Anko Kitime: Wanamuziki wa Moshi na maajabu yao
Muktasari:
- Moshi ilitoa wanamuziki waliokuja kutikisa anga za muziki Afrika ya Mashariki. Bahati mbaya historia hiyo, kama zilivyo historia nyingi za sanaa za nchi yetu, hazijulikani sana.
Moshi. Katika uwanja wa John Shule Park mjini Moshi, kwa wiki mbili za kwanza za mwezi Julai 2026, kulikuwa na tamasha la filamu lililoitwa Kilimanjaro Film Festival. Tamasha lilifana sana. Tamasha hilo lilinifanya nikumbuke umuhimu wa jiji la Moshi katika historia ya sanaa ya nchi yetu.
Moshi ilitoa wanamuziki waliokuja kutikisa anga za muziki Afrika ya Mashariki. Bahati mbaya historia hiyo, kama zilivyo historia nyingi za sanaa za nchi yetu, hazijulikani sana.
Zawadi kubwa ambayo Moshi ilitoa duniani ni wimbo maarufu wa Malaika. Wimbo huu ambao sifa na mapato yote huelekezwa kwa marehemu Fadhili William, mwanamuziki kutoka Kenya, lakini hakuna shaka kabisa kuwa aliyeutunga aliitwa Adam Salim. Na wimbo huu aliutunga kumuimbia binti aliyeitwa Halima, na ulikuwa wa kutoka moyoni kwani ilikuwa nia ya Adam kumuoa huyo Halima, lakini wazazi wake walimkatalia kwa kuwa walikuwa binamu, hivyo ikaonekana si vizuri ndugu kuoana. Ndugu wa Adam Salim, na ndugu wa Halima wapo wengi tu mjini Moshi.
Mwanamuziki mwingine maarufu kutoka Moshi alikuwa ni Frank Humplik au enzi zake wenzie walimuita ‘Kijana wa Kichaga’, Frank alikuwa mpiga gitaa, muimbaji na mtunzi, na alikuwa akishirikiana na dada zake katika kundi walilojiita Frank na Dada Zake. Muziki wao ulikuwa maarufu sana Afrika Mashariki yote enzi zao, na umeendelea kuwa muziki wenye nafasi kwenye nyoyo za wengi waliopata bahati kuusikia. Baba yake Frank aliingia nchini mwanzoni mwa karne ya 20 akitokea Austria, aliletwa nchini na serikali ya Wajerumani, walimuhitaji atengeneze ramani ya reli ya kutoka Arusha hadi Tanga. Bahati mbaya vita ya kwanza ya dunia ikasimamisha mradi huo na Mzee Joseph Humplick akahamia Marangu ambako alioa na kupata watoto wanne, watatu ndio hao waliokuja kutengeneza kundi la Frank na Dada Zake.
Frank hakuwa mpiga gitaa pekee Moshi, walikuweko wapigaji wengine ambao nao kama ilivyokuwa kwa Frank na Adam Salim walirekodi nyimbo zao katika santuri.
Najua watu wengi watashangaa kwa hili, kwani mkoa huu huwa hautajwi wakati ikiongelewa mikoa yenye histori ya muziki. Mikoa ambayo hutajwa sana ni Tanga, Morogoro, Tabora, na Dar es Salaam kutokana na kuwa na makundi maarufu ya bendi, kama Tabora Jazz Band, Jamhuri Jazz band, Morogoro Jazz Band na Cuban Marimba Band. Lakini ukiangalia hata bendi nyingi kubwa za Dar es Salaam zilikuwa mali ya wafanya biashara kutoka Moshi, mfano Orchestra Safari Sound, Kyauri Voice TP Santa Fe na kadhalika.
Wanamuziki wa kutoka mkoa wa Kilimanjaro walifanya kazi nzuri ya kurekodi nyimbo nyingi kwa lugha ya Kiswahili na Kichaga na Kipare. Muamko wa kurekodi nyimbo za lugha ya Kichaga ulikuwa na mchango mkubwa Chief Thomas Mareale ambaye wakati huo aliwahi kumuuliza Frank Humplik, kwanini harekodi nyimbo za Kichaga wakati kuna nyimbo nyingi zilikuwa zinapatikana wakati huo zikitoka Afrika ya Kusini, waimbaji wake wakiimba katika lugha mbalimbali za huko?
Pamoja na Frank wapiga magitaa wengine kutoka Kilimanjaro, waliyafanyia kazi maombi hayo ya Chief Mareale na hakika nyimbo nyingi za lugha za kiasili zilirekodiwa. Baadhi ya majina ya wanamuziki wa enzi hizo kutoka Moshi ni Wilfred Kuite, Jumanne Omari, Michael John huyu alitoa santuri kwa lugha ya Kipare, Hosea Macha, Shayo Nguoi, Robinson na Kisarambue, Ali Magitaa pia kulikuweko na kundi liloitwa Kimambo Brothers. Wote hawa walitoa santuri ambazo wakati huo zilifahamika zaidi kutokana na spidi yake ya mzunguko wa mara 78 kwa dakika (78rpm). Tanzania ina historia nzuri na kubwa na ya kujivunia ya muziki. Kwa mfano wapenzi wengi wa muziki hawajui kuwa Tanzania ilikuwa na bendi kabla ya Kongo, wengi hudai kuwa Tanzania ilifundishwa muziki na Kongo, jambo hili ambalo hata wanamuziki wengi wa muziki wa rhumba huamini, lina athari kubwa kwani hata wanamuziki wengine hutunga hata nyimbo zao wakiangalia kwanza kinachoendelea Kongo. Historia hizi zimekuwa ngumu kuwafikia wananchi ili waweze kujivunia nchi yao, na hata wasanii kuwa na mtizamo mwingine katika muziki wao.
Katika mika ya 70 kulikuwa na bendi kadhaa maarufu mjini Moshi. Kulikuwa na Zaire Success, Bana Afrika Kituli, bendi ya Chuo cha Polisi PTS Band, bendi mbili za shule, Orchestra Mosesco ya Old Moshi Secondary, bendi ya Chuo cha Ufundi Moshi Technical, na bila kusahau Mkulima Jazz Band. Katika tamasha la Kilimanjaro Film Festival, waandaaji waliwezesha hadhira kusikia baadhi ya nyimbo za Frank Humplik na Hosea Macha zilipigwa, jambo la heshima kubwa kwa Moshi.