Angel Nyigu amejipata, anapiga mkwanja wa maana kupitia video

Muktasari:

  • “Kupitia kazi yangu ya ‘dansi’ niliwahi kupata fedha nyingi kwa mara ya kwanza Sh50 milioni na ilikuwa kwa ajili ya kazi ya ‘influncer’, kwa kweli nilifurahi ilinipa nguvu zaidi ya kuendelea kufanya kazi,” amesema.

Mambo ya kucheza kwa kujifurahisha siku hizi hakuna tena, kuna watu wanapata maisha na kuzunguka sehemu mbalimbali duniani kupitia dansi pekee, miongoni mwao ni Angel Nyigu amba-ye, anakumbuka fedha ya kwanza kubwa kuishika kutokana na kazi yake ni Sh50 milioni, huku akitembelea nchi zaidi ya 10.

Angel, dansa maarufu ambaye hucheza katika video za wasanii mbalimbali hasa wa Bongofleva, miaka ya hivi karibuni ameonekana katika video nyingi za Zuchu kama Sukari, Kwikwi, Nani Remix, Honey n.k.

Huyu ni mzaliwa wa Njombe akitokea katika familia ya watoto 10. Punde tu alipohitimu kidato cha nne jijini Dar es Salaam alijikita katika ‘kudansi’ ambako amefanikiwa sana kwa kushinda tuzo za ndani na nje.

Akizungumza na gazeti hili, Angel Nyigu amesema hadi kuchukua uamuzi wa kuingia kwenye ‘dansi’ ni kutokana na kuvutiwa na wanenguaji kutoka nchi mbalimbali ambao aliwafahamu kupitia mitandao ya kijamii.

Mwanzo alikuwa anapenda kucheza na watu wanafurahia kipaji chake, ndipo akasikia wakisema akiendelea kucheza vizuri anaweza kupata fedha huko mbele, basi akaona aifanye dansi kuwa kazi yake rasmi tangu wakati huo.

“Kazi hii naipenda, ningependa kuona hata watoto wangu wanaifanya kwa misingi ambayo nimeifuata. Dansi imeniletea faida nyingi kwa miaka siyo chini ya saba au minane, nimekuwa naishi maisha mazuri na nimepata mashabiki zaidi ya milioni 5,” amesema.

“Kupitia kazi yangu ya ‘dansi’ niliwahi kupata fedha nyingi kwa mara ya kwanza Sh50 milioni na ilikuwa kwa ajili ya kazi ya ‘influncer’, kwa kweli nilifurahi ilinipa nguvu zaidi ya kuendelea kufanya kazi,” amesema.

Amesema mwaka 2016 ndipo alianza ‘kudansi’ katika video za muziki na hadi sasa tayari amefanya video takribani 30, huku wasanii wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz na Zuchu wakiwa wanufaika wakubwa wa kipaji chake.

“Kwa Diamond nafikiria nimedansi katika video zake nne au tano, ambazo nazikumbuka ni za nyimbo kama Jeje, Iyo na Sound akimshirikisha Ten. Na kwa Zuchu nyimbo zote ambazo zilikuwa zinahusiana na ‘dansi’, basi nilikuwepo kwa sababu mimi ni dansa wake rasmi,” amesema.

“Mimi na Zuchu tunafanya kazi vizuri, ni mtu wa kujitoa sana na ninafurahia kufanya kazi naye kwa sababu yupo makini kwenye kazi yake, anafanya kazi yake inavyotakiwa na kila kitu kinakuwa sawa,” amesema Angel.

Ukiachana na Diamond na Zuchu, Angel anawataja wasanii wengine wa Tanzania ambao amewahi kufanya kazi nao ni pamoja na Vanessa Mdee, Harmonize, Rayvanny, Mimi Mars na Rosa Ree. 

Licha ya kusafiri  katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kutumbuiza, kujifunza na kutangaza kazi yake, Angel kuna mataifa ambayo anatamani kurejea na mengine kuyatembelea kwa mara ya kwanza.

“Nimesafiri nchi nyingi, siyo chini ya 10, Ulaya nimetembelea nchi sita, ila ambazo ningetamani kurudi ili kuendelea kutangaza kazi zangu ni baadhi ya zile za Ulaya ambazo sijafika pamoja na Marekani. Kuna nchi za Afrika kama Nigeria, Afrika Kusini, pia Ghana ambayo sijawahi kufika,” amesema.

“Ziara yangu ya Ulaya mwaka uliopita lengo lake lilikuwa ni kufundisha ‘dansi’ na kuongeza maarifa kwa kuingia katika madarasa ya watu wengine, hilo ndiyo lilikuwa lengo kubwa namshukuru Mungu nilifanikiwa,” amesema Angel.

Mwaka uliopita Angel alishinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) kama Mchezaji Bora wa Kike 2023, huku akiwa na tuzo mbili za kimataifa kutoka Kenya na Afrika Kusini. 

“Binafsi kila nikishinda tuzo naona kabisa siku hizi ‘dansi’ inaheshimika na ndiyo sababu tunawekwa kwenye tuzo kubwa kama TMA, hii inaonyesha ni jinsi gani wanaheshimu kile tunachofanya,” amesema Angel.

Angel pia ni muanzilishi wa jumuiya ya Tanzania Dance ambayo imejikita katika kufundisha dansi watu wazima na watoto na tayari wamewafikia watu takribani 500 ambao huja na kuondoka. 

“Niliianzisha ili kuwezesha wengine kufuata nyayo zangu kutokana na ufundishaji wangu, yaani kushirikishana ujuzi, mimi nilikuwa najifunza mtandaoni na nikatamani hiki kitu kifanyike katika nchi yangu.

“Kumfundisha mtoto dansi ni rahisi sana kama amependa kitu hicho kutoka akilini mwake, ni rahisi kuliko kumfundisha mtu mzima kwa sababu ana mambo mengi ila mtoto anafanya kitu unachomuelekeza,” amesema Angel.

Idadi kubwa ya ‘madansa’ kutoka Tanzania Dance walishiriki katika ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 2023.

Angel amesema kupata dili hilo katika tukio hilo la kihistoria ni kitu cha kujivunia kwao kwa sababu lengo lake ni kuwapa kazi ‘madansa’ wengi hapa nchini kadiri wawezavyo.

“Tulipata kazi ya kutumbuiza uzinduzi wa AFL lakini nilikuwa kwenye ziara wakati wa maandalizi, niliporudi nilikuwa nawasimamia kuhakikisha wanafanya vitu vinavyotakiwa na kupata malipo yao, hivyo nilikuwepo pale kama mwakilishi wa Tanzania Dance,” amesema.

“Nilipata hiyo kazi kutokana na marafiki ninaojuana nao, kuna marafiki wapo Dubai hao ndiyo waliniunganisha na kampuni ambayo ilikuwa inahusika na uandaaji wa ufunguzi wa AFL,” amesema Angel. 

Dansa huyo amekiri kuwa mitandao wa kijamii ina mchango mkubwa katika kazi yake kwa kuwa inawasaidia kuwafikia walengwa wengi zaidi bila kukutana nao. 

“Kazi yangu bila mitandao kuna kitu kinakuwa kinapungua kwa asilimia kubwa, kwa kupitia mitandao nimeweza kupata kazi nyingi zikiwemo za ‘influencer’ (matangazo), kazi ambayo inahitaji ushawishi katika mitandao ya kijamii,” amesema.

Angel Nyigu amesema mwaka huu amejipanga kuanzisha vitu vipya na kuendeleza vilivyokuwepo, huku akisisitiza kaulimbiu yake kwa miaka yote ambayo ni “sikubali kurudi nyuma”.