Ongezeko la wasomi wasio na ajira latajwa changamoto nchini Tanzania

Friday October 11 2019

Kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Anga

Kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremi. 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ongezeko la vijana wasomi wasio na ajira imeelezwa kuwa  kati ya changamoto kubwa za usalama nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremi.

Amesema kila mwaka watu 900,000 wanaingia katika soko la ajira nchini wakati fursa zilizopo ni kwa watu 50,000 hadi 60,000.

Ametoa kauli hiyo katika kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Tanzania, mwalimu Julius Nyerere linalofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Brigedia Mkeremi amesema viwango vya juu vya ukosefu wa ajira hufanya washiriki katika vitendo vya uhalifu.

"Mfano ugaidi unafanywa na vijana wasio na ajira na ambao kimsingi wanaweza kushawishiwa kwa urahisi kujiunga na makundi hayo," amesena Brigedia Mkeremi.

Advertisement

Amesema Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limekuwa likiwafundisha vijana elimu ya kujitegemea, “tunawafundisha vijana tunatoka wapi tupo wapi na tunaenda wapi.”

Amesema mwalimu Nyerere aliamini kuwa amani na usalama wa Taifa haviwezi kutenganishwa na maendeleo, haki za binadamu na haki za jamii.

"Kwetu sisi mwalimu Nyerere  bado hajafa na wala hajafariki ni wazi atabaki kuwa shujaa katika kupanga mikakati inayolihakikishia Taifa amani, ulinzi na usalama," amesema.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema elimu ya kujitegemea ina thamani na ni muhimu kuwa na mitaala inayoendana na mazingira itakayo wasaidia vijana kujiajiri.

 

Advertisement