“Wataalamu wa mambo ya idadi ya watu wanadai kutakuwa na ongezeko kubwa la vijana kwenye uchaguzi wa mwaka 2025. Hii inaashiria kuwa vijana ndio watakuwa na sauti kwa mustakabali wa nchi,” anasema Mkapa na kuongeza kuwa mwaka huo idadi ya Watanzania inaweza kufikia watu milioni 67.

Tatizo la ajira lilijidhihirisha mwaka 2017 wakati watu 56,000 walipojitokeza kuwania nafasi 400 za ajira zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Mwaka huo, watu 6,740 walijitokeza katika usaili wa kutafuta watu 47 kwa ajili ya kuajiriwa Shirika la Viwango (TBS).

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi uliofanywa na Shirika la Takwimu (NBS) mwaka 2014, watu 23,000 (sawa na asilimia 10 ya nguvukazi), hawana kazi.

Ili kulikabili tatizo hilo, Mkapa anaishauri Serikali iwe na programu madhubuti za kukabiliana na suala hili la ongezeko la watu.

Anatoa mfano wa kipindi cha utawala wake alipokumbana na tatizo la ongezeko la watu wakati alipoingia madarakani mwaka 1995.

Wakati huo kulikuwa na watu milioni 27.4 ila mwaka 2005 wakati anaondoka, walifikia milioni 36.1, ikiwa ni ongezeko la asilimia 31.7.

Anaeleza kuwa lazima Serikali iwe na majibu katika suala la kukabili tatizo la umaskini, elimu bora, afya na maji safi na pia kutatua tatizo la ajira.

Mkapa pia amesema anaona kuna tatizo la ukuaji wa maendeleo ya nchi, ambao hauendi sambamba na ongezeko la watu, akisema ni tatizo kwa nchi nyingi Afrika.

Hali ilivyo ya tatizo la ajira

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imewahi kueleza namna ambavyo tatizo la ajira kwa vijana lilivyo kubwa nchini, ikisema hali hiyo pia imechangiwa na sekta ya umma na binafsi kuwa na nafasi chache.

Inakadiriwa kuwa vijana wapatao milioni 1.2 huingia katika soko la ajira baada ya kuhitimu vyuo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alikaririwa hivi karibuni akisema idadi hiyo kubwa ya vijana inahitaji ajira wakati nafasi za kazi ni finyu.

Rais John Magufuli alisema mwaka 2016 kuwa tatizo la ajira kwa vijana litaendelea kupatiwa ufumbuzi hatua kwa hatua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sera ya Tanzania ya uchumi wa viwanda inatekelezwa kwa vitendo baada ya Serikali kuanza kuchukua hatua za kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi.