Sugu alivyowakutanisha mabalozi watano usiku wa Bongo Fleva Honors

Muktasari:

Ulikuwa ni zaidi ya usiku wa kidiplomasia baada ya tamasha hilo kuhudhuriwa na mabalozi watano, ni ufunguzi wa bongo fleva honors msimu wa pili

Dar es Salaam. "Usiku wa burudani ulivyogeuka kuwa wa kidiplomasia." Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya tamasha la Bongo Fleva Honors kuwakutanisha mabalozi watano kwa pamoja.

Tamasha hilo linalohusisha wasanii wa zamani wa muziki wa bongo fleva linaandaliwa na mwanamuziki mkongwe na mwanasiasa, Joseph Mbilinyi maarufu 'Sugu' lilifanyika jana usiku Januari 26, 2024 na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo wanadiplomasia.

Pia, wafanyabiashara na wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Godbless Lema walijitokeza katika ukumbi wa Alliance Francaise Upanga jijini Dar es Salaam. Ni tamasha la ufunguzi wa msimu wa pili lililotumbuizwa na msanii Lucas Mkenda (Mr Nice).

Mabalozi waliohudhuria tamasha hilo ni Michael Beatle kutoka Marekani), Christine Grau (Umoja wa Ulaya EU)), Nabil Hajalaoui (Ufaransa), Peter Huyghebaert (Ubelgiji) na Jorge Moragas wa Hispania.

Wasanii waliohudhuria ni Raymond Shaban maarufu Rayvanny na Webiro Wasira maarufu Wakazi.

Tamasha lilianza saa 1. 23 usiku kwa muandaaji Sugu kutumbuiza na kuwakaribisha wahudhuriaji kisha kufuatiwa na msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Mr Nice kabla ya kupanda Khalid Mohamed maarufu TID aliyekiwasha kuanzia saa 5: 48 hadi saa 6.02 usiku.

Baada ya kuisha tamasha hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Sugu aliwatambulisha mabalozi hao waliohudhuria na kuwashukuru kwa uwepo kushiriki kwao pamoja na kummpongeza Mr Nice kwa kutumbuiza katika uzinduzi huo wa msimu wa pili wa tamasha hilo.

"Congratulations (hongera) Mr Nice kwa concert (tamasha) la jana ulikonga sana nyonyo za watu mzee wa takeu," amesema Sugu kwenye ukurasa wake wa Instagram

Mwananchi Digital limezungumza na Sugu aliyewahi kuwa mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) juu ya tamasha hilo na kusema “kwangu mimi sishangai, haya mambo yataendelea kuwepo na hayatokei kwa bahati mbaya. Mabalozi watano na wanadiplomasia zaidi ya 15 kushiriki si kazi ndogo.”

“Hawa ni wakubwa na watu muhimu, kwa nafasi zao wana mambo mengi ya kufanya lakini kutenga muda na kuja wanaonyesha wamethamini na kuamua kuja. Ni njia moja ya kutangaza kimataifa sanaa yetu na kudumisha mahusiano kupitia sanaa,” amesema Sugu.

“Sasa wale wanaosema Sugu ni muhuni kwa sababu ni mwanamziki na mpaka kesho ninapofanya mambo ya maana ya wananchi na siasa wananihusisha na uhuni, mazingira kama haya yanawakataa. Kuwakutanisha wanadiplomasia wote hawa ni heshima sana kwangu.”

Kwa upande wake, Miriam Joseph miongoni mwa wahudhuriaji wa tamasha hilo amesema hatua ya wanadiplomasia kushiriki tukio hilo ni ishara chanya kwa ukuaji wa muziki wa bongofleva na kuaminika kwa Sugu.

"Unajua hawa mabalozi siyo rahisi kuwapata katika matukio ya kiburudani hii inamaanisha wanathamini muziki wa bongo fleva na unazidi kukua.

"Lakini lazima tumpongeze Sugu kwa kuweza kuaminika na wanadiplomasia na jumuiya za kimataifa," amesema Miriam.