Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ANKO KITIME: AI italeta furaha na vilio katika anga za utunzi wa muziki

Muktasari:

  • Juzi nilikuwa naongea na msanii maarufu ambaye ana wimbo ambao kwa sasa haukosi kupigwa hewani mara tatu kwa siku. Kizazi chake wanasema ametoka. Nilikuwa na maswali machache kwa ‘supastaa’ huyu.

Dar es Salaam.Utunzi wa muziki unapitia mageuzi kaatika kila zama. Ukianzia na zama za muziki wa asili ambao chombo pekee cha muziki ulikuwa mwili wa msanii. Mdomo wake, mikono, miguu na kadhalika. Ikaja enzi ya vyombo vilivyotengenezwa kwa ajili ya muziki, ngoma, marimba, zeze na kadhalika. Lakini kila mara mtunzi alikuwa mwa-namuziki mwenye kipaji. Lakini tumeingia zama ambazo si lazima uwe mwanamuziki kutunga muziki mzuri. Teknolojia ya Akili Mnemba (AI), sasa inawezesha anaejua kuitumia anaweza kutengeneza kazi za sanaa japokuwa si msanii. Hakika yajayo yatafurahisha kwa wengine lakini yanatisha kwa wana sanaa na wapenzi wa sanaa za asili.

Juzi nilikuwa naongea na msanii maarufu ambaye ana wimbo ambao kwa sasa haukosi kupigwa hewani mara tatu kwa siku. Kizazi chake wanasema ametoka. Nilikuwa na maswali machache kwa ‘supastaa’ huyu. Nilipokuwa nausikiliza wimbo wake nilipenda sana uimbaji wake lakini nilikuwa shida kuelewa mpangilio wa vyom-bo katika muziki huo, hivyo nilitaka kujua aina ya vyombo alivyotumia na  pia kujua alikuwa ana sababu gani kutumia vyombo hivyo.

Kifupi tu alishangaa swali hilo na alikuwa hana jibu. Alisema aliyepanga hivyo vyom-bo si yeye bali producer wake. Jibu lake lilinirudisha nyuma sana wakati nikiwa katika bendi miaka ya 80 jinsi tulivyokuwa tukitunga na hatimae kurekodi nyimbo, hakika taratibu zilikuwa tofauti. Katika zama hizi msanii hutunga ‘mistari’ yake na kufanya mazoezi ya kuuimba peke yake kisha huingia studio ambako ‘producer humtengenezea muziki au maarufu ‘beat’ kutoka hapo wimbo huenda hewani.

Hali ilikuwa tofauti sana huko nyuma.  Labda nirudishe picha miaka ya 80 mwishoni nilipokuwa bendi ya Tancut Almasi iliyokuwa na masikani yake Iringa.  Mwanamuziki yoyote mwenye uwezo wa kutunga aliruhusiwa kutunga wimbo, watunzi walikuwa wa aina tofauti, watunzi maarufu  mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa walikuwa wakitunga nyimbo zao kwa pamoja, na kwa kuwa Kasaloo alikuwa akijua kupiga gitaa,  mapacha hawa walikuwa wakileta wimbo ambao umekwisha pangwa sauti za uimbaji na hata magitaa ya kusindikiza, ambayo waliyaimba kwa mdomo, na hivyo kurahisisha kidogo utengenezaji wa wimbo mzima. Lakini watunzi wengine walikuja tu na mashairi na kutegemea watu wengine watunge sauti na kupanga vyombo.

Lakini kitu cha kwanza ambacho  kilikuwa kinafanyika kwa tungo yoyote ile,  ilikuwa ni mtunzi kuyasoma mashairi yake mbele ya watu wote, na hapo mashairi yalianza kuchambuliwa  kuona kama yalikuwa na mistari iliyoleta maana na kama mistari hiyo ilikuwa katika Kiswahili fasaha, na  pia yaliangaliwa maadili katika tungo hiyo. Kama bendi imekubaliana ndipo mtunzi alianza kufundisha alichokitunga.  Baada ya hapo waimbaji walianza kupangiana sauti ili kuleta muafaka katika wimbo huo.

Wakati huo mpiga gitaa mmoja mara nyingi mpiga gitaa la rhythm, alikuwa akisindikizana na waimbaji ili kuanza kujenga njia za wimbo huo.  Baada ya hapo wapiga magitaa wote walikaa pembeni na kupanga magitaa yao kwa kufuata njia ambazo mpiga gitaa la rhythm amezitengeneza.  Vyombo vya upulizaji vilifuata na hatimaye wimbo ulikuwa tayari. Haikuwa ajabu bendi kuufanyia wimbo mazoezi hata mwezi mzima kabla ya kuanza kuupiga kwenye kumbi. 


Siku ambayo wimbo ulikuwa unapigwa ukumbini kwa mara ya kwanza hadharani, kila mmwanamuziki wakiwamo mafundi mitambo hata marafiki wa karibu wa bendi walikuwa wakiangalia wimbo umepokelewa vipi na wapenzi, wimbo ukionekana umepigwa mara mbili au tatu lakini haujapokelewa vizuri, wimbo huo ulirudishwa tena mazoezini au mara nyingine ulikufa hapohapo na haukupigwa tena, labda mtunzi angeupika tena na kuja nao baada ya marekebisho makubwa.

Wimbo ambao haukupokelewa vizuri, ulifanyiwa kikao, na wanamuziki kujadiliana kwanini wimbo huo haukupokelewa vizuri na wapenzi wao. Katika vikao hivi hakuku-wa na unafiki, na watunzi hawakulalamika kwani walijua kuwa ili wimbo upendeze unahitaji kuboreshwa. Mara nyingi baada ya kufanyiwa marekebisho wimbo uliweza kupokelewa vizuri na kuingizwa katika orodha ya nyimbo za kurekodiwa.

Nyimbo zilipigwa ukumbini kwa muda wa miezi kadhaa kabla ya kurekodiwa, hivyo ‘kuuivisha’ kwa maboresho ya hapa na pale kila ulipopigwa ukumbini. Bendi zilikuwa zikirekodi nyimbo zao katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), utarat-ibu uliokuweko ni kuwa kabla ya kupangiwa siku ya kuingia studio, bendi ililazimika kuwasilisha mashahiri ya nyimbo zote ambazo zilitegemewa kurekodiwa. RTD iliku-wa na kamati ambayo iliyapitia mashahiri hayo na kuidhinisha kurekodiwa au kukataa kurekodiwa, hasa tatizo kubwa lilikuwa ni maadili au mara nyingine hata Kiswahili kisichofasaha. Kulikuwa hakuna nafasi kwa tungo tata kurekodiwa. Nyimbo nyingi zilipita bila kupingwa kwa kuwa bendi zilikuwa zinafanya kikao cha ndani cha kuangalia upya mashahiri kabla ya kuyapeleka RTD. Lakini pamoja na matayarisho hayo,  bado nyimbo kadhaa zilikwama au nyingine kukatazwa kurushwa hewani japo zilikuwa zimepita katika kamati ya awali.

Teknolojia ya siku hizi inamruhusu mtu mmoja kurekodi vyombo vyote peke yake na hata kuimba sauti zote peke yake, hivyo anaweza kuchukua mwezi mzima akishinda studio kurekodi wimbo mmoja, hali haikuwa hivyo zamani. RTD walikuwa wakitoa siku mbili kwa kila bendi kuwa studio. Siku ya kwanza kurekodi nyimbo zote, hata kama ni 15.

Mara nyingi bendi zilianza kurekodi saa nane mchana, lakini muda wa mwisho kuwa studio ilikuwa ni saa 12 jioni. Na kwa kuwa teknolojia iliruhusu kikundi kurekodi kwa pamoja tu au siku hizi inajulikana ni ‘live’, ilikuwa muhimu kabla ya kwenda studio bendi ifanye mazoezi makali sana, kulikuwa hakuna nafasi ya kukosea, kwani akikosea mtu mmoja lazima wimbo wote urudiwe.

Siku ya pili bendi ilishiriki katika kurekodi kipindi cha Club Raha Leo Show. Ni wazi ukielewa aina ya ugumu wa taratibu za kurekodi na kuona kuwa nyimbo zilizore-kodiwa katika mazingira hayo bado ni maarufu miaka 60 au 70 baada ya kurekodi-wa, hakika lazima kukiri ubora na umakini wa wanamuziki katika miaka hiyo. 

Kutokana na aina ya kurekodi hii mwanamuziki ulijua kabisa ni vyombo gani vime-tumiwa katika wimbo wako na kwanini chombo kimepigwa katika sehemu fulani. Halikuwa jambo la kumuachia producer. Hakika kila zama na vitabu vyake.