Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbosso kamsahau Aviola!

MBO 03

Muktasari:

  • Hata hivyo, licha ya umaarufu wa wimbo huo pamoja na namba zake za kuridhisha katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki, ni kama Mbosso ameamua kuuchunia kimtindo jambo linaloacha maswali.

Dar es Salaam. Bado Mbosso anaendelea kutamba vilivyo na Extended Playlist (EP) yake ya pili, Room Number 3 (2025) yenye nyimbo kali kibao ukiwemo ‘Aviola’ ambao ni maarufu sana kwa baadhi ya mashabiki wa soka nchini pengine kutokana na ujumbe wake.

Hata hivyo, licha ya umaarufu wa wimbo huo pamoja na namba zake za kuridhisha katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki, ni kama Mbosso ameamua kuuchunia kimtindo jambo linaloacha maswali.

Room Number 3 EP (2025) ikiwa na nyimbo saba zilizochanganywa kwa ustadi, hisia, ubunifu na miondoko ya kisasa, inaonyesha ukuaji wa Mbosso ikijumuisha aina maarufu za muziki kama Bongo Fleva, Afrobeat, R&B na Amapiano.

Kila wimbo unazungumzia mada zinazogusa maisha ya kila siku kama vile mapenzi na safari ya maisha kwa kutokana na maneno yenye kugusa hisia na midundo ya kuvutia inayozungumza moja kwa moja na kizazi cha sasa.

MBO 01

Kwa sauti ya kipekee na utayarishaji wa kiwango cha juu, Mbosso anaendelea kuthibitisha kwa nini anabaki kuwa moja ya nguzo kuu za muziki Afrika Mashariki. Kupitia Khan Music, amefungua ukurasa mpya akiwaahidi mashabiki muziki halisi na usiosahaulika.

Ndani ya Room Number 3 (2025), EP iliyoachiwa miezi mitatu iliyopita, ndivyo Mbosso alivyofanya akitoa nyimbo maarufu kama kama Pawa, Nusu Saa, Merijaah na Aviola ambao hadi sasa video yake haijatoka licha ya kufanya vizuri.

Baada ya uzinduzi wa EP hiyo, ndani ya saa 24, wimbo wa Aviola ndiyo ulioanza kujadiliwa sana mtandaoni kutokana na tukio la Queen Fraison, dansa maarufu kama ‘Bongo la Dada’ kuonyesha uwezo wa kucheza wimbo huo katika hafla hiyo.

MBO 02

Tangu siku hiyo Aviola akawa wimbo maarufu ndani ya Bongo Fleva huku ukitumika zaidi katika utani wa kisoka na ndiyo uliokuja kuzalisha jina la ‘Bonge la Dada’ ila cha ajabu Mbosso amegoma kuachia video yake hadi leo hii.

Aviola ni wimbo wa kusisimua wa kukonga nyoyo na uliojaa sifa, ukieleza furaha ya uhusiano unaoshinda mashaka na kuendelea kukua kadri muda unavyosonga huku ukichanganya methali za Kiswahili na midundo ya kucheza.

Unamsifu mwanamke mrembo ajulikanae kama Aviola  anayeelezwa kama ‘Bonge la Dada’ ambaye ni mwanamke mzuri na wa kuvutia akiwa na mvuto wa pekee kiasi hata mama yake anampenda.

MBO 03

Kwa ufupi, Aviola ni sherehe yenye furaha iliyosheheni hisia za upendo na shukrani, ukiwasilishwa kwa mtindo wa kipekee, mathalani kupitia tashbihi za kishairi, kama vile kupanda Mlima Kilimanjaro, akimaanisha safari ya mapenzi.

Ukitazama YouTube, wimbo (audio) wa Aviola ambao umetayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic, tayari umesikilizwa zaidi ya mara milioni 5 ukiwa ni wa pili kufanya vizuri nyuma ya Pawa wenye milioni 6.2.

Hivyo ni wazi mashabiki wana kiu ya kutazama video rasmi ya Aviola kwa sababu huwa ni ngumu sana kwa audio pekee kufikia namba hizo. Watu wanataka kumuona ‘Bonge la Dada’ mwenyewe. Je, ni huyu tunayemjua au atabadilishwa?

MBO 04

Hadi sasa katika EP hiyo, Mbosso ameachia video moja pekee, nayo ni ya wimbo ‘Pawa’ ambayo inaendelea kufanya vizuri ikiwa ndiyo video pekee ndani ya Bongo Fleva iliyotoka mwaka huu ambayo imetazamwa zaidi YouTube.

Video ya ‘Pawa’ imetazamwa mara milioni 33 ikiwa ni video ya kwanza kwa Mbosso kufanya hivyo ndani ya miezi mitatu na sasa ikipanda hadi nafasi ya sita katika orodha ya video za mwanamuziki huyo zilizotazamwa zaidi. Pengine Mbosso anachelewa kutoa video ya ‘Aviola’ akihofia atapunguza nguvu ya ‘Pawa’ ambayo imeshafikia nusu ya namba ya video yake, Baikoko (2021) ambayo ndiyo namba moja YouTube kwa kutazamwa zaidi upande wake.

Katika EP ya kwanza, Khan (2022) iliyoachiwa na nyimbo sita, Mbosso alitoa video mbili tu (Huyu Hapa na Shetani), hivyo huwenda Room Number 3 (2025) nayo ikapita humo humo au akabakia na video hiyo moja.

MBO 05

Ikumbukwe Room Number 3 EP (2025) inaonyesha safari ya Mbosso kimuziki na ukuaji wake ikiwakilishwa vipindi vitatu tofauti - Yamoto Band, WCB Wasafi na Khan Music akiwa kama msanii anayejitegemea kwa kila kitu.

Kwa mchanganyiko wa hisia, uandishi wa hadithi nzuri na sauti iliyokomaa, Room Number 3 EP (2025) inaakisi umbali aliotoka Mbosso kimuziki na haya ni matokeo ya shauku na dhamira ya kweli katika kuzifikia ndoto kubwa maishani.