UN Women waiomba Tanzania kutoa elimu huduma za biashara

Muktasari:

  • Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women) limeiomba Serikali ya  Tanzania kutoa elimu na huduma za biashara kuanzia ngazi ya kata na halmashauri ili kuwainua kiuchumi wafanyabiashara wadogo hasa wanawake

Dar es Salaam. Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women) limeiomba Serikali ya  Tanzania kutoa elimu na huduma za biashara kuanzia ngazi ya kata na halmashauri ili kuwainua kiuchumi wafanyabiashara wadogo hasa wanawake.

Akiwasilisha taarifa kuhusu sera ya biashara ndogo katika mkutano wa wadau wa biashara ulioandaliwa na shirika hilo na  Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Aurelia Kamzola amesema elimu na huduma bora za biashara zitasaidia wanawake kupiga hatua katika maendeleo.

Amesema asilimia 54 ya wanawake wanajishughulisha na biashara ndogo lakini hazikui kutokana na mtaji wao kuwa mdogo.

“Katika utafiti wetu tulioufanya tulibaini pia changamoto zinazokwamisha biashara nchini, tumebaini wananchi wengi hawana uelewa katika masuala ya kodi,  kila unayemuuliza anakwambia hajui hasa hawa wafanyabiashara wadogo.  Bila  kuwa na uelewa mzuri kuhusu  kodi biashara yako haiwezi kupiga hatua.”

“Lakini pia tumebaini biashara za Tanzania zinabaki kuwa ndogo huku mitaji yao siyo ya kuridhisha,”amesema.

Mkurugenzi wa biashara na viwanda na biashara ndogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara,  Consolatha Ishebabi amesema mkutano huo umekuja wakati muafaka wakati Taifa likielekea katika uchumi wa kati.

Amesema UN kwa kushirikiana na Serikali wamejipanga kutatua changamoto za biashara kwa wanawake nchini ili waweze kukuza kipato chao na uchumi wa Taifa.

Naye mkurugenzi mkazi UN Women,  Hodan Addou amesema shirika hilo litaendelea kuwezesha wanawake katika nyanja mbalimbali bila kujali dini, rangi wala kabila.