Basata yatoa siku mbili Harmonize, Killy na Cheed kumalizana
Muktasari:
Killy na Cheed waliojiunga rasmi na lebo ya Konde Music Worlwide Septemba 2020 wakitokea lebo ya King’s Music inayomilikiwa na msanii Alikiba.
Dar es Salaam. Ngoma bado mbichi, ndivyo unavyoweza kueleza sakata la msanii wa Bongofleva Rajabu Abdul maarufu kwa jina la Harmonize na wasanii wake, Ally Omar (Killy) na (Rashid Mganga) Cheed, baada ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kuwapa siku mbili kumaliza mambo waliyoafikiana katika mkataba wao.
Harmonize kupitia kampuni yake ya Konde Music Worldwide, Oktoba 10, 2022 alitangaza kuvunja mkataba na wasanii hao kwa sababu ambazo hawakuwa tayari kuziweka wazi.
Killy na Cheed waliojiunga na kampuni hiyo hiyo Septemba 2020 wakitokea kampuni ya King’s Music inayomilikiwa na msanii Ali kiba.
Kutokana na hatua hiyo wasanii hao walikimbilia Basata kufikisha malalamiko yao ya kutofuatwa kwa utaratibu wa kuvunjwa kwa mkataba huo ikiwemo kutopewa barua rasmi.
Kikao cha kwanza cha kuwakutanisha pande zote mbili ilikuwa kifanyike Oktoba 12, lakini kilishindikana kutokana na upande wa Harmonize kutotokea na kuahirishwa hadi jana.
Hata hivyo, leo Oktoba 18 pia Harmonize hakufika katika kikao hicho na badala yake alimtuma mwanasheria wake anayejulikana kwa jina la Musa Nassoro.
Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa kikao hicho, Ofisa Sanaa Mwandamizi wa Basata, Abel Ndaga amesema mambo waliyoafikiana katika kikao hicho ni kwenda kuweka sawa yote waliyokubaliana katika mkataba endapo upande mmoja utaamua kusitisha mkataba kama walivyoandikishiana wakati wanaingia katika ndoa hiyo.
"Tumejadiliana vizuri kwenye kikao na kila kitu kimeenda sawa, tumewapa siku mbili waweke mambo sawa na kurudi hapa kwa kuwa kila kitu kwenye mkataba kinajieleza," amesema Ndaga.
Hatahivyo, Ndaga alisema katika kikao hicho sasa lazima Harmonize mwenyewe awepo na hawatahitaji kumuona tena mwakilishi kwa kuwa maamuzi yanaenda kutolewa rasmi.
Alipotafutwa Meneja wa Harmonize kwa njia ya simu anayejulikna kwa jina La Chopa kujua sababu ya wao kutotokea katika kikao hicho kwa mara ya pili, amemjibu mwandishi kwa kifupi, “subiri nitakupigia,” na kukata simu.
Kwa upande wake mwanasheria wa Harmonize alipoulizwa walichoamua kufanya katika shauri hilo, amesema yeye sio mzungumzaji na kutaka atafutwe Harmonize mwenyewe.
Mwananchi lina taarifa kuwa moja ya masharti waliyokubaliana katika mkataba ilikuwa upande wa lebo ukivunja mkataba unapaswa kuwalipa Sh10 milioni wasanii hao kila mmoja na kama wasanii ndio wangevunja mkataba wangepaswa kuilipa lebo zaidi ya Sh1 bilioni.
Hata hivyo, pamoja na kampuni hiyo kuvunja mikataba, wasanii hao wamelalamika kutolipwa fedha zao kwa mujibu wa mkataba na kwamba kampuni ilikimbilia kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari kabla ya kukamilisha taratibu.