Wapishi wa ngoma walioupiga mwingi 2023

Muktasari:

  • Hii ni orodha ya watayarishaji wa muziki ambao wamefanikisha kutengeneza kazi ambazo zimependwa na kila mtu.

Kila mwaka tumekuwa tukisifia na kuwapa heshima wasanii wa Bongofleva kwa kufanya vizuri katika nyimbo ambazo wamezifanya.

Lakini, katika nyimbo hizo kali kuna mikono ya maproducer ambao walihakikisha kuwa zinakuwa an vibe.

Mwaka 2023, zimeachiwa kazi nyingi  Bongofleva, ambazo zimefanya vizuri mpaka kuchukua au kuingia  kwenye vinyanganyiro vya tuzo mbalimbali.

Hii ni orodha ya watayarishaji wa muziki ambao wamefanikisha kutengeneza kazi ambazo zimependwa na kila mtu.

S2KIZZY

Salmin Kasimu Maengo, maarufu kama S2Kizzy au Zombie, bila shaka 2023 amefanikiwa kwa sehemu kubwa kukata kiu za mashabiki wengi wanaopenda muziki nchini.

Kama ambavyo jina linasadifu, ‘We Zombie’, amehakikisha kuwa hatuna tunachomdai kwa sababu mkono wake umetayarisha nyimbo kumi bora zinazofanya vizuri kwa sasa katika anga ya Bongofleva.

Safu yake ya ushambuliaji wa vibao umebebwa na nyimbo nyingi kali kama ‘Shu’ ambayo imeimbwa na Diamond Platnumz, ‘Enjoy’ ambayo imeimbwa na Jux, ‘Shisha’ ambayo imeimbwa na Marioo, ‘Nitongoze’ ya Rayvanny, ‘Gibela’ ya Chino Kidd na ‘NaNi’ kutoka kwa Abby Chams.

Nyimbo hizi zimekuwa zikifanya vizuri na kuongoza chati tofauti tofauti katika mitandao ya kustream nyimbo duniani kama vile Apple Music, Audiomack na Boomplay.

Licha ya kuwa na rekodi hiyo ya kipekee kwa mwaka huu, S2kizzy pia ameingia kwenye kipengele cha tuzo za Grammy 2024 kupitia wimbo wa ‘Mama Tetema remix’, wimbo ambao aliutengeneza mwaka 2019, ulioimbwa na Rayvanny pamoja na Diamond Platnumz.

Kipenele hicho ni ushiriki wa nyimbo hiyo kuwa moja ya nyimbo 10 zinazopatikana katika albam mpya ya Maluma inayofahamika kama ‘Don Juan’, kama ikatokea album hiyo ikashinda tuzo ya Grammy basi S2kizzy pamoja na Rayanny watanyakua tuzo hiyo.

MR LG

Lugendo Kileo, almaarufu MRLG, ni moja ya watayarishaji wa muziki ambao katika playlist yako, najua huwezi kukosa nyimbo zake hata tano.

Nazungumzia vibao kama vile ‘Honey’ ya Zuchu, moja ya nyimbo ambayo imefanya vizuri kwa mwaka huu, ikiwa na jumla ya wasikilizaji takribani milioni 20.

Nyimbo nyingine ni ‘Tajiri’ ya Lavalava, ‘Chapati’ iliyofanywa na Zuchu pamoja na kibao cha ‘Basupa’ kilichoimbwa na Young Dee pamoja na Dj Ally B.

Kupitia kurasa yake ya Instagram, MrLg alishare na mashabiki zake kuonyesha namna ambavyo nyimbo zake zimesikilizwa.

Takribani jumla ya nchi 179, wamesikiliza vibao ambavyo vimeandaliwa na mtayarishaji huyo ambaye amekuwa akifanya vizuri katika anga za muziki wa Bongofleva.


ABBAH

Unapokuwa unazungumzia orodha ya watayarishaji wa nyimbo bora kwa mwaka wa 2023, jina la Abbah sio la kukosa.

Abbah Mwinula, maarufu kama Abbah Process, amekuwa kwenye tasnia ya Bongofleva kwa muda mrefu akitengeza vibao ambavyo vinaendelea kuishi mpaka leo.

Hata hivyo, 2023 ameonyesha kutopumzika kwa kushindana na vizazi vipya vya watayarishaji muziki.

Mwaka huu, amejitahidi kuonyesha ule uzoefu wake katika nyimbo kama  ‘Huku’ kilichoimbwa na Alikiba, ‘Milele’ iliyoimbwa na Abby Chams, ‘Ananipenda’ iliyoimbwa na Platform na ‘Nakuja’ kilichowekewa vocal na Tommy Flavour.

Vibao vyote vimefanikisha kuwa na watazamaji pamoja na wasikilizaji zaidi ya milioni, huku video za kucheza na kuimba nyimbo hizi zikiwa zinafanya vizuri kwenye mtandao wa Tiktok

Geniusjini

Mpishi mwingine kwenye orodha ya watayarishaji muziki ni geniusjinix66.

Geniusjini ni moja ya watayarishaji wenye vipaji vya kutayarisha, kuimba na kuandika nyimbo kali za Bongofleva.

Vibao vyake, 'Kamtu', 'Juu', pamoja na 'Wewe' vimekuwa vinafanya vizuri TikTok.

Licha ya kukufanya ujisikie unapenda tena, nyimbo zake zinaonyesha wazi jinsi inavyowezekana kumpenda mtu na kupendwa.

Iam Trone

James Pascal Nyaoza, almaarufu Trone, au unaweza kumwita ‘young zombie’.

Huyu ni mdogo wa producer S2kizzy ambaye anafanya kazi chini ya studio ya S2kizzy ‘Pluto Republic’.

Ni moja ya producers ambaye amebarikiwa na mapishi ya kibunifu linapokuja suala la muziki.

Wengine humwita mchawi wa wachawi wa muziki linapokuja suala la kutengeneza nyimbo maarufu.

Anajulikana kwa vibao vyake kama vile 'Naringa' na 'Shika' zote kutoka kwa Zuchu.

Kama ulikuwa umesahau, huyu ndiye aliyesuka ‘Sukari’ ya Zuchu mwaka 2021 na kuufanya kuwa wimbo wa bora wa muda wote.

Lakini si hivyo tu, amehusika katika kuandaa nyimbo za msanii mpya wa WCB Dvoice katika albam ya ‘Swahili Kid’.

Nyimbo zenyewe ni pamoja na ‘Bam Bam’ na ‘Mpeni Taarifa’

Kimambo Beats

Kuanzia Bongofleva hadi nyimbo za mandhari ya soka, Kimambo hakika anajua kutengeneza vibao katika kila kona ya burudani.

Katika upande wa michezo, Kimambo alitubariki na ‘Mnyama’ nyimbo ya Simba SC ambayo imeimbwa na Alikiba.

Hata hapo awali, pia alitupatia hit kwa ajili ya mashabiki wa Yanga, ‘Yanga Anthem’ ngoma ambayo iliimbwa na Marioo.

Tukirudi katika radha yetu ya Bongofleva, Kimambo aliwakosha wapenda burudani kupitia kibao cha ‘Falling’ kilichoimbwa na Nandy.


Lizer Classic

Ni muda mrefu umepita tangu Iraju Hamisi, almaarufu Ayo Lizer, kutayarisha wimbo kwa ajili ya Diamond Platnumz.

Kama jinsi ilivyokuwa miaka iliyopita, mwaka 2023 Lizer ameweza kutengeneza ngoma ‘Yatapita’ na ‘Zuwena’.

Amekuwa kwenye tasnia ya muziki kwa miaka sasa tangu alipokuja mwaka 2014. Ni mmoja ya watayarishaji waliotengeneza rekodi isiyo na kikomo ya Diamond Platnumz na WCB kwa miaka mingi.

Nyimbo kama vile ‘Sikomi’, ‘Eneka’, ‘Zilipendwa’, ‘Jibebe’ na nyinginezo nyingi zinachangia wimbo wa Diamond Platnumz.