Waziri aishauri Ufaransa kufundisha Kiswahili kwenye vyuo vyao

Sunday December 15 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Vyuo vikuu nchini Ufaransa vimeshauriwa kuweka somo la Kiswahili katika mitaala yao ili wanafunzi wa nchini humo waweze kujifunza lugha hiyo.

Hayo yamesemwa jana Desemba 14, 2019 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, alipokuwa akifungua  mkutano kati ya vyuo vikuu vya Tanzania na vyuo vikuu vya Ufaransa, uliofanyika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere.

Mkutano huo wa siku moja ulionendana na maonyesho kutoka vyuo mbalimbali, lengo lake kuu ilikuwa kuendeleza mahusiano ambayo yapo katika sekta ya elimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Ole Nasha amesema Ufaransa imekuwa rafiki wa muda mrefu na Tanzania huku ikitaka watu wanaoenda kufanya kazi kwao au kusoma wazungumze lugha yao.

‘Kama mnavyojua marafiki huzungumza lugha moja kama wanavyotaka sisi tuongee Kifaransa na mimi nimeomba mufundishe Kiswahili kwenu.

“Hivyo Balozi nakuomba upeleke pendekezo hilo kwenu  na kama ni walimu tutawapatia kwa kuwa tunao wa kutosha,” amesema.

Advertisement

Kwa upande wake balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier, amesema  zaidi ya watu 500,000 kutoka nchi za kigeni husoma nchini Ufaransa na kati yao wapo waliopatiwa ufadhili wa masomo ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo, Clavier alisema udhamini wa msomo huo kwa mwaka mpya wa masomo kwa upande wa Tanzania umeongezeka kutoka wanafunzi 30 hadi 50, na kuwasihi wanaotoka kwenda kusoma huko kuchangamkia fursa hiyo.

“Watu 50 sio wachache, naomba wanafunzi waliopo hapa wasisite kutuma barua za maombi kwani huwezi kujua na kama mnavyojua mbali ya kusoma huko Ufaransa kuna fursa pia za ajira,” amesema.

Amesema masomo wanayofundisha ni pamoja na kilimo, mazingira, uhandisi, hesabu na  masuala ya afya.

Balozi huyo amesema mkutano huo ambao umewakutanisha zaidi ya wanafunzi 900, wanapata fursa ya kupata taarifa juu ya kozi zinazotolewa Ufaransa na kupata fursa ya kupata udhamini wa kusomeshwa.

Amesema kupitia makampuni hayo wanaweza kupata ajira kutokana na aina ya kozi ambazo wanafunzi hao wamesomea hivyo ni mkutano muhimu kwa Tanzania.

Advertisement