Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Wasanii wapenda vya bure wanawashusha watayarishaji

Muktasari:

Kimsingi wao ndiyo wapishi wa kila wimbo mzuri, lakini cha kustaajabisha ni kwamba wengi wao hawajawahi kupata faida ya kile wanachokifanya au kama wanapata basi ni kiduchu ukilinganisha na ukubwa na umuhimu wa kazi yao.

Wakati Watanzania tunajivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika muziki wa Bongo Fleva; idadi kubwa ya watayarishaji wanaugulia maumivu licha ya kwamba wana mchango mkubwa katika tasnia hiyo.

Kimsingi wao ndiyo wapishi wa kila wimbo mzuri, lakini cha kustaajabisha ni kwamba wengi wao hawajawahi kupata faida ya kile wanachokifanya au kama wanapata basi ni kiduchu ukilinganisha na ukubwa na umuhimu wa kazi yao.

Mara kadhaa tumewasikia wakilalamika kwenye vyombo vya habari jinsi wanavyominywa na kukosa kufaidi jasho lao, huku lawama kubwa wakizielekezea kwa wasanii hasa wenye majina makubwa.

Watayarishaji wapo sahihi kwani jinsi mfumo wa muziki nchini ulivyo, watu pekee wanaotafuna ama kuwadhulumu jasho lao ni wasanii ambao wamekuwa vichwa ngumu kwenye kufanya malipo baada ya kutengenezewa kazi zao.

Ugumu wao wa kuwawezesha kiuchumi ndiyo unaowapoteza kwenye tasnia watayarishaji wenye vipaji.

Mara kadhaa mtayarishaji mpya anaibuka, anavuma sana kwa kuwatengenezea nyimbo kali wasanii wakubwa, lakini ghafla anapotea kwenye ramani ya muziki.

Kinachotokea ni kwamba; kwa kawaida mtayarishaji anayechipukia anakuwa na lengo la kujitangaza. Katika harakati za kufanikisha hilo, wengi wanakuwa tayari hata kufanya kazi na wasanii wakubwa bila malipo.

Lengo la mtayarishaji kujitangaza linapotimia unakuwa wakati mwafaka kwa yeye kuanza kula matunda ya kipaji alichonacho na kazi anayoifanya lakini ajabu ni kwamba utakuta hadi wanafika katika hatua hii msanii mkubwa bado anataka kufanyiwa kazi bure.

Wanapofikia hatua hii hakuwezi kuwa tena na maelewano, msanii anaamua kutafuta mtayarishaji mwingine mdogo kwa ajili ya kuendeleza kamchezo cha unyonyaji; wakati watayarishaji wengi huamua kufanya kazi wenyewe ingawa katika hatua hii siyo wengi wanaofanikiwa na hapo ndipo utaona ghafla anapotea.

Katika hili bado wasanii wetu wanastahili kubebeshwa mzigo wa lawama. Idadi kubwa ya wasanii wetu wenye majina ‘wanaopenda vya bure’.

Wanafurahia kuwanyonya wengine kwa kigezo cha umaarufu na ukubwa wa majina yao, hawathamini wala kujali ugumu wa kazi zinazofanywa na washirika wao, hawajali ubunifu wanaotumia wengine kuhakikisha muziki wao unakonga nyoyo za mashabiki.

Mifano yenye kuthibitisha tabia ya kupenda vya bure ya wasanii wetu iko mingi sana.

Kwa mfano wanawalipa ‘waelekezi wa video’ pesa kiduchu huku wakitaka kutengenezewa video nzuri; matokeo yake wanapotengenezewa kazi zenye kuendana na pesa waliyolipa wanakuwa mbogo na kuanza kuwatupia lawama waelekezi kwamba hawana ubunifu.

Hata kwenye kutengeneza ‘kava’ kwa ajili ya nyimbo zao, wasanii wengi wamekuwa ‘wakiwalalia’ wasanifu huku wakitaka kutengenezewa kava kwa gharama ndogo au hata bure eti kwa sababu tu wana majina makubwa yanayoweza kumsadia mtengenezaji kujitangaza.

Mbali na hilo, wasanii wenye majina wamekuwa na kawaida ya kuwanyonya hata wachenza dansi wao.

Msanii anawachezesha vijana jukwaani tena kwenye tamasha kubwa tu lakini kiasi anachowalipa ni aibu hata kusema.

Nadhani umefika wakati kwa wasanii kubadilika, tabia ya kupenda vya bure haiwezi kuboresha kazi zao na kuwa za kimataifa kama ambavyo wasanii wengine kutoka hapa hapa nyumbani wamefanikiwa.

Unapojali na kumthamini mtayarishaji ni rahisi kutuliza akili na kufanya ubunifu ambao utakusaidia kukutengenezea kazi zenye ‘utamu’ wa hali ya juu masikioni mwa mashabiki. Kuthaminiana ni jambo jema.

0713 482816