Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bila Ozalima hakuna Mbosso Khan

Muktasari:

  • Mbosso, mwanachama wa zamani wa Yamoto Band, aliwahi kueleza kutokana na kupenda kusikiliza nyimbo za Kihindi ndio sababu baadhi ya nyimbo zake zina mahadhi hayo, na ndio sababu ya kujiita Khan.

Dar es Salaam. Je, umeshawahi kujiuliza kwanini Mbosso anajiita Mbosso Khan? Hilo jina la Khan msingi wake ni upi katika safari yake ya muziki? Basi majibu ya maswali hayo yote tunayapata kupitia wimbo wake mpya, Ozalima (2026).

Mbosso, mwanachama wa zamani wa Yamoto Band, aliwahi kueleza kutokana na kupenda kusikiliza nyimbo za Kihindi ndio sababu baadhi ya nyimbo zake zina mahadhi hayo, na ndio sababu ya kujiita Khan.

Na ndicho alichokifanya mwimbaji huyo katika wimbo wake mpya, Ozalima (2026) ambao umetayarishwa na Kimambo, ikiwa ni kazi yake ya pili kuachia tangu mwaka ulipoanza.

Neno Ozalima au Zaalima linatokana na lugha ya Kihindi au Kiurdu, likiwa na maana ya mtu mnyanyasaji, mkatili au mtu mdhalimu. Hata hivyo, katika wimbo huu neno hilo limetumika katika muktadha wa kimapenzi, na si katika maana yake halisi.

Kwa muktadha huo, linamwelezea mwanamke ambaye uzuri wake una nguvu kubwa kiasi cha kumtesa mwanaume wake. Si kwamba yeye ni mkatili kwa matendo, bali uzuri na mvuto wake vinampa mateso makubwa mwanaume anayempenda.

Hivyo katika wimbo huo, Mbosso anamwita mpenzi wake Ozalima kwa sababu uzuri wake unamchanganya akili. Unavuruga mawazo yake na kumfanya aote ndoto zisizo na mpangilio kila mara.

Kutokana na uzuri wake huvutia watu wengi, Mbosso anaonekana kuwa na wivu wa kimapenzi ambao umepitiliza, hivyo anaamua kumlinda mpenzi wake huyo kwa njia zifuatazo kama anavyoeleza katika wimbo huo.

Mosi; ni kufuga mbwa wenye meno makali ili kumlinda dhidi ya wanaomtamani. Pili; kuweka bango kuwa hapa kuna hatari ili wanaomtamani wasimkaribie. Na tatu; kuajiri komandoo kama Arnold au Rambo, akionyesha yupo tayari hata kupigana ili kumlinda Ozalima.

Kwa kifupi, Ozalima ni jina la kimahaba linaloelezea jinsi uzuri wa mwanamke unavyoweza kumteka na kumchanganya mwanaume anayempenda kiasi cha kuhisi anateswa na mapenzi yake.

Na ndivyo ilivyo katika nyimbo maarufu za Bollywood (sekta ya filamu India) zinazomtaja Ozalima kama mrembo anayewatesa wanaompenda kwa uzuri wake, au mtu ambaye uzuri wake unamfanya mpenzi wake ashindwe kujizuia.

Hata hivyo, Mbosso hajaanza kutumia maneno ya Kihindi katika wimbo huu wa Ozalima, mathalani wimbo wake uliotangulia, Darasa la Saba (2026) una kionjo cha maneno ya Kihindi.

Maneno hayo ni ‘tere rireh tere sanaam:, yakiwa na maana ya ‘kwa ajili yako, mpenzi wangu’. Hivyo katika wimbo ‘Darasa la Saba’ unampomsikia Mbosso akisema; tere rireh tere sanaam, tambua anazungumza na mpenzi wake!.

Baada ya wimbo wake, Nipepee (Zima Feni) (2018) aliyoimba kwa mahadhi ya Kihindi kwa mara ya kwanza kumpatia mafanikio makubwa, ndipo alipoendeleza utamaduni huo na hata kuanza kujiita Mbosso Khan.

Kwa mujibu wa Mbosso, baada ya kusainiwa na WCB Wasafi alitoa nyimbo nyingi lakini hazikufanya vizuri kwa kiwango kikubwa kama alivyotarajia, ila baada ya kubadili mtindo wake wa uimbaji na kuja na wimbo huo (Nipepee) mashabiki wakampokea vizuri.

Zilifuata nyimbo nyingine za aina hiyo ambazo ni Hodari (2018) na Maajab (2019), ambazo ndio hasa lilitambulisha na kuleta maana kamili ya jina la Mbosso Khan.

Kati ya nyimbo hizo, Hodari ndio uliokuja kufanya vizuri zaidi hadi kuwa wimbo wake namba moja ilivyotazamwa zaidi YouTube (most viewed), ambapo kwa sasa unashika nafasi ya tatu huku video yake ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 63.


Kwa asilimia 100, video hiyo imebeba mwonekano wa Kihindi kuanzia wahusika wake walivyovaa, kucheza na hata kuingiza, kwa kifupi haitofautiani sana na nyimbo tunazoziona katika filamu za Bollywood.

Kwa maana hiyo, mahadhi ya muziki wa Kihindi ndio yaliyomfungulia Mbosso ukurasa mwingine katika muziki baada ya awali kutamba na kundi la Yamoto Band ambalo alifanya nalo kazi tangu mwaka 2012 hadi 2017.

Ili kutunza alama hiyo, Mbosso hakuishia kujiita Khan tu, bali hata lebo aliyoianzia baada ya kuachana na WCB Wasafi, ameipa jina hilo ikitambulika kama Khan Music ambayo ndio inasimamia kazi zake kwa wakati huu.

Ikumbukwe Khan Musici ni lebo inayoakisi umbali aliotoka Mbosso kimuziki, na haya ni matokeo ya dhamira ya kweli katika kuzifikia ndoto zake.

Kwa mara ya kwanza Mbosso alipata umaarufu akiwa Yamoto Band baada ya kuachia wimbo wao, Ya Moto (2013) uliotengenezwa Vibe Records na Shirko, na kuanzia hapo jina lake limekuwa likijizolea sifa lukuki katika Bongofleva.