2024 bendi zijaribu kurudisha utamaduni wa kiingilio bia

Muktasari:

  • Utamaduni wa bendi kupiga madansi na kulipwa kwa kuburudisha wanywaji si jambo geni duniani, hapa Tanzania jambo hili lilipata msukumo zaidi mwishoni mwa miaka ya tisini wakati kulipokuwa na ushindani mkubwa wa kampuni kubwa mbili za kutengeneza bia.

Dar es Salaam. Nimepigiwa simu na mwanamuziki mmoja rafiki yangu akilalamika kuwa ni wiki ya pili sasa bendi yake haijapiga muziki kwa sababu baa ambazo walikuwa wanapiga zimeamua kupunguza malipo kutokana na kupungua wateja. Mambo mengi yamenijia  kichwani niliposikia hili, nimekumbuka utamaduni wa kupiga kwenye mabaa  bila kiingilio ulipoota mizizi.

Utamaduni wa bendi kupiga madansi na kulipwa kwa kuburudisha wanywaji si jambo geni duniani, hapa Tanzania jambo hili lilipata msukumo zaidi mwishoni mwa miaka ya tisini wakati kulipokuwa na ushindani mkubwa wa kampuni kubwa mbili za kutengeneza bia.

Moja ya kampuni hizi ilianza kutumia mbinu ya kukodi wasanii  na kuwazungusha katika baa mbalimbali kufanya maonyesho ya kuhamasisha mauzo ya vinywaji vyake, utaratibu uliopewa jina la ‘promosheni’, awali  walikuwa wakikodishwa wasanii  wachekeshaji, wacheza sarakasi, ngoma na kadhalika, baadaye zikaanza kuhusishwa  bendi mbalimbali za muziki.

Kutokana na ushindani wa kibiashara, moja kati ya kampuni hizi ilipotea kwenye soko, upinzani ukawa umepungua, hivyo hata ile kampuni iliyobaki taratibu ikajiondoa katika shughuli za kukodi wasanii na kuwazungusha kwenye baa mbalimbali, lakini wakati huo utamaduni wa baa kuzilipa bendi ili kutumia muziki kuita wateja ulikuwa umeota mizizi na kuwa jambo la kawaida nchini.

Kama nilivyosema kuwa mtindo wa kupiga kwa ajili ya kuburudisha wateja si mgeni duniani, ila kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa sasa hapa nchini na sehemu nyingine nyingi duniani, pengine hii ni kutokana na jinsi mfumo huu ulivyoanza, kwani haukuanzishwa kwa ajili ya kuuza muziki, bali ulianzishwa ili kuuza pombe, hivyo malipo yalitegemea sana na mwenye biashara ya pombe alivyohisi ni vipi bendi itaongeza mauzo.

Miaka ya nyuma hoteli nyingi zilizokuwa chini ya Bodi ya Utalii nchini zilikuwa na bendi zilizoitwa ‘resident band’, kimsingi hakuna tofauti ya malengo ya bendi hizi na zinazopiga kwenye baa siku hizi. Bendi maarufu kama Bar Keys, ambayo sasa inafahamika kama Tanzanites, The Revolu tions inayojulikana kama Kilimanjaro Band zilifikia mpaka kupewa vyumba vya kulala wanamuziki katika hoteli hizo na hata kupewa chakula cha siku nzima,  kazi kubwa ya bendi hizi ilikuwa ni kupiga muziki wa kuvutia wateja kwenye hoteli .

Tofauti na ilivyo sasa, bendi hizi zilikuwa na mikataba ya malipo. Hivyo basi  ikinyesha mvua au likiwaka jua, bendi hizi za hotelini zilikuwa zikilipwa kiasi ambacho kilikubalika katika mikataba. Malipo hayakutegemea upepo wa biashara ya hoteli. 

Katika nchi nyingine kampuni za bia ndizo huwa zinaingia mikataba moja kwa moja na bendi katika kufanya maonyesho ambayo yatasaidia katika kutangaza bidhaa zao, katika mfumo huo  wanamuziki huwa wanapata kipato kizuri

Kupiga muziki kwenye baa katika nchi nyingine huwa ni kwa bendi ndogo ambazo zinatafuta ‘kutoka’. Bendi ndogo hutumia maonyesho haya kwenye baa kujijenga na kutengeneza staili zao na kisha kurekodi nyimbo zao ili kujiwekea nafasi katika ushindani mkubwa uliopo katika ulimwengu wa muziki. Hali ni tofauti hapa kwetu kwa kuwa huku hata bendi ‘kubwa’ nazo zinapiga muziki wa kiingilio bia.

Mwaka 2000 baadhi ya wanamuziki walijikusanya kujaribu kuunda chombo kilichoitwa Union of Tanzanian Musicians (UTAMU). Nia ya chombo hiki ilikuwa ni kupata muungano ambao utaangalia maslahi ya mwanamuziki kama mfanyakazi. UTAMU haikufika mbali, kwani kwanza wanamuziki wenyewe hawakuiunga mkono, labda kutokana na kutofahamu umuhimu wa chombo hicho katika maslahi yao, pili UTAMU ilikataliwa kujiunga na shirikisho la wafanyakazi wakati ule, kwani ilidaiwa kuwa wanamuziki wamo katika kundi la  chama  kilichokuwa cha wafanyakazi wa majumbani na mahotelini CHODAWU (Tanzanian Conservation, Hotels, Domestic and Allied Workers’ Union).

Kukosekana kwa chama cha kulinda maslahi ya wafanyakazi wanamuziki, ni moja ya sababu ambazo zinayumbisha kipato cha wanamuziki, hasa wa bendi kwani hakuna viwango vyovyote vinavyofuatwa, na hivyo kuleta fujo katika tasnia.  Wanamuziki wenyewe wamekuwa wanalalamikiana  kuhusu tabia za wanamuziki wenzao ambao hushusha bei za kukodishwa mpaka kufikia kiwango ambacho ni cha chini mno.

Siyo ajabu kusikia bendi yenye watu saba ikakodishwa kupiga muziki kwa masaa sita ikakubali kulipwa shilingi laki moja na nusu. Kwa hesabu hiyo hujui hata hawa wanamuziki wanagawana vipi pato lao baada ya kulipia gharama za kukodi vyombo  na usafiri wao na wa vyombo.

Mwisho ni woga wa wanamuziki ambao hawajawahi kupiga muziki kwa kuweka kiingilio, wengi wa wanamuziki vijana wameanza muziki katika zama hizi za kulipwa na wenye kumbi, hivyo hawaamini kama wanaweza kuingiza pesa kwa kunadi kiingilio. Bendi moja kubwa ilianza kufanya majaribio ya kurudi kwenye kiingilio wakati wa onyesho lao la mwisho wa mwaka jana, walijikuta wakikusanya mara tatu ya malipo waliyokuwa wakilipwa na wenye kumbi. Bendi zijaribu kubadili upepo 2024.