Vikao vya Bunge vinavyoanza kesho kuendeshwa kidijitali

Muktasari:

  • Bunge la 11 kesho kuhamia katika Bunge Mtandao, pamoja na mambo mengine, imeelezwa mfumo huo unakwenda kuokoa Sh1bilioni kwa mwaka zilizokuwa zikitumika katika uchapishaji wa nyaraka mbalimbali.

Dodoma. Bunge litaanza kutumia Bunge Mtandao katika Mkutano wa 17 unaoanza kesho jijini ambao utapunguza gharama zilizokuwa zikitumiwa na mhimili huo kwenye uchapishaji wa nyaraka mbalimbali kutoka Sh 1.2bilioni hadi Sh 200milioni kwa mwaka.

Akizungumza leo Jumatatu Novemba 4, 2019 baada ya maelekezo kwa wabunge kuhusu matumizi ya Tablets (Vishikwambishi), Katibu wa Bunge Stephen Kigaigai amesema mfumo huo utaokoa fedha zilizokuwa zikitumiwa na Bunge pamoja Serikali.

“Wizara zinazohusika tumezitaka zije na karatasi kiasi kwa ajili ya kumbukumbu za ofisi. Kwa maana ya maktaba na baadhi ya maeneo kwa hiyo kwa kesho tunaanza Mpango wa Serikali nadhani tutakuwa na nakala ambazo hazitazidi 10 zamani walikuwa wakileta nakala 500, ”amesema kigaigai.

Kigaigai amesema wamenunua Tablets 450 zenye  thamani ya zaidi ya Sh900 milioni ambazo zitagawiwa kwa wabunge na makatibu wa bunge.

Amesema mfumo huo utakuwa ukitumika wakati wa vikao vya Bunge na kamati zake.

Akijibu maswali ya wabunge, Mtalaam wa Tehama wa Bunge Lilian Mraba amesema kwasasa mfumo huo utafanya kazi ndani ya viwanja vya Bunge.

“Tunawaahidi kwamba Bunge lijalo tutakuwa tumeboresha mfumo wetu ili uweze kupatikana nje ya viwanja vya Bunge,” amesema.

Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge amewataka wabunge kukubali mabadiliko kwa sababu ni lazima yatokee.

“Sasa hii chachu iliyoanzishwa na Bunge inahamia kwenye vyombo vingine vya Serikali ipunguze gharama hii ya paper work ambayo tumeilea kwa sababu ambazo hazieleweki,” amesema.

Mbunge wa Kilolo (CCM) Venance Mwamoto, amesema hatua hiyo haipunguzi tu gharama bali na usumbufu wa kupata majibu yanayotakiwa kwa haraka katika taasisi mbalimbali.

“Spidi yetu itakuwa kubwa zaidi kuliko mwanzo nafikiri waende mbali sasa kwenye shule za sekondari na baadaye kwenye za msingi kwa sababu katika maeneo mengi sasa kuna umeme,” amesema.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema walikuwa wanasubiri kwa hamu vifaa hivyo kwa sababu tangu wameingia bungeni mwaka 2015 waliahidiwa wangepewa.

“Mwanzoni tulikuwa tukipewa kwa njia ya makaratasi ripoti na nyaraka mbalimbali kwa kweli. Kwa njia hii itakuwa kuwa kikirushwa kitu wote tunapata. Italeta ufanisi wa juu katika Bunge letu tunamshukuru sana mheshimiwa spika kwa kazi nzuri aliyoifanya,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Lucy Owenya ameomba hatua hiyo isiishie hapo bali iende hata kwa madiwani wanaotumia fedha nyingi kwenye makaratasi na gharama za usafirishaji.

“Katika halmashauri zetu wanatumia hadi saa tatu kusambaza nyaraka mbalimbali.  Wakiweza kupatiwa hizi Tablets tutaweza kusave fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Joyce Sokombi amesema wamefurahia sana mpango huo na kwamba mbali na kupunguza gharama itawasaidia kupunguza makabrasha waliyorundika majumbani.

“Ukija nyumbani utakuta makabrasha mengi yamelundikana lakini hii haina haja ya kubeba makabrasha. Uongozi wa Bunge niusifu kwa kweli pale ambapo pale panapostahili tutoe pongezi,” amesema.