Hekaya za Mlevi: Gen Z oneni enzi zetu
Muktasari:
- Kule nyanda za juu kusini bibi anateremka kutoka kilimani kuja kumsalimia mwenzake aliye kisimani. Usishangae akiuliza kuku na bata “waghonile?” Na makatapela (maparachichi) hayajambo?
Dar es Salaam. Waswahili huifanya salamu kuwa ni habari kamili. Badala ya kusalimiana huku wakipishana, wao huweka kikazi kabisa. Utaulizwa habari za nyumbani, za kazini, za kijijini kwenu na kadhalika.
Kule nyanda za juu kusini bibi anateremka kutoka kilimani kuja kumsalimia mwenzake aliye kisimani. Usishangae akiuliza kuku na bata “waghonile?” Na makatapela (maparachichi) hayajambo?
Mambo yetu yalikuwa ya kianalogia kwelikweli; mtu aliweza kuandika barua ya karatasi mbili, nusu ya barua nzima ikiwa ni salamu: “Mara baada ya salamu natumaini hujambo na unaendelea vema kusukuma gurudumu la maendeleo.” Usije ukadhani kuwa kamalizia hapo, atakuja na “natumaini pia kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mama na ndugu zangu wote hapo nyumbani hawajambo”.
GenZ hawayawezi kabisa mambo hayo. Siku hizi wanabofya simu na kuandika herufi mbili tu: “vp”. Jibu linakuja kwa herufi moja: “p”. Hayo ndio mambo ya digitali. Japokuwa nao wakati mwingine wanazingua, badala ya kuandika “sasa” wanaandika “xaxa”. Lakini wanajitahidi kuokoa muda kwa kufanya mawasiliano kuwa mafupi na yenye tija. Kwa mfano anaposema “mishe vp” anakuwa tayari ameshaomba kazi.
Ni kama mpira wa zamani wa Wamisri; kipa anarusha mpira kwa beki mbili anayepiga ndefu kwa winga namba saba. Saba anakunja ya juu kwa namba tisa, kinapigwa kichwa na watu wanarudi wakishangilia. Watu hawakuwa wakihesabu pasi za timu, wao walitaka magoli tu. Na enzi zile hakukuwa na VAR wala sheria 17, hivyo goli lilitegemea ujanja na ubabe wa wachezaji.
Kwa mfano gemu ya Simba na Pan Afrika pale Uwanja wa Taifa. Siku hiyo nilijua nini maana ya uzalendo michezoni. Ngoma ilipigwa hadi nyasi zilibadilika rangi. Ukiutazama uwanja kutoka jukwaani unauona wazi ukifuka moshi. Wote ni watoto wa mjini pale Kariakoo, hivyo dabi yao ilikuwa gumzo kila walipokutana. Ukileta usela unapewa undava!
Pan wakapigwa bao la kwanza. Walikuwa na kawaida ya kumuuliza Peter Tino kila wanapofungwa. Akikubali basi wanapeleka mpira kati akikataa basi mpira utaishia hapo kwa mateke na magumi. Tino alilikubali goli, mpira ukapelekwa kati. Tino aliwapa moyo kuwa analo bao mguuni kwake, na kweli kufuatia kazi nzuri ya Hussein Ngulungu, Gordian Mapango na yeye mwenyewe wakarudisha bao.
Kwa upande wa Simba nako, akina Adam Sabu na Jumanne Hassan (Masimenti) waliliandama lango la Pan kama nyuki. Nadhani siku hiyo kipa wa Pan alilazimika kukanda mikono baada ya mechi. Alimiminiwa makombora hadi alijiuliza kama hawa washambulizi wa Simba walikuwa na nia njema kwake. Lakini hakuna mpenda soka asiyemjua Pondamali “Mensah”.
Dakika ziliyoyoma na kutishia mpambano huo kuishia katika suluhu. Simba wakaona hapana, imma fa imma lazima ushindi upatikane. Iwe kwa heri au shari; hata ikibidi silaha za maangamizi zitumike. Wakafosi hadi wakapata kona. Simba walishangilia kwa nguvu kwani kwao kona ilikuwa mwendo wa goli. Nilikwambia mpirani hakukuwa na sheria zenu za sasa. Ati kipa asiguswe! Wenzenu wanamtaka huyo kipa waishi naye.
Hilo lilikuwa ni jambo la hatari sana kwa kipa Juma Pondamali. Yeye na Sabu walicheza katika timu hasimu za mchangani, pale Kariakoo. Kama sikosei moja iliitwa Kunkoma Nyani. Ni zile gemu zilizochezeshwa na waamuzi watata kama marehemu King Sabata. Ukimsachi hutakosa kumkuta na bisibisi kiunoni. Kwa hiyo waliwatambua vema maana hawakuishia kudundana wenyewe, bali na refa alikuwamo.
Basi Mohammed Kajole aliyekuwa mtaalamu wa kupiga kona akaufuata mpira. Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Ponda, maana Kajole alikuwa na uwezo wa kupiga kona ikaingia wavuni bila kuguswa. Hivyo akawapanga walinzi wake katika nafasi zao, akaweka umakini zaidi kwa Sabu na Kajole.
Kona ikapigwa. Kufumba na kufumbua Sabu alikwishafika kwa Ponda, akamkanyaga miguuni ili asiweze kuruka. Ponda alimpigia kelele mwamuzi kutoka Lindi lakini haikusaidia. Mpira ulikwenda kugonga besela la juu, ukarudi. Masimenti akapiga kichwa cha juu, maana ilikuwa si rahisi pale langoni. Ilitanda ngome ya akina Jella Mtangwa, Leodegar Chilla Tenga, Jaffari Abdulrahmani na Mohammed Mkweche.
Ngoma ilikwenda kugonga besela kwa mara ya pili. Wakati wote huo Ponda hakuweza kujinasua kutoka kwa Sabu. Mpira uliporejea ukamkuta Mtemi Ramadhani. Hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, hivyo akausindikiza mpira kwa mkono. Mwamuzi akasema “ni bao, weka kati”.
Pondamali alivurugwa kwelikweli. Akamfuata refarii, lakini akarudishwa kwa kadi ya njano. Peter Tino alimhakikishia kuwa atasawazisha bao hilo la pili, maana katika mtanange huo Pan walihitaji sare tu. Afanaleik! Peter Tino alisawazisha bao kwa shuti la mbali. Ponda alimkimbilia tena mwamuzi kumtambia “kiko wapi!” Lakini refa alipomwona, akaingiza mkono kwenye mfuko wa ghorofani.
Ponda alipiga hesabu za haraka: Alishapigwa ya njano, itakayotoka sasa itakuwa nyekundu”. Basi kama kifutu, alimrukia mwamuzi na kumchota “mtama”. Kwa msioelewa alimpiga ngwala ya kisasa (kwa wakati ule). Acha nimalizie kwa kusema mpira uliishia hapo, ukapokelewa na mchezo wa mchanganyiko wa ndondi, mieleka, judo, karate na mingine ya aina hiyo. Ajabu, mchezo huu usio rasmi ndio ulioshangiliwa zaidi.