Anna wa Jua Kali awachana watukutu

Muktasari:
- Anna aliliambia Mwanaspoti, ili wasanii watimize malengo na kufanya kazi bora na zinazoishi kwa muda mrefu sokoni lazima wawe na heshima na nidhamu ya kazi.
MKALI wa fani ya filamu anayetamba katika tamthilia mbalimbali ikiwamo ya Jua Kali, Godliver Gordian 'Anna amewataka wasanii pamoja na watayarishaji wa kazi za sanaa kuwa na nidhamu ya kazi ili kuwa na kazi bora.
Anna aliliambia Mwanaspoti, ili wasanii watimize malengo na kufanya kazi bora na zinazoishi kwa muda mrefu sokoni lazima wawe na heshima na nidhamu ya kazi.
“Siri kubwa ya kufanya kazi nzuri na kujipatia mashabiki wengi ni nidhamu, ndio imekuwa msingi wa kila kitu kwenye jambo lolote lile, kitu ambacho msanii yoyote akiweka mbele nidhamu ya kazi lazima atafanya vizuri katika sanaa yake," alisema mwanadada huyo aliyeanza kujipatia umaarufu katika tamthilia ya Siri ya Mtungi mwaka 2012.
Mwanadada huyo aliyewahi kunyakua Tuzo ya Mwigizaji Bora kupitia Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF) na Tuzo za Filamu nchini kati ya 2016 na 2021, alisema, licha ya kuwa na nidhamu ya kazi pia wasanii wanapaswa kuwa na upendo kwa wengine kwani nidhamu na upendo ni vitu vinavyoenda sambamba katika kufanikisha mipango uliyojiwekea.
“Wasanii walioko ndani ya sanaa ya uigizaji, nidhamu na Mungu vinapaswa kupewa kipaumbele pindi unapotaka kufanya kazi yako, ni vitu viwili ambavyo vikiwa pamoja vinaleta uwiano wa kazi,” alisema Anna.