Harmonize na Poshy Queen ni suala la muda tu!

Muktasari:

  • Huu ni uhusiano wa tano kwa Harmonize kuuweka hadharani baada ya kufanya hivyo kipindi akiwa na Jacqueline Wolper, Sarah Michelotti kutokea Italia, Kajala Masanja, Briana kutokea Australia na Yolo The Queen wa Rwanda.

Kutokana na historia ya Harmonize katika ulimwengu wa mapenzi, kuna mambo ambayo kuna uwezekano mkubwa yakaja kumkuta mpenzi wake wa sasa Poshy Queen ambaye walitangaza kuwa pamoja hapo Januari.

Huu ni uhusiano wa tano kwa Harmonize kuuweka hadharani baada ya kufanya hivyo kipindi akiwa na Jacqueline Wolper, Sarah Michelotti kutokea Italia, Kajala Masanja, Briana kutokea Australia na Yolo The Queen wa Rwanda.

Utakumbuka hadi sasa Harmonize amefunga ndoa mara moja ambapo alimuoa Sarah Septemba 2019 na kuachana Desemba 2020, ikiwa ni takribani mwaka mmoja wa ndoa yao ambayo sherehe yake ilikuwa ya faragha. 

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakijirudia sana kwa Harmonize pindi anapokuwa katika penzi jipya ni kuwatumia warembo anaokuwa nao katika video za nyimbo zake kitu ambacho kinawavutia mashabiki wengi.

Alimtumia Wolper katika video ya wimbo, Niambie (2017), Sarah katika video za nyimbo, My Boo Remix (2019) na Niteke (2019), Kajala katika video ya wimbo, Nitaubeba (2022), huku Briana na Yolo The Queen wakisalimika katika utamaduni huo.

Poshy Queen ndiye mrembo ambaye kwa sasa yupo na Harmonize ambaye tayari kasema atamuoa mwaka huu. Je, naye tutamuona katika kundi la kina Kajala na Sarah au atasalimika kama kina Briana?, ni suala la muda tu.

Ikumbukwe Harmonize ameiga utamaduni huu kutoka kwa aliyekuwa bosi wake, Diamond Platnumz.

Diamond amefanya video na warembo wengi ambao amewahi kuwa nao, alianza na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu aliyetokea kwenye video ya wimbo wake, Moyo Wangu (2011), kisha Hamisa Mobetto katika video, Salome (2016).

Naye Zari The Bosslady, kama alivyojaliwa watoto wawili na Diamond, Tiffah (2015) na Nillan (2016), huyu ametokea katika video mbili za Diamond, Utanipenda (2015) na Iyena (2018) na ndiye mpenzi pekee wa Diamond mwenye rekodi hiyo.

Jambo lingine linaloweza kumtokea Poshy Queen katika uhusiano na Harmonize, ni kutungiwa nyimbo pale anapomkosha sana au kumuumiza. Ikifikia hatua hiyo, Konde Boy huwa hachezi mbali na studio, Kajala ni mfano halisi katika hilo.

Kipindi penzi lake na Kajala limpamba moto, Harmonize alimuimbia nyimbo kama Deka (2022) na Nitaubeba (2022), na pindi alipomuumiza na kuachana, akamtolea nyimbo kama Mtaje (2021), Vibaya (2021) na You (2022).

Utakumbuka Harmonize ambaye ni Baba wa mtoto mmoja, Zurekha, ameshatoa albamu nne, Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022) na Visiti Bongo (2023), pamoja na EP moja,  Afro Bongo (2019) akiwashirikisha Burna Boy, Yemi Alade na Mr. Eazi.