Bendi za Rifters na Sunburst zilifungua njia ya muziki

Muktasari:

  • Tofauti nyingine ni kuwa kulikuwa na vikundi vya muziki nchi nzima, na kila kimoja kilitaka kujitokeza kwa muziki wenye ubunifu wake wenye mahadhi mbalimbali

Kitu kimoja ambacho kilikuweko zamani na bado kipo mpaka leo ni nia ya wanamuziki wenye vipaji kutaka kuvitoa vipaji vyao hadharani. Tofauti kubwa ni kuwa zamani muziki ulikuwa ni jambo la kundi na si mtu mmoja peke yake, kwani kulihitajika wapiga vyombo na waimbaji kuwa pamoja.

Tofauti nyingine ni kuwa kulikuwa na vikundi vya muziki nchi nzima, na kila kimoja kilitaka kujitokeza kwa muziki wenye ubunifu wake wenye mahadhi mbalimbali. 

Vingine vikielemea kwenye muziki wa Magharibi vingine vikielemea Kongo na vingine vikibuni mitindo yao kutokana na muziki wa makabila ya hapa nchini.

Kwa mchanganyiko huo vilizaliwa vikundi vingi ambavyo vingine vilikuja kuwa maarufu sana. 

Vijana hasa waliokuwa sekondari walikuwa wanaanzisha vikundi vyao ambavyo vilikuwa vikipiga muziki kwa kuiga muziki wa Magharibi, wanamuziki waliweza kuiga na kupiga nyimbo za vikundi maarufu vya Ulaya na Marekani, kama vile Beatles, Temptations, The Famous Flames  na kadhalika, vikundi hivi viliiga hata majina  ya vikundi maarufu na kulikuweko na vikundi vilivyoitwa, The Tonics, The Sparks,The Rifters na kadhalika, majina yalionyesha pia aina ya muziki ambayo vikundi hivi vilikuwa vikipiga ulielemea wapi.

Vikundi vya muziki vilivyokuwa vinapiga muziki kuelemea muziki wa Congo kwanza majina ya vikundi yalikuwa na sifa ya kuwa Jazz Band au Orchestra kwa mfano, Western Jazz Band, Kilwa Jazz Band, Orchestra Selesele, Orchestra Santa Fe na kadhalika.

Kuna vikundi ambavyo kwa mfano awali vilikuwa ni vya muziki ulioelemea Ulaya, vikundi hivyo vilipobadili muelekeo kimuziki lakini vilibakia na majina yao ya awali kama vile The Safari Trippers na Afro 70.

Kati ya bendi zilizokuwa na mfumo wa kuangalia Magharibi kulikuweko na kundi lililoitwa The Rifters. Bendi hii ilianzishwa Dar es Salaam na Adam Kingui na mwenzie James Mwinga mwaka 1966, vijana  hawa wawili walikuwa machachari sana wakati huo. 

Adam Kingui alidumu kwenye bendi mpaka pale ilipokuja kufutika. Bendi ilianza na wanamuziki wafuatao, Mlima akiwa kwenye gitaa la rhythm, Mudi kwenye gitaa la bezi, James Mwinga kwenye drums, baadaye Mohamed Mdoe akajiunga kama mpiga bezi lakini baadaye akahamia kupiga drums. Raphael Sabuni akiwa anapiga gitaa la solo na gitaa la  rhythm. 

Kadri muda ulivyoenda kukawa na mabadiliko na Kingui aliwaingiza katika kundi lake wanamuziki wengine vijana kama akina Ebby Sykes, Nasoro “Mick Jagger” 

Fadhili kwenye gitaa la bezi, Khalid Mosty kwenye drums na mwanamuziki toka Afrika ya Kusini Vuli Yeni, akiwa mwimbaji, huyu Vuli kwenye miaka ya 90 alikuja kujiunga na kundi la Lucky Dube.

Kundi la Rifters baadaye lilianza kuandaa maonyesho yaliyoitwa Tammi Shows katika Ukumbi wa Splendid Hotel, ambapo pamoja na muziki kulikuwa na wacheza show, jambo ambalo linapinga nadharia ya muda mrefu ya watu wengi kuwa stage show zilianza baada ya safari ya Franco Tanzania mwaka 1973.

Kwa bahati mbaya bendi hizi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wenye mlengo wa magharibi hazikuwa zikirekodi kwani nyimbo nyingi walizokuwa wakipiga zilikuwa ni za kuiga, hivyo picha na hadithi zao tu ndio zimebaki. 

Katika miaka hii kukaanza muziki ulioitwa Afro Rock, huu ulikuwa ni aina ya muziki ulioanzishwa na hizi bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wa mahadhi ya Kimagharibi, wanamuziki wao walianza kutunga nyimbo zilizokuwa na mchanganyiko wa muziki asili na muziki wa Ulaya. 

Katika bendi iliyokuwa maarufu kwa mtindo wa Afro Rock ni bendi ya Sunburst, bendi hii ilikuwa na mchanganyiko wa wanamuziki kutoka Tanzania, Nigeria na Kongo, na bahati nzuri ilikua moja ya bendi zilizorekodi muziki wake, hivyo kumbukumbu za aina ya muziki uliokuwa ukipigwa bado zipo na zinathaminiwa. 

Miaka michache iliyopita kampuni ya Strut Records ilizisambaza upya nyimbo hizo ambazo wanamuziki wake wengi hawapo tena duniani.

Kundi la Sunburst, lilianzishwa mwaka 1970 na mwanamuziki mwenye asili ya Kongo aliyeitwa Hembi Flory, yeye akawakusanya wanamuziki wenzie kama mpiga drum Johnny ‘Rocks’ Fernandes huyu alikuwa Mtanzania mwenye asili ya Kigoa, mpiga bass Bashir Idd Farhani, na mpiga kinanda Kassim Magati, mwimbaji James Mpungo kijana kutoka Mbeya ambaye miaka ya baadaye alikuja kujiunga na kundi la Les Mangelepa.

Mwaka 1973 kundi la Sunburst lilishinda mashindano ya Bendi Bora yaliyofanyika Dar es Salaam, katika mashindano hayo bendi ya Tonics ilikuwa ya pili na Safari Trippers ikawa ya tatu. 

Mwanamuziki mwingine muhimu aliyekuwa katika kundi hili ni Toby John Ejuama mpiga saksafon aliyekuwa Mnaijeria kutoka Jimbo la Biafra, wakati huo jimbo la Biafra likiongozwa na Ojukwu lilikuwa likitaka kujitenga kutoka Nigeria, kwa ajabu sana Tanzania tulikuwa tunaunga mkono jambo hilo. Wanigeria kadhaa walihamia Tanzania wakati huo.

Nimalizie kwa kusema tukitumia msemo maarufu siku hizi, tuzipe maua bendi za Rifters na Sunburst. Rifters kwa kuanzisha stage show na Sunburst kwa kufungua milango ya Afro Rock kwa bendi za Tanzania.