Diamond afunguka ishu ya Komasava kuitwa takataka
Muktasari:
- Kupitia mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni na DW, Diamond Platnumz alifichua kwamba alipowasilisha wimbo wa 'Komasava' kwa WMG kama sehemu ya mkataba wake, waliukataa na kusema kuwa ni "takataka."
Dar es Salaam. Diamond ambaye ni mwanamuziki anayetamba na kibao cha ‘Komasava’ kilichotazamwa zaidi ya mara milioni 31 kwenye mtandao wa YouTube, amedai lebo inayotamba Afrika ya Warner Music Group (WMG) iliukataa wimbo huo.
Kupitia mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni na DW, Diamond Platnumz alifichua kwamba alipowasilisha wimbo wa 'Komasava' kwa WMG kama sehemu ya mkataba wake, waliukataa na kusema kuwa ni "takataka."
“Nilipowasilisha wimbo huo kwa wasambazaji wangu, ambao ni Warner, hawakuutaka, walisema ni takataka. Kwa sababu mimi na wao tuna makubaliano ya kuwapa nyimbo fulani,” alieleza Diamond Platnumz.
Licha ya changamoto hiyo, Diamond alisema alirejea nyumbani na kuusikiliza tena, akiwa na imani kwamba wimbo huo mkubwa na bora sana.
“Kwa nini hawaelewi wimbo huu? Huu wimbo ni hit. Niliutoa tu,” alieleza Diamond.
Akizungumzia sababu ya WMG kuita wimbo wake ‘Takataka’ Diamond alisema ni kutokana na mawazo ya kizamani waliyonayo.
“Unapowapa muziki wenye sauti mpya, hawataki kuuchukua. Sasa, baada ya wimbo kutoka, wanautaka. Nilimwambia meneja wangu kuwa sitaki awape wimbo huu kwa sababu waliukataa,” aliongezea Diamond.
Wimbo huo ambao umechezwa na baadhi ya mastaa kutoka Marekani akiwemo Chris Brown na Swae Lee umepokelewa kwa ukubwa duniani kote kutokana na kuwepo na lugha mbalimbali ikiwemo Kifaransa, Kihindi, Kiswahili na nyinginezo.