Diamond afunguka kilichojiri Nairobi hadi kukacha shoo
Muktasari:
- Diamond ameyasema hayo kufuatia vurugu hizo zilizotokea zikihusishwa na ugomvi baina yake na msanii wa Kenya, Willy Paul
Dar es Salaam. Mwanamuziki anayetamba na ngoma ya ‘Komasava’ Diamond Platnumz, amefunguka kuhusiana na mgogoro uliotokea katika Tamasha la Furaha City lililofanyika Desemba 7, 2024 huku akidai kuwa vurugu ndiyo sababu za kuondoka bila kutumbuiza.
Diamond ameyasema hayo kufuatia vurugu hizo zilizotokea zikihusishwa na ugomvi baina yake na msanii wa Kenya, Willy Paul.
“Siku ya shoo nilifika uwanjani mapema, nafika pale alikuwa anafanya shoo Khalighraph, unajua mimi nikifika kwenye shoo sipendi kuingia backstage (nyuma ya jukwaa), napenda kukaa kwenye gari, toka nafika kuna vurugu chini ya stage (jukwaa) zisizojulikana ni sababu gani,” amesema Diamond kupitia video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mbali na hilo, Diamond ameweka wazi kuhusiana na suala la kumzuia msanii mwenzake kufanya shoo akidai kuwa hajawahi kufanya hivyo.
“Mtu anakujua anasema umemzuia kufanya shoo, mimi mwenyewe mgeni, sikupata nafasi ya kufanya shoo ndio maana nikaona acha niondoke zangu, mimi nimelipwa zaidi ya dola 150 (zaidi ya Sh400 milioni za Tanzania).
“Siwezi kuja kwenye event (tukio) halafu nika-force (lazimisha) nipande kwenye stage (jukwaa), wewe ushanilipa, mimi nasubiri muda wangu wa kuperfom (kutumbuiza), nikiona muda huu siyo wa kupanda kwenye stage (jukwaa) naondoka zangu, siwezi ku-force, ukishindwa kunipandisha katika muda tuliokubaliana naondoka zangu na pesa yako nakuwa nimeila,” amesema Diamond ambaye anatambulika pia kwa jina la Simba.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii huku kila mmoja upande wa Will Paul na Diamond akimtuhumu mwenzake kusababisha vurugu hizo.