VIDEO: Undani wa ajali ya moto Hoteli ya Coco Beach, gari la zimamoto lapata ajali likielekea kuuzima

Muktasari:

Buhatwa amesema moto huo umeanza kuwaka kati ya saa 7:00 mchana katika Ukumbi wa juu uliokuwa umesitisha ujenzi wake. Katika jengo hilo la ukumbi, hakukuwa na umeme uliounganishwa wala shughuli zilizofanyika

Dar es salaam. Juhudi za kuokoa madhara zaidi katika tukio la kuteketea Hoteli ya Coco Beach zimeingia kirusi baada ya gari la zimamoto lililokuwa inakwenda kusaidia kupata ajali ,kona ya Kanisa la Mtakatifu Peter.

Hoteli hiyo iliyopo Coco Beach imeanza kuteketea kwa moto kuanzia saa 7:30 mchana.

Mmiliki wa hoteli hiyo, Alphonce Buhatwa ameiambia MCL DIGITAL leo Septemba 22, 2019 Jijini Dar es salaam kuwa ,asilimia 80 ya mali zote katika hotel hiyo zimeteketea.

Buhatwa ameanza kufanya biashara katika ufukwe huo tangu mwaka 1994, na baadhi ya biashara zilizofanyika katika hoteli hiyo ni Maduka ya bidhaa za nguo, vinyago, vyakula,kukodisha ukumbi na vinywaji.

Buhatwa amesema moto umeanza kuwaka katika Ukumbi wa juu uliokuwa umesitisha ujenzi wake. Hakukuwa na umeme uliounganishwa wala shughuli zilizofanyika.

Chini ya ukumbi huo uliowaka moto, kuna huduma za kanisa la Dar es salaam Christian Fellowship, ambao hukutana Kila jumapili kusali.

Waumini wa kanisa hilo wakiwamo raia wa kigeni katoka Nchi mbalimbali, wameonekana wakiokoa vifaa vya muziki na meza kutoka dani ya Ukumbi.

"Ibada tumeanza saa 2:30 hadi saa 6:00 mchana na tukaondoka waumini wote ila Kijana wetu hapa Lucas Manyama alipoona moto akaanza kutoa vitu nje, kwa hiyo tunaondoa vitu kuhifadhi mahali pengine, "amesema Angela Scott, raia wa Afrika kusini anayeishi hapa Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu makadirio ya thamani ya Mali zote katika hotel hiyo, Buhatwa amesema: "Siwezi kusema thamani ya mali, ni jambo linalofanyiwa uchunguzi lakini Ukumbi ninakodisha sh1.4 milioni kwa siku.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Musa Taibu amesema uchunguzi wa tukio umeanza na hakuna taarifa zozote za awali kuhusu uhakika wa chanzo cha moto.

Hata hivyo uchunguzi wa Mcl Digital kutoka kwa watu wa karibu eneo la tukio, umebaini chanzo kinaweza kuhusishwa na hujuma zilizofanywa na watu waliopanga tukio hilo.

Baada ya kuulizwa kuhusu Mazingira ya hujuma za watu wasiojulikana kufanya tukio kwa nia ovu,  mmiliki huyo amekiri akisema mazingira yanaonyesha huenda ikawa ni tukio lililopangwa.

"Sigara kwa bahati mbaya haiwezi kuwasha makuti yaliyojengewa katika Ukumbi huo, nadhani pengine kuna mtu amedhamilia kufanya hivyo, "amesema Buhatwa.

Ajali ya gari la zimamoto

Katika Juhudi za kuzima moto uliokuwa Ukiendelea kuathiri katika eneo hilo, gari la zimamoto lililokuwa limebeba lita 8000 za maji limepinduka, eneo la Mbuyuni kona ya kanisa la Mtakatifu Peter.

Kamanda wa Zimamoto Katoka Manispaa ya Kinondoni, Jenifer Shirima amesema gari hilo limepata ajali wakati dereva akiwahi kuzima moto katika hotel hiyo.

"Hili lilikuwa ni gari la tatu lililokuwa linapeleka tripu ya nane kuzima moto  dereva Elisha Mwamugiga ameumia mkono na amepelekwa hospital,"amesema Kamanda Jenifer.