VIDEO: Warioba apigilia msumari ukomo wa urais

Butiama. Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi na wananchi kuendeleza utaratibu wa kupokezana vijiti ili kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, akiwaambia kuwa wakiona mabadiliko ya kuondoa ukomo yanafanywa, basi wajue “kiongozi wa juu ndiye ana uchu wa madaraka”.

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo katikati ya mjadala wa ukomo wa urais ambao umekuwa ukijadaliwa mara kwa mara siku za karibuni.

Rais John Magufuli ameshasema hana mpango wa kuendelea kukaa madarakani baada ya muda wake kuisha, lakini hiyo haijatosha kuzuia mjadala kuhusu kuongeza muda wa urais na sasa kuondoa kabisa ukomo.

Kuanzia wakati mbunge wa Nchemba, Juma Nkamia alipotaka kuwasilisha hoja binafsi ya kuongeza muda wa urais kutoka miaka mitano kwenda miaka saba, hadi mkulima Desdellius Patrick Mgoya kuhoji mahakamani tafsiri ya ibara inayomzuia mtu aliyeshika urais kwa vipindi viwili kugombea tena, mjadala huo sasa unakua taratibu.

Mjadala huo ulikuwa ukiibuka na kuzimika na kuibuka tena, lakini umeanza kushika kasi baada ya Mgoya kufungua kesi hiyo ya kuhoji ukomo wa urais katika Mahakama Kuu.

Pengine kutokana na matukio hayo ndio maana jana mwenyekiti huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliamua kuzungumzia suala la ukomo wa urais na umuhimu wa kupokezana vijiti.

Jaji Warioba alikuwa miongoni mwa wazungumzaji mjini Butiama jana katika kongamano maalumu la kuelezea maisha ya Mwalimu Nyerere lililopewa jina la ‘Nilivyomfahamu Nyerere’.

Jaji Warioba, ambaye amewahi kuwa waziri mkuu wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili, alisema muasisi huyo wa Taifa aliyefariki Oktoba 14, 1999, aliamini katika falsafa ya kubadilisha uongozi wa juu kwa kuasisi utaratibu wa kupokezana kijiti kupitia ukomo wa uongozi.

Warioba, ambaye pia amewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais, alisema marais waliomtangulia John Magufuli pia walikuwa wakiombwa waongezewa muda, lakini walikataa.

Marais hao ni Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

“Ukiona kuna mabadiliko (ya Katiba kuondoa ukomo), ujue kiongozi wa juu ndiye ana uchu wa madaraka kutaka kusalia madarakani,” alisema mwanasheria huyo mkuu wa zamani.

“Hoja ya kubadili Katiba kuondoa ukomo haikuanza leo. Iliibuliwa wakati wa Mzee Mwinyi, ikaja tena wakati wa Benjamini Mkapa katika Awamu ya Tatu na hata kipindi cha Jakaya Kikwete. Lakini wote walikataa na kuondoka madarakani muda wao ulipoisha kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

“Hata sasa wameanza kusemasema, lakini bahati nzuri Rais John Magufuli ameshasema wazi kuwa hataki. Nadhani tuendeleze utaratibu huu kumuenzi Mwalimu Nyerere.”

Jaji Warioba, ambaye anasema alimfahamu Mwalimu Nyerere akiwa na umri wa miaka 12, anaamini kuna haja ya kujenga utamaduni wa kubadilisha viongozi wa juu.

Jaji Warioba aliwaambia washiriki wa kongamano hilo lililoongozwa na mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima kuwa asili ya utaratibu wa kukabidhiana vijiti ulianza kwa wazo la Mwalimu Nyerere mwenyewe wakati wa mkutano mkuu wa Tanu mwaka 1975 alipokubali kwa shingo upande kugombea tena urais.

Alisema ilipofika mwaka 1980, wajumbe walimshinikiza tena Mwalimu Nyerere kuendelea kubaki madarakani kutokana na hali halisi ya wakati huo baada ya vita vya Kagera na kwamba licha ya kukubali aliwapa masharti kuwa hiyo ingekuwa awamu yake ya mwisho

“Wakati anaachia uongozi (1985), Mwalimu Nyerere alikuwa na madaraka makubwa na alikuwa akipendwa na watu, lakini aliamua kuondoka,” alisema Jaji Warioba.

Alisema Mwalimu Nyerere alionyesha tabia ya kutopenda wala kung’ang’ania madaraka tangu mwaka 1962 alipojiuzulu uwaziri mkuu na kukabidhi madaraka kwa Rashid Kawawa (marehemu) ili aende kuimarisha Tanu.

Sifa za Nyerere

Akitaja baadhi ya sifa za Mwalimu Nyerere, Jaji Warioba alisema kiongozi huyo hakutaka kujikweza, utukufu wala kuonekana mtu tofauti na binadamu wengine.

“Alijishusha na kuwa mwananchi wa kawaida. Alipiga marufuku kuitwa mtukufu Rais na badala yake akaagiza aitwe mwalimu au ndugu. Hata mke wake hakutaka aitwe first lady bali Mama Maria na ndivyo anavyojulikana hadi leo,” alisema.

Jambo jingine alilotaja kuonyesha kutojikweza kwa Mwalimu Nyerere ni uamuzi wake wa kupiga marufuku taarifa za habari kwenye vyombo vya habari na utangazaji vya umma kuanza na habari inayomhusu Rais.

Wakati Jaji Warioba akizungumzia kuheshimu ukomo kumuenzi Mwalimu Nyerere, makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Phillip Mangula alizungumzia jinsi muasisi huyo wa Taifa alivyojenga msingi wa uongozi ikiwemo kuwajengea uwezo kupitia mafunzo maalumu ya chuo cha uongozi Kivukoni.

“Mwalimu Nyerere kwa jinsi alivyopenda na kuthamini elimu alihakikisha siyo wananchi wa kawaida pekee wanaridhishwa, bali hata viongozi walifundishwa na kujengewa uwezo,” alisema Mangula

“Aliasisi wazo na kulitekeleza kwa kujenga chuo cha mafunzo ya uongozi Kivukoni kwa lengo la kupika na kuwaandaa viongozi,” alisema.

Mangula alisema tofauti na kipindi cha Mwalimu Nyerere, sasa viongozi hawapikwi kiasi cha kila mmoja kujiibukia na mambo yake mwenyewe.

“Ili kuepuka makosa ya viongozi wa chini, Mwalimu Nyerere alihakikisha viongozi wanafundishwa kanuni, miiko, majukumu na dhamana ya uongozi na malengo ya Serikali.” alisema Mangula.

“Baada ya kutoka chuo, walipelekwa wilayani (vijijini) kuishi na wananchi kujifunza kwa vitendo maisha halisi ya watu kabla ya kupangiwa na kusambazwa kwenye vituo vya kazi,” alisema.

Kuchukia umaskini

Katika mjadala huo, Stephen Wasira, mmoja ya viongozi waliofanya kazi kipindi kirefu chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, alisema kiongozi huyo alichukia umaskini hadi kuutangaza kuwa adui wa Taifa na kuhimiza kila mmoja kupambana nao kwa kuchapa kazi.

“Lakini hakupenda utajiri wake binafsi. Alitaka watu wote waishi maisha mazuri kwa kila mmoja kupata makazi bora, elimu na huduma ya afya kutokana na kufanya kazi kwa bidii,” alisema Wasira.

Tofauti na viongozi wengine wa Kiafrika, alisema Mwalimu Nyerere hakutumia madaraka yake kujilimbikizia mali ndiyo maana kwa maisha yake yote alijenga nyumba moja ndogo ya kawaida kijijini kwake Butiama huku mengine yote akifanyiwa na watu wengine pamoja na Serikali.

“Aliishi maisha yanayofanana na anachoamini ndiyo maana hakujilimbikizia mali. Angetaka angekuwa kiongozi tajiri kuliko wote Afrika na hata duniani kutokana na utajiri wa madini uliopo nchini,” alisema.

Akizungumzia vyama vya ushirika wakati wa Nyerere, alisema vilikuwa imara na bora kwa sababu vilitokana na hiari ya wakulima wenyewe, lakini vikaharibiwa na baadhi ya viongozi waliokabidhiwa dhamana na kutaka kujinufaisha badala ya wakulima.

Mdahalo huo wa jana ambao uliendeshwa na mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima na kurushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), ulitoa nafasi kwa wananchi na viongozi kuuliza maswali kwa wastaafu ambao walipata nafasi ya kufanya kazi na Mwalimu.

Maswali na majibu

Katika maswali hayo, mwenyekiti wa CCM wa Mara, Samuel Kiboye aliuliza tofauti ya mfumo wa uongozi kwenye chama na Serikali iliyopo kati ya kipindi cha Mwalimu na uongozi wa sasa.

“Mwalimu Nyerere wakati anaongoza, naona watu walikuwa wamenyooka sana, kuna tofauti gani kati ya wakati ule na wakati huu hasa kwenye chama na Serikali,” aliuliza Kiboye.

Akijibu swali hilo, Mangula alisema “mwenyekiti tofauti ipo. Kama nilivyosema Mwalimu aliamini katika masomo kwa viongozi, kwa sasa hawaendi masomoni. Kwa hiyo kila mtu anaenda kwa utaratibu wake, anabuni mwenyewe namna ya kuendesha shughuli zake, hakuna utaratibu wa pamoja wa namna ya kuchukua mafunzo” alisema Mangula huku akicheka.

Pia, alisema Mwalimu Nyerere alisisitiza mafunzo ya vitendo kwa viongozi kuliko nadharia.

“Pili, alikuwa anasema msiwafundishe tu nadharia viongozi waende wakakae vijijini. Hivyo walikuwa wanaenda vijijini wanakaa mwezi mzima na wananchi,” alisema.

Mwingine aliyeuliza swali kwenye kongamano hilo ni aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alitaka kujua sababu za mwalimu kutaifisha shule. “Mzee Mangula, nadhani ulikuwa mwalimu na Mwalimu alitaifisha shule. Hebu tueleze kidogo unadhani ilikuwa ni nini,” aliuliza Profesa Muhongo ambaye ni mbunge wa Musoma Vijijini

Mangula akisema lengo la Mwalimu Nyerere kutaifisha shule lilikuwa ni kujenga utaifa

“Moja, alikuwa ana jitihada za kujenga utaifa maana shule zilikuwepo za wazungu, Waasia na tuligawanywa katika makundi kwa wanafunzi waliomaliza shule mbalimbali. Akaamua hapana hebu tuondoe hii, akataifisha zile shule zote zikawa za Taifa, wote wanatoka popote wanaenda kusoma popote,” alisema Mangula.