Waumini wa kikristo watakiwa kuchukua tahadhari sikukuu ya pasaka

Unguja. Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi imewataka waumini wa dini ya kikristo kufanya ibada na kusherehekea sikukuu ya Pasaka kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maaambukizi ya maradhi ya corona.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Hassan Khatib Hassan ameeleza hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari  ofisini kwake Vuga kuelekea sikukuu ya Pasaka.
Amesema waumini hao wana wajibu wa kufanya ibada na kusherehekea sikukuu, hivyo ni vyema tahadhari za makusudi zikachukuliwa kuepusha mkusanyiko kulingana na hali ya maradhi ilivyo.
“Sisi kama viongozi wa Serikali tunajua umuhimu wa ibada na sikukuu hii na Serikali ipo pamoja nao lakini mazingira si salama sana kwa hivyo tunawaomba wenzetu wafanye ibada kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya na mara tu ya kumaliza ibada warudi nyumbani kuepusha mikusanyiko maana usalama wa afya zetu ni jambo la kipaumbele maradhi yakiisha tutaendelea kusherehekea sikukuu mbali mbali,”amesema.
Hassan amewasisitiza viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya kikristo kusimamia na kutekeleza maelekezo hayo ya Serikali kwa kuwaelimisha waumini wao juu ya madhara ya maradhi ya corona na kuacha nafasi baina ya waumini wakati wakiendelea na ibada sambamba na kusherehekea sikukuu hiyo wakiwa nyumbani na kuacha mialiko na kuongeza idadi ya watu katika nyumba.
Amesisitiza umuhimu kwa waumini hao kuepusha mikusanyiko mara baada ya sala na kuwataka viongozi wa dini kufupisha muda wa mahubiri na sala huku mahubiri  yao yakielekeza katika utoaji wa elimu juu ya maradhi hayo ikiwa na lengo la kuchukua tahadhari ya kuwakinga waumini na maradhi.
Hata hivyo amesema serikali ya mkoa kupitia kamati ya ulinzi na usalama itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kipindi hichi cha sikukuu na kuwataka wananchi kubaki nyumbani pale wanapomaliza shughuli zao za msingi.