Jay Melody anatoa changamoto kubwa tuzo za TMA

Muktasari:

  • Hiyo ni kutokana na hakuna wimbo mwingine wa Bongo Fleva uliofanya vizuri na kuandika rekodi kubwa kwa mwaka 2023 kama ulivyofanya huo wa Jay Melody ambao katika TMA 2022, ulizibwaga nyimbo za wakali kibao.

Katika tuzo za muziki Tanzania (TMA) mwaka huu, Jay Melody anawapa changamoto wasanii wenzake katika kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka 2023, ambacho alikishinda msimu uliopitia kupitia wimbo wake, Nakupenda (2022).

Hiyo ni kutokana na hakuna wimbo mwingine wa Bongo Fleva uliofanya vizuri na kuandika rekodi kubwa kwa mwaka 2023 kama ulivyofanya huo wa Jay Melody ambao katika TMA 2022, ulizibwaga nyimbo za wakali kibao.

Katika kinyanganyiro hicho ambapo tuzo zilitolewa Machi 2023, Jay Melody ulizibwaga nyimbo kama Pita Huku (Dulla Makabila), Nitaubeba (Harmonize), Kwikwi (Zuchu) na Mwamba (Rayvanny).

Utakumbuka tuzo za TMA zilianzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata), chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, mwaka 2003 zilipata mdhamini na kujulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA), hadi ziliposimama.

Tuzo hizo ambazo zilirejea mwaka 2021 baada ya kusimama tangu mwaka 2015, bado hazijatolewa kwa mwaka huu ambapo watawatunza wasanii waliofanya vizuri kwa mwaka 2023 ukiwa ni msimu wa tatu tangu kurejea kwake.

Wimbo huo wa Jay Melody, Nakupenda (2022) uliotoka Julai 20, 2022, ndiyo uliofanya vizuri kuliko wowote ule kwa mwaka huo, na kwa asilimia 100 ulistahili kushinda TMA kama Wimbo Bora wa Mwaka 2022.

Mathalani, ndiyo wimbo wa Bongo Fleva uliosikilizwa zaidi Boomplay ambapo ulimaliza mwaka ukiwa na 'streams' zaidi ya milioni 50 na kuiacha mbali EP ya Diamond Platnumz, First of All (FOA), iliyotoka Machi 11, 2022 ikiwa na nyimbo 10.

Hadi sasa ndiyo wimbo uliosikilizwa zaidi Boomplay kwa muda wote ukiwa na 'streams' zaidi ya milioni 80.5, kwa lugha rahisi, Tanzania hii na Afrika Mashariki yote kwa ujumla, hakuna wimbo wa msanii yeyote wenye namba za juu kama huo.

Kwa matokeo hayo, mnamo Septemba 2023, Jay Melody aliandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha 'streams' milioni 200 katika jukwaa la Boomplay bila kutoa albamu wala EP.

Utakumbuka wasanii wote wa Bongo Fleva wenye 'streams' zaidi milioni 200 Boomplay ambao ni Diamond, Rayvanny, Harmonize, Mbosso na Zuchu, walishawahi kutoa albamu au EP, ila Jay Melody alifika huko bila vitu hivyo viwili.

Na siyo Boomplay tu, hata YouTube wimbo huo una rekodi yake, mathalani ndiyo wimbo pekee wa Bongo Fleva ambao 'lyric video' yake imesikilizwa zaidi kwa muda wote ambapo hadi sasa ikiwa na 'views' zaidi ya milioni 30.6.

Kwa muktadha huo, kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka wa TMA 2023 kina changamoto sana maana hakuna wimbo uliofanya vizuri kwa mwaka huo kama wa Jay Melody, Nakupenda.
Utakumbuka Jay Melody aliwahi kuwa chini ya Tanzania House of Talent (THT) alipotoka kimuziki na wimbo wake, Goroka (2018), huku jina hilo akipewa na aliyekuwa msimamizi wa THT, marehemu Ruge Mutahaba.

Kuna kipindi alipotea kabisa kimuziki hadi aliporejea kwa kishindo na wimbo wake, Huba Hulu (2021) kisha zikafuata nyimbo kali kama Najiweka (2021), Sugar (2020), Nakupenda (2020), Nitasema (2023), Sawa (2023) na Baridi (2023).

Ameshiriki kuandika nyimbo za wasanii wengi, mfano ndiye msanii aliyemwandikia Nandy nyimbo nyingi zaidi na zote zikafanya vizuri, nyimbo hizo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018) ft. Willy Paul, Hallelujah (2019) ft. Willy Paul na Do Me (2020) ft. Billnass.