Burna Boy, Shakira sasa rasmi kukiwasha Kombe la Dunia
Muktasari:
- Ushiriki huo unamweka Burna Boy katika historia ya muziki wa Afrika, akitajwa msanii wa pili kutoka Afrika kukiwasha katika kombe la dunia baada ya msanii mwenzake Davido ambaye aliuwasha moto katika Kombe la Dunia la mwaka 2022 lililofanyika jijini Qatar.
Marekani. Mkali wa Afrobeat kutoka Nigeria, Burna Boy ameendelea kunga’ara baada ya kuthibitishwa rasmi kwa ushiriki wake na malkia wa muziki wa Latin, Shakira kuwa watatumbuiza katika sherehe ya ufunguzi wa Kombe la Dunia FIFA 2026, ufunguzi utakaofanyika jijini Mexico hivi karibuni.
Ushiriki huo unamweka Burna Boy katika historia ya muziki wa Afrika, akitajwa msanii wa pili kutoka Afrika kukiwasha katika kombe la dunia baada ya msanii mwenzake Davido ambaye aliuwasha moto katika Kombe la Dunia la mwaka 2022 lililofanyika jijini Qatar.
Mbali na kutumbuiza, Burna Boy na Shakira tayari wameunganisha nguvu kwa kuachia wimbo rasmi wa Kombe la Dunia uitwao ‘Dai Dai’, ambao umechaguliwa na FIFA kuwa sehemu ya utambulisho wa mashindano hayo yatakayofanyika katika nchi tatu ambazo ni Mexico, Marekani na Canada.
Wimbo huo wa ‘Dai Dai’ umekuwa ukifanya vizuri katika chati za muziki duniani ambapo mpaka kufikia sasa umeshatazamwa zaidi ya mara milioni 79 katika mtandao wa YouTube ukiwa na siku 12 tu tangu kuachiwa kwake.
Kwa Shakira, huu ni mwendelezo wa safari yake ndefu na Kombe la Dunia. Nyota huyo tayari aliwahi kuandika historia kupitia nyimbo kama Waka Waka (This Time for Africa) mwaka 2010 na La La La mwaka 2014, nyimbo ambazo ziligeuka alama za mashindano hayo kwa mamilioni ya mashabiki duniani.
Kwa upande wa Burna Boy, ushirikiano huu unaendelea kuthibitisha ukuaji wa muziki wa Afrika katika soko la kimataifa. Katika miaka ya hivi karibuni, nyota huyo amefanikiwa kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa duniani na kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa, huku sasa akipata nafasi ya kupeleka sauti ya Afrobeats kwenye moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo duniani.
Kombe la Dunia la FIFA 2026 litakuwa la kwanza kushirikisha timu 48 na linatarajiwa kuanza Juni 11, 2026 katika Uwanja wa Azteca, Mexico City, huku sherehe ya ufunguzi ikitarajiwa kuvutia mamilioni ya watazamaji duniani. Kwa uwepo wa Burna Boy na Shakira pamoja na wimbo wao “Dai Dai”, FIFA inaonekana kulenga kuanza mashindano hayo kwa mchanganyiko mkubwa wa soka, utamaduni na muziki wa dunia.
Hata hivyo mbali na Burna naye msanii Davido anatarajia kutumbuiza kwenye tamasha kubwa la FIFA World Cup 2026 Countdown Concert litakalofanyika Juni 10 katika ukumbi wa Crypto.com Arena jijini Los Angeles, Marekani.
Davido atatumbuiza pamoja na kundi la muziki la Major Lazer, linaloongozwa na DJ maarufu Diplo. Huku waandaaji wakieleza kuwa siku zijazo watatangaza wasanii wengine wa kimataifa ambao wataungana na Davido katika hafla hiyo.
Kwa mujibu wa FIFA, tamasha hilo litafanyika Juni 10, 2026 saa 5:00 usiku na litakuwa moja ya matukio makubwa ya burudani yanayounganisha mashabiki wa soka duniani kabla ya mashindano hayo kuanza rasmi.