Waliokimbia na Sh1.2 bilioni za wakulima wa korosho Mtwara wasakwa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara kuwakamata  viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wanaotuhumiwa kukimbia na Sh1.2 bilioni za wakulima wa korosho.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara kuwakamata  viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wanaotuhumiwa kukimbia na Sh1.2 bilioni za wakulima wa korosho.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Oktoba 25, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Newala katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya stendi kuu.

Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea ripoti ya jumla ya madeni wanayodai wakulima hao katika Wilaya za Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba.

“Nilivyofika Mtwara jambo la kwanza nilimuuliza kamanda wa Polisi wa hapa kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais (John Magufuli) alilolitoa siku za hivi karibuni alipokuwa katika  ziara na kuagiza kukamatwa kwa viongozi wawili wa vyama vya msingi vya ushirika  wanaodaiwa fedha za korosho na wakulima.”

“Akanieleza kuwa walitekeleza agizo na hao viongozi  wawili tayari wameanza kulipa hizo fedha,” amesema Masauni.

 

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya madeni kwa Wilaya zote, Masauni amewataka polisi kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobakia za Mtwara, Newala, Masasi, Nanyumbu na Tandahimba ambazo katika taarifa ya jumla inaonyesha Sh1.2 bilioni bado zinadaiwa na wakulima hao.

“Rais kwenye ziara yake aliishia wilaya ya Masasi lakini katika ripoti hapa inaonyesha wilaya nyingine wakulima pia wanadai fedha zao nyingi. Nakuagiza Kamanda wa Polisi wakamate viongozi wengine katika wilaya zilizobaki na hakikisha kiasi hicho cha fedha kinalipwa,” amesema Masauni.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chitanda inaonyesha vyama vya ushirika 61 vinadaiwa na wakulima katika wilaya za Mtwara, Masasi, Tandahimba na Newala kuanzia msimu wa korosho wa mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018.