Dvoice anacheza zake anga za Alikiba

Ikiwa ni takribani miezi miwili tangu D Voice ametambulishwa kwenye ‘lebo’ ya WCB Wasafi, kupitia albamu yake, Swahili Kid (2023) tayari ameingia kwenye anga za wasanii wengine, akiwemo Alikiba aliyoiweka miaka miwili iliyopita.

Albamu hiyo ya D Voice yenye nyimbo 10 iliwashirikisha wasanii wa WCB Wasafi pekee ambao ni Diamond Platnumz, Lava Lava, Mbosso na Zuchu aliyesikika katika nyimbo mbili, BamBam na Nimezama.

Utakumbuka D Voice ni msanii wa saba kutambulishwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018) na Zuchu (2020).

Kati ya hao, wasanii watatu wamejitoa katika lebo hiyo ambao ni Rich Mavoko (2018), Harmonize (2019) na Rayvanny (2022) kisha kwenda kuanzisha zao, Billionea Kid, Konde Music Worldwide na Next Level Music (NLM).

Hadi sasa D Voice tayari ametoa video za nyimbo tano kutoka katika albamu yake, ikiwa sawa na asilimia 50, nyimbo ambazo video zake zimetoka ni BamBam ft. Zuchu, Lolo, Mtamu, Mpeni Taarifa ft. Mbosso na Turudiane ft. Lava Lava.

Kwa matokeo hayo, D Voice ameingia kwenye anga za rekodi ya albamu ya tatu ya Staa wa Kings Music, Alikiba, Only One King (2021) yenye nyimbo 16 ambayo nayo idadi ya video zake zilizotoka zilifikia asilimia 50.

Alikiba alifanya video za nyimbo nane ambazo ni Infidele, Ndombolo ft. Kings Music, Salute ft. RudeBoy, Jealous ft. Mayorkun, Oya Oya, Bwana Mdogo ft. Patorankig, Utu na Niteke ft. Blaq Diamond.  Only One King ilizizidi albamu zilizotoka mwaka huo kama Sound From Africa (Rayvanny), Defination of Love (Mbosso), High School (Harmonize), Air Weusi (Weusi), 20 (Lady Jaydee), Asante Mama (Dogo Janja), Experience (Stereo), The Gift of Life (Best Naso) n.k.

Ikumbukwe D Voice ndiye msanii wa kwanza wa WCB Wasafi kutambulishwa
na albamu, Zuchu alitambulishwa na Extended Playlist (EP), I Am Zuchu (2020) yenye nyimbo sita, huku akiwashirikisha Mbosso na Khadija Kopa ambaye ni mama yake mzazi.

Wengine wote waliobaki walitambulishwa na wimbo mmoja mmoja kama ifuatavyo: Harmonize (Aiyola), Rayvanny (Kwetu), Rich Mavoko (Ibaki Story), Queen Darleen (Kijuso), Lava Lava (Tuachane) na Mbosso (Watakubali).

Na albamu hiyo ya D Voice, Swahili Kid iliyotoka rasmi Novemba 17, 2023 tayari imefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 8 YouTube, huku Boomplay Music ikiwa imesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 16.9.

Kutokana na uwekezaji huo, inatazamiwa kuwa miongoni mwa albamu zitakazowania tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2023 ikiwa ni msimu wake tangu zirejee kufuatia kusimama kwa miaka saba.

Ikumbukwe albamu ya Barnaba, Love Sounds Different (2022) ndiyo ilishinda TMA msimu uliopita kama  Albamu Bora ya Mwaka baada ya kuzibwaga nyingine kali kama ‘The Kid You Know’ ya Marioo, ‘Made For Us’ ya Harmonize, ‘Street Ties’ ya Conboi na ‘Romantic’ ya Kusah.