Wazazi, ndugu waongoza kwa kuwafanyia ukatili watoto-Ripoti

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),  Anna Henga (kulia), Mkurugenzi Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji wa kituo hicho, Felista Mauga na Balozi Mdogo wa  Norway,  Hans Corneliussen wakionyesha nakala za Vitabu vya Ripoti ya Haki za Binadamu nchini ya Mwaka 2018 baada ya kuzinduliwa jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Dar es Salaam. Ukiukwaji wa haki za watoto unaendelea kushika kasi nchini, kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inayoonyesha wazazi na ndugu wengine ndio wahusika wakuu wa kufanya vitendo hivyo.

Ripoti hiyo ya haki za binadamu ya mwaka 2018 iliyozinduliwa jana inaonyesha ongezeko la ukatili dhidi ya watoto kutoka matukio 4,728 mwaka 2017 hadi 6,376 mwaka 2018.

Mbali na ukatili dhidi ya watoto, ripoti hiyo inaonyesha kuvunjwa kwa haki tano muhimu ambazo ni pamoja na haki ya kuishi, uhuru wa kujieleza, usawa mbele ya sheria, usalama wa mtu na haki ya kutoteswa.

“Lililozidi ni ukatili dhidi ya watoto na asilimia 80 ya matukio yanafanywa na wanafamilia kama baba, mama, mjomba shangazi,” alisema mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga.

“Ni matukio machache yalifanywa na watu wa nje.”

Henga alisema ukatili huo dhidi ya watoto ni pamoja na wa kingono, kulawitiwa na kubakwa, matukio ambayo hufanywa na ndugu.

Akifafanua zaidi kuhusu ukubwa wa tatizo hilo, naibu msajili wa mahakama, Nyigula Mwaseba alisema katika kuzingatia haki za watoto, wamechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutunga kanuni na kutoa miongozo ya haki ya mtoto.

Hata hivyo, alisema tatizo hilo linachangiwa na Idara ya Ustawi wa Jamii kushindwa kuwasilisha ripoti za kesi za watoto.

“Tunaomba ikiwezekana kamishna awawezeshe maofisa ustawi wa jamii ili litekelezwe,” alisema Mwaseba. Alisema wanapata taarifa kutoka maeneo ya wilayani kuhusu matukio hayo, lakini ustawi wa jamii wanashindwa kuwapelekea taarifa.

“Sheria ya mtoto iko wazi, lakini wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo tunaomba ikiwezekana kesi zote za ulinzi na usalama wa watoto ziletwe mahakamani,” alisema.

Juhudi za kuwapata Wizara ya Afya inayohusika na ustawi wa jamii hazikufanikiwa.

Mbali na watoto, suala jingine lililomo kwenye ripoti hiyo ni haki ya kufanya siasa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni na kujumuika. Wakili Pacience Mlowe wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alisema ukandamizwaji unatokana na kutungwa kwa sheria kandamzi.

“Leo tunakuwa na sheria inayoruhusu kufanya siasa, lakini anatoka mtu mwingine anatunga sheria ambayo inaingilia hadi wanachama wa chama husika,” alisema.

“Mimi mwanasheria nina leseni ya kufanya kazi, lakini anakuja mtu na kutaka niwe na kibali cha kufanya kazi?”

Kuhusu haki za kijamii, Patrick Kinemo wa taasisi ya Sikika, alisema japo Serikali imejitahidi kuwa na mipango, changamoto iko kwenye utekelezaji.

“Kuna sera ya afya inayofanyiwa upembuzi, lakini hadi sasa wananchi wenye bima ya afya ni asilimia 33 tu,” alisema.