Wanamuita Sugu ‘The Legend’

Sunday June 05 2022
SUGU PIC

Rais Samia Suluhu Hassan akimpa Tuzo msanii wa muziki wa HipHop nchini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ya kuthamini mchango wake katika sanaa na kuzalisha ajira kabla ya kuzindua kitabu cha msanii huyo.

By Dk Levy

Kila kitu kilikuwa ni shoo. Ungeweza kutoa kiingilio ili uwatazame viumbe waliohudhuria pale. Ungeweza kutoa kiingilio ili uweze kumuona kwa ukaribu Mkuu wa Nchi. Na ungeweza kulipa kiingilio ili uwashuhudie binadamu wa daraja la kwanza wanaoishi hapa Bongo. 

Vyote ungelipa na wala usingejutia. Kila kitu kilikuwa ni shoo. Eneo alipo Rais, mawaziri, mabalozi na vigogo wa kampuni kubwa na wa taasisi za Serikali na binafsi. Binadamu maarufu wa fani zote mpaka ‘Tivu Ake’. Unataka nini zaidi? Yaani ilikuwa ni zaidi ya Super Bowl. 

Kila kitu kilikuwa ‘klasiki’, kilikuwa ‘supa’ na zaidi vilifanywa kwa wakati. Kamati ya maandalizi mpaka leo ina ‘hangover’ za pongezi. Kuna wakati watu hustahili heshima kuliko pesa. Na heshima hizi hupewa binadamu mwenye mtazamo chanya kwa jamii yake.

‘Lokesheni’ yenyewe ni shoo kamili ile. Tunaongelea ‘Faivu Staa hoteli’ ‘Ladezi endi Jentromeni’. Matukio ya namna hii huwa yanatokea kila baada ya miaka 50. Serikali kuu kukaa eneo moja na ‘wahuni’ na kufuta rasmi dhana ya hip hop ni uhuni. Saluti!

Imeisha hiyo na ndio neno rafiki na rahisi kulitamka katika mchongo wa andiko la leo. Sasa ni hivi: Hii haijawahi kutokea wala kutegemewa. Na huenda isitokee tena kwa kizazi hiki.

Ni jioni ya Mei 31, 2022 na tukio moja tu la kiburudani, likafanya nchi nzima ielekeze macho eneo moja. Pale Serena Hotel katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Yes! Ilijengwa upya historia nyingine kwa muziki wa ‘kihuni’. Hii ni kubwa sana.

Advertisement

Ni Joseph Osmund Mbilinyi, ‘2 Proud’, ‘Mr 2’, ‘Sugu’, ‘Jongwe’ na sasa muite ‘Taita’. Alisherehekea miaka 30 ya uwepo wake kwenye muziki wa kizazi kipya. Na pia akisherehekea kutimiza miaka 50 ya kuishi duniani. ‘Mchizi’ kakata nusu karne mjue sio mchezo. ‘Taita’ huyu kutoka kitaa cha Sae pale Green City. Mwenye mikato na ‘swaga’ za Mwanjelwa (‘Njelii). Leo ‘mhuni’ huyu kamuinua ‘Madam Prezidenti’ pale Ikulu ya Magogoni na kutimba katika shoo ya muziki wa ‘kihuni’ (hip hop). Usichukulie poa. 

Muziki ulioitwa wa kihuni. Taji Liundi na wenzake wakihatarisha vibarua vyao kwa kuupiga pale Radio One. Ilikuwa miaka ya 90 mwanzoni kabisa. Leo hii raia namba moja na Amiri Jeshi Mkuu. Anakuwa mgeni rasmi kwenye shoo hii.

Nani awasimulie hili tukio masela wetu. Kama Nigga One, D Rob, Geez Mabovu, Complex, Father Nelly, Langa, Ngwea na wengi waliotangulia mbele za haki? Ule muziki wa ‘kihuni’ uliopondwa na wazazi wao, leo hii mkuu wa nchi anahudhuria shoo zake na kueleza mambo mazito yenye maslahi makubwa kwa vizazi vilivyopo na vinavyokuja.

Wakati zamani shoo za hip hop zilipambwa kwa marashi ya ganja kuanzia kwa mashabiki hadi wasanii wenyewe. Hii shoo ya juzi ilipambwa na manukato ya gharama mwanzo mwisho.

Hapa Sugu pale Jide, AY na FA. Kulia Joh Makini na Niki wa Pili. Kuna G Nako na Lord Eyes. Hawa kwa sasa siyo wale wa miaka kumi nyuma. Ina maana kubwa hata jukwaani pale kulikuwa na ‘kokteli’ ya manukato. ‘Machizi’ hip hop wa sasa wananukia uturi na ni mabishoo haswa na pesa inapumua.

Shoo ya ‘Kitaita’ muziki mzuri na ‘saund’ yenye usikivu. Wageni wengi walioingia pale shoo za Sugu wakiwa sekondari na sasa waliingia wakiwa mabosi kwenye kampuni, idara na taasisi za Serikali na binafsi. Hii kitu amazing sana.

Na hapa ndipo ulipo mtaji wa Sugu. Kila anakopita anakutana na watu wa aina hii. Anaingia benki anakutana na msela akiwa na ‘waifu’. Anaambiwa ‘Huyu ni ‘waifu’ niliwahi kuja naye kwenye shoo yako pale Mango Park Moro, wakati huo tukiwa wapenzi tu tukisoma Mzumbe.” Hao ndo mashabiki wa Sugu na ndio waliojaa pale Serena. Wakikumbukia zama zile pindi wakiwa wavulana au wasichana. Kipi cha kusema zaidi ya ‘kumbukizi bora’?

Shoo ya kwanza nchini Rais wa nchi akiwa mgeni rasmi na kuwakutanisha wanasiasa wakubwa. Alikuwepo Mama Samia, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe meza moja.

Ndio shoo ya kwanza kuwakutanisha mabosi wengi wa wizara na taasisi za Serikali. Mabalozi na watu mashuhuri. Hata ‘Big Man’ Jenerali Ulimwengu alikuwepo ndani ya nyumba. Na kile kilichovutia zaidi ni Rais na wasaidizi wake kuiongelea hip hop wakionyesha wameiishi na wanaijua. Ilivutia sana.

Mawaziri Nape Nnauye na Mohamed Mchengerwa. Bosi Nehemia Mchechu kutoka NHC, Majid Nsekela wa CRDB na mnene wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga.

Wote wamefanya kazi na Sugu, siyo wageni kwake kabisa. Kisiasa, kimuziki na kibiashara. Ni watu wanaomfahamu Sugu na kile anachofanya. Ndo maana hakukuwa na kigugumizi wakati wanatoa madini yao. ‘Lijendari’ ‘Mr T’ Taji Liundi, aliongoza shoo kwa kipaza na ‘Lijendi’ Dj Bonny Love kwenye mashine akisugua santuri.

Huu ulikuwa ubatizo wa moto kuonyesha maana halisi ya ‘Lejendi’. Hizi mishe ni za Sugu tangu na tangu na tangu ya tangu. Ndio maana siku zote amekuwa wa kwanza kwenye lolote linalohusu muziki huu wa kizazi kipya.

Sugu ni wa kwanza nchini kwa muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’ kuugeuza kutoka kujifurahisha na kuwa biashara, wakati wazazi wao wakiuita ni muziki wa kihuni, yeye akawa anapiga pesa kupitia muziki huu.

Wakati wengi waliwahi kurekodi kabla yake, lakini yeye akaja kwa miguu miwili kwa kutoa albamu ya kwanza ‘Ni Mimi’ na kuiingiza sokoni kuuza ‘tepu’ zake viunga vya Coco Beach na kwingine. Aliamini katika ndoto zake na hapa ndipo watu wakaanza kumjua. 

Wapo waliorekodi albamu kabla, lakini hakuishia kujifurahisa magetoni na washikaji wa Mbagala. Alipeleka bidhaa yake mitaani na kuwaonesha kwamba haya ni maisha kamili. Ni ndoto ambayo leo hii imetimia na kuvuka matarajio yake na huku mtaani madogo wanapiga pesa tu.

Kwa maana nyingine albamu yake ya kwanza tu, ilitosha kuugeuza muziki wa ‘kihuni’ kuwa biashara kubwa. Katika hili la muziki wa Bongo Fleva ‘mchizi’ yupo dunia ya peke yake. Ni zaidi ya ‘Lejendi’, ndo maana alijiita Nyerere wa Rap, kwa wakati ule alimaanisha na ikawa kweli.

Leo hii wakati wasanii wengi wanapiga shoo nje ya nchi, Sugu alikuwa msanii wa kwanza Bongo kufanya shoo Ulaya. Tena kwenye majukwaa makubwa yale ya Festival. Mwaka 1998 alipanda jukwaa moja na staa kutoka Zimbabwe ya Mugabe, Oliver Mutukuzi (RIP), kule Stockholm- Sweden. 

Shoo hii ndo ilimfanya wafahamiane rasmi na marehemu James Dandu, ambaye wakati ule alikuwa akiishi huko. Mwaka huohuo 1998, Sugu aliwaleta wanamuziki wa Hip Hop, toka Marekani wa kundi la Lost Boys.

Nyakati zile wanamuziki wa kutoka nje waliokuwa wanaletwa Bongo wengi walikuwa kutoka DR Congo (Zaire) na ‘Sauzi’ kidogo.

The Lost Boyz ni kundi la muziki wa hip hop kutoka Jamaica, Queens, New York, Marekani likiongozwa na MC Mr. Cheeks, MC mdakiaji na promota Freaky Tah (1971–1999), DJ Spigg Nice na Pretty Lou.

Wakati leo hii wanamuziki wanarekodi video huko Afrika Kusini, mwaka 1999 Sugu akawa mwanamuziki wa kwanza kurekodia albamu nzima Ulaya. Albamu iliitwa ‘Nje ya Bongo’, ndani yake kukiwa na dude lililokimbiza sana la Deiwaka.

Wakati Profesa Jay anaibuka na Chemsha Bongo mwaka 2000 na Hard Blasters, tayari Sugu alikuwa na albamu tano mtaani. Ni mimi, Ndani ya Bongo, Niite Mr Two, Nje ya Bongo na Millenia. Na mwaka 2001 akaachia albamu ya sita Muziki na Maisha. Kila mwaka ilikuwa kitu juu ya kitu.

Wasanii kama Profesa Jay, waliona fursa ya sanaa ya muziki huu kupitia Sugu na ndio maana hakuona hatari kuachana na kazi yake kule Tanga na kuamua kujikita jumla jumla kwenye muziki na katika hili Sugu ni kama ‘greda’ lao alishakwangua barabara.

Wakati leo wanamuziki wa kizazi kipya ‘wakipushi’ mikoko ya maana mjini na wengine wakihonga pisi kali ndinga za maana. Miaka 22 iliyopita Sugu alikuwa mwanamuziki wa kwanza kwa kizazi hiki kununua gari kwa pesa za muziki, siyo gari tu, lilikuwa la kifahari.

Ni mwaka 2000 alimiliki mkoko aina ya Honda Inspire na ndio sababu ya mstari wa kwenye ngoma ya ‘Wanakuita Sugu’. Siasa za muziki zilipotamalaki, 2002 jamaa akasepa zake Ulaya. Lakini, huku nyuma alituachia albamu ya saba ya Itikadi na humo ndio kuna dude lile la ‘Wanakuita Sugu’. Mwaka 2003 akaachia albamu ya ‘Sugu’  yenye pini la ‘Moto Chini’. 

2004 akawa mwanamuziki wa kwanza kuandaa kungamano kubwa la muziki likiitwa Hip Hop Summit, hili lilikuwa kongamano la elimu ya muziki kuwa ni ajira. Elimu iliyotolewa ilikuwa kubwa sana, huku wahadhiri kadhaa toka pale UDSM wakishusha nondo kibao.

Yote haya aliyafanya kwa sababu ya kupenda muziki huu na kuuheshimu na aliamini kuna maisha na utajiri mkubwa kupitia muziki huu. Leo hii kila mtu shahidi kwa kuwatazama madogo wa sasa. Wanapita kwenye barabara iliyochongwa na Sugu.

Mwaka 2010 akawa mwanahip hop wa kwanza kuwania na kupata ubunge na katika hili Profesa Jay amekuwa mwanafunzi mzuri kupitia Sugu. Toka kwenye muziki mpaka kwenye siasa anapita njia zile zile anazopita Sugu.

Baada ya miaka mitano yote Sugu kutamba peke yake kimuziki, Profesa Jay akawa mwanamuziki wa pili kuanza kutoa albamu mfululizo. Na kwenye siasa baada ya miaka mitano ya ubunge wa Sugu, Profesa Jay naye akajitosa kwenye siasa na kutoboa vilevile.

Na baada ya Jay kuanza kutoa ngoma na albamu kama Sugu, ndipo kina FA na wenzao wakaaminishwa kuwa hata wao wanaweza. Hata ajira zao benki wakazipiga kapuni. Na kwenye ubunge baada ya Sugu na Jay kina Mwana FA nao wakaona siyo kesi wakazama na kushinda. 

sasa ni Sugu tena kwenye The Dream Concert ambayo Rais Samia alisema majina na matukio ya Sugu huwafanya wengi kuamini kuwa jamaa ni mtukutu. Lakini, Rais Samia akawaaminisha watu kuwa, yeye alikuwa na Sugu pale bungeni anafahamu kuwa siyo mtukutu ni mtu mwema.

‘Mchizi’ kafanya makubwa mengi nje ya muziki. Hip Hop Summit, Malaria No More, hata mambo aliyofanya jimboni kwake. Yatakupa picha kuwa huyu ni zaidi ya kile unachomuwazia. Mbeya hawakuwa wajinga kumpa ubunge kwa kura nyingi zaidi ya wabunge wote nchini. 

Hata kuutazama muziki huu miaka 30 nyuma kuwa ni mchongo, ni suala la upeo na kukisimamia unachokiamini. Kutokukata tamaa wala kuyumbishwa na dawa ya ndoto siyo kuziota tu, ni kuzifanyia kazi.

Kwa wanaomfahamu toka kitambo hawakushangaa kumuona anaingia kwenye siasa mwaka 2010. Wale ambao Rais, alisema kuwa wanamtafsiri vibaya Sugu kwa jina na matukio. Ndiyo hao hao walioona kama kadata hivi kutaka kugombea ubunge, lakini wananchi wa Mbeya Mjini wakawapa majibu kama ambayo Rais Samia amewapa juzi usiku. Huyu ndio Joseph Osmund Mbilinyi a.k.a Sugu The Legend.

Advertisement