Anko Kitime: Ndoa ya muziki na soka ilifungwa kitambo
Muktasari:
- Kitongoji hiki kilianza kati ya mwaka 1920 hadi 1925, na kilikuja kuwa kitongoji kikuu cha mwanzo cha watu waliokuja Dar es Salaam kutoka kila kona ya nchi.
Dar es Salaam. Burudani kubwa mbili hapa kwetu ni muziki na soka. Hali hii imekuweko kwa miaka mingi sana. Kitongoji cha Kariakoo ndicho kinaweza kupewa sifa kubwa ya kuwa chanzo cha utamaduni wa burudani za soka na muziki hapa nchini.
Kitongoji hiki kilianza kati ya mwaka 1920 hadi 1925, na kilikuja kuwa kitongoji kikuu cha mwanzo cha watu waliokuja Dar es Salaam kutoka kila kona ya nchi.
Muziki wa dansi ulianza kuingia nchini mwetu kupitia klabu za uchezaji wa dansi zilizoenea karibu kila mji mkubwa nyakati hizo, mfano kule Lindi kulikuwa na klabu kubwa mbili, New African Club na Young People Dancing Club, Tanga kulikuwa na klabu iliyoitwa Young Noverty Dancing Club, na Dar es salaam kulikuwa na New Generation Dancing Club.
Wanachama wa klabu hizi walikutana mwisho wa wiki na kuanza kucheza muziki uliotoka kwenye santuri, jambo ambalo miaka mingi baadae lingeitwa ‘Disco’. Klabu zilifanya mashindano makubwa ya dansa.
Muziki wa Taarab ambao uliingia kabla ya muziki wa dansi ulianza kuenea. Kati ya vikundi vikongwe vinavyokumbukwa ni Egyptian Musical Club na Alwatan Musical Club. Hili kundi la Egyptian Musical Club linasemekana lilianzishwa mwaka 1930 na bwana Abdulbar Diwani na rafiki yake Bom Ambaron.
Kundi limekuwa hai mpaka miaka ya karibuni sana. Egyptian Musical Club na Alwatan Musical Club zilikuwa hasa zinakodishwa katika sherehe za harusi na wapenzi wa muziki wa Taarab.
Bendi za kwanza zilitokana na klabu za dansa, kati ya bendi za kwanza zilikuwa ni African Association Band, Coast Social Orchestra na YMCA Social Orchestra na Dar es Salaam Jazz Band.
Baada ya vita ya pili ya dunia mwaka 1945 ndipo bendi nyingi zikaanza kuchipuka katika miji mbalimbali nchini. Katika jiji la Dar es Salaam, bendi nyingi zilitengenezwa kutoka wanamuziki waliotoka kabila moja.
Huu ulikuwa ni wakati wa ukoloni wa Waingereza ambao walihamasisha sana vijan kutengeneza klabu za kikabila, kwani hata wao walikuwa na klabu kama Italian Club, Greek Club na kadhalika.
Kutokana utaaribu huu ndipo zikaanza bendi kama Ulanga Jazz Band iliyoanzishwa na Wapogoro waliokuwa wakiishi Kariakoo. Wandengereko nao wakaanzisha bendi walioiita Rufiji Jazz Band.
Wanyamwezi kadhaa wakiwa chini ya Iddi Nhende nao wakaanzisha Western Jazz Band. Bendi ilipewa jina hilo kwani wakati huo, Nzega ambako Nhende alitokea, ilikuwa katika jimbo lililoitwa Western Province.
Pia katika enzi hizohizo ndipo kulizaliwa Kilwa Jazz band, bendi iliyoanzishwa na Ahmed Kipande mwenyeji wa Kilwa ambaye alijitoa Tanganyika Jazz Band na kuunganika na wenzie kutoka Kilwa.
Kulikuwa na uhusiano mkubwa kati ya bendi na vilabu vya mpira. Kulikuwa na klabu za mpira zilizokuwa na bendi, mfano klabu maarufu enzi hizo iliyoitwa Young Bombay Football Club ilikuwa pia na bendi yake, iliyoiita Young Bombay.
Klabu kongwe ya mpira ya Sunderland ambayo kwa sasa inajulikana kama Simba Sports Club iliwahi kuwa na kundi lake la muziki lililoitwa The Sunderland Strings.
Klabu ya Sunderland ilikuwa na uhusiano wa karibu na Dar es Salaam Jazz Band. Wakati huo huo klabu ya Young African, ikawa na urafiki na Western Jazz Band.
Ukaribu ulikuwa mkubwa kiasi cha bendi ziliweza kufanya kufanya hata maonyesho ya kuchangisha fedha kwa ajili ya klabu hizo za mpira. Wapenzi wa muziki wa bendi hizi pia walikuwa wapenzi wakubwa wa klabu rafiki za muziki.
Na kama kawaida bendi kazi yake muziki na kuna nyimbo kadhaa ambazo zilitungwa aidha kutania klabu pinzani au kusifia klabu zao.
Kuna wakati Sunderland Sports Club iliwahi kuwafunga Young Africans Sports Club, Dar es Salaam Jazz band wakatunga wimbo uliopata umaarufu sana na ulikuwa na maneno haya;
Yamewafika wenzetu,
Kila wakitaka kujitahidi,
Mambo yamewa shangaza,
Wamebaki wanalia,
Wanasema tutakonda,
Mambo hayo yamezidi,
Tutafanya jambo gani oo.
Kwa vile tunajua utani wa mashabiki wa klabu hizi mbili, nadhani si vigumu kuelewa wimbo huu ulichukuliwaje. Kwa vile ulikuwa wimbo mzuri sana hata wale ambao hawakujua sababu ya kutungwa kwa wimbo huu hakika waliufurahia.