Usiponunua kifurushi cha mawasiliano umeumia

Wakati idadi ya Watanzania wanaotumia intaneti ikiongezeka, gharama za kununua data zinatofautiana kati ya kampuni moja na nyingine lakini unafuu upo kwenye vifurushi.

Taarifa za Mamlaka ya Mawasilino (TCRA) za robo mwaka iliyoishia Septemba 2019 zinaonyesha kila kampuni hutoza kiasi tofauti kwa anayetumia salio bila kujiunga na kifurushi.

Wateja wa Vodacom kwa mfano hulipa Sh205 kwa kila megabyte (MB) moja ya intaneti wakati wale wa Zantel wakitozwa Sh93 kwa kila MB moja.

Wanaotumia mtandao wa Airtel wanalipa sawa na wale wa Tigo, Sh29 kwa MB moja wakati Halotel inawatoza wateja wake Sh22. Wateja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wanalipa Sh10 huku wa Smile wakitozwa Sh5 kwa kiasi hicho cha data. Gharama hizi ni bila kodi.

“Kati ya Julai na Septemba, kulikuwa na ongezeko la wateja 517,186 hivyo kuwa na jumla ya watumiaji milioni 44.7,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Katika wateja wapya waliosajiliwa katika kipindi hicho, Vodacom inayoongoza sokoni ilikuwa ya pili kwa kupata wengi zaidi baada ya kuvuna watu 207,771 ikiwa nyuma ya Airtel iliyowapata 337,688. Tigo ilifuata katika orodha hiyo kwa kupata wateja wapya 108,950 halafu TTCL 88, 695 na Smile 654.

Hali ilikuwa mbaya kwa Halotel na Zantel ambazo zilipoteza sehemu ya wateja iliokuwa nao. Wakati Halotel ikipoteza wateja 197,644 Zantel iliwapoteza 28,928.

Pamoja na ukweli huo, Vodacom ndio kampuni yenye wateja wengi zaidi nchini (zaidi ya milioni 14.8) sawa na asilimia 33 ya watumiaji wote wa simu za mkononi nchini.

Kutokana na tofauti kubwa ya gharama za data iliyopo baina ya watoa huduma, mkurugenzi wa masuala ya sekta wa TCRA, Dk Emmanuel Manase anasema wajibu wao ni kuwajuza wananchi ili wafanye uamuzi wakiwa na taarifa sahihi.

“Kwenye vifurushi hawatofautiani sana. Hizi ni gharama kama hujajiunga kifurushi. Wewe umefahamu ukweli, kila mtu akifahamu itasaidia kufanya uamuzi sahihi,” anasema mkurugenzi huyo.

Dk Manase anafananisha bei ya data na tofauti iliyopo kwenye sekta ya hoteli kwamba samaki unayeweza kumla kwa Sh5,000 kwenye mgahawa wa kawaida mtaani unaweza kumpata kwa fedha nyingi ukienda hoteli ya kitalii.

“Kila mteja anaenda anakotaka. Na kabla hujala unapewa ‘menu’ uchague utakachoweza kukilipia,” anasema.

Ukinunua kifurushi, takwimu za TCRA zinaonyesha utalipa kati ya Sh21 hadi Sh62 kupata dakika moja ya kupiga simu, MB moja ya intaneti na ujumbe mfupi mmoja.

Kaimu mkuu wa kitengo cha bidhaa na huduma za mteja wa Vodacom, Celvin Mmasy anasema kiasi kikubwa cha wateja wananunua vifurushi wanapotaka kutumia intaneti.

“Asilimia 99.97 ya wateja wote wananunua vifurushi. Ni asilimia 0.03 tu ndio hutumia salio lililomo kwenye simu zao. Bei za vifurushi zinalingana kwa kampuni nyingi,” anasema Mmasy.

Takwimu za TCRA zinaonyesha mpaka mwaka 2018 kulikuwa na zaidi ya watu milioni 23.1 wanaotumia intaneti huku wengi zaidi (milioni 22.2) wakifanya hivyo kupitia simu za mkononi.

Wateja wa mawasiliano wanasema hawakujua kama kuna makato makubwa kiasi hicho na mara nyingi walikuwa wanashangaa kuona salio limeisha ndani ya muda mfupi.

“Kama hujazima data, ukiweka salio la buku (Sh1,000) ni kufumba na kufumbua limeisha. Unaweza ukakasirika kwa kuamini umeibiwa kumbe ni haya makato ya MB,” anasema Msafiri Joseph, mteja wa huduma za simu jijini Dar es Salaam.

Vifurushi

Kwa vifurushi, taarifa ya TCRA inaonyesha kuna tofauti kwa wanaojiunga kwa ajili ya kuwasiliana ndani ya mtandao na wanaofanya hivyo kwenda mitandao mingine.

Mpaka robo ya tatu ya mwaka jana, kifurushi cha Halotel kilikuwa nafuu zaidi kwani mtaja alipaswa kulipa Sh21 kupata dakika moja ya mawasiliano, MB moja na ujumbe mfupi wa maneno ndani ya mtanda huku wale wa Zantel wakilipa Sh58.

Wateja wa Tigo walilipa Sh21 wakati wale wa Vodacom wakilipa Sh31 na Airtel Sh41.

Wakati wastani wa kifurushi cha kupiga ndani ya mtandao kikigharimu kati ya Sh21 na Sh58 kile cha nje ya mtandao ni kati ya Sh33 na Sh62.

Wateja wa Tigo wanalipa kidogo zaidi, Sh33 wakati wale wa Zantel wakitozwa Sh62. Airtel wanakata Sh54 wakati Vodacom wakitoza Sh52 na Halotel Sh42 kufanikisha mawasiliano nje ya mtandao.