Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HEKAYA ZA MLEVI: Waachieni watoto wauishi utoto wao

Muktasari:

  • Zilikuwa na malengo ya kuwajenga kwa uzalendo kwenye jamii yetu. Lakini ukizichukulia kwa mapana zaidi, ziliwasisitizia uadilifu na uzalendo wa Taifa lao. Hadithi hizi zilisindikizwa na nyimbo za kizalendo pia; “Tazama Ramani”, “Tanzania Nakupenda” na kadhalika.

Dar es Salaam. Nani anakumbuka hadithi za kina Kalikalanje, Nunda Mla Watu, Kalume-kenge, Kibanga Ampiga Mkoloni na Sikili Mimi Maskini? Ni simulizi zisizoisha ladha japokuwa walengwa wake ni watoto.


Zilikuwa na malengo ya kuwajenga kwa uzalendo kwenye jamii yetu. Lakini ukizichukulia kwa mapana zaidi, ziliwasisitizia uadilifu na uzalendo wa Taifa lao. Hadithi hizi zilisindikizwa na nyimbo za kizalendo pia; “Tazama Ramani”, “Tanzania Nakupenda” na kadhalika.


Mataifa yote hapa duniani huwafundisha watu wao uzalendo wa kikwao. Sisi tulifundishwa kulilinda Taifa dhidi ya maadui wa nje na ndani. Maadui wa nje ni wavamizi, wachochezi na kadhalika. Wa ndani ni wengi zaidi wakiwamo wanafiki, ujinga, umasikini, maradhi na ukosefu wa maadili. Elimu ya uzalendo ilianzia utotoni ili mtoto aishi nao hadi ukubwani mwake. Tena ilianzia kwa kina babu na bibi katika hadithi za kutafutia usingizi.


Mtoto hajawahi kupitia uzee, lakini mzee aliwahi kuupitia utoto. Kwa vile mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, inaonesha wazi kuwa babu na bibi walijengwa kitabia wakingali watoto. Walipokuwa wazazi, wakawalea watoto wao vema. Hata walipopata wajukuu, hawakuacha kuwakumbusha watoto wao kuwasimamishia nguzo imara wajukuu zao. Enzi zile hakuna mtoto aliyekwenda kulala bila kupata japo hadithi ya kizalendo kila siku.


Huo ni upande mmoja tu, ambao ni elimu ya mapokeo. Lakini kama nilivyotangulia kusema, kila rika lilikuwa likifundishwa elimu ya uzalendo kwa namna yake. Shuleni kulikuwa na masomo  ya kimtaala kama Siasa na Uraia. Kama vile haitoshi, watoto walifundishwa sanaa na stadi za kazi zilizowaruhusu kuendeleza vipaji vyao. Lakini pia ilikuwapo elimu ya uzalendo kwa marika ya jamii zilizoishi kimila kwa kuzingatia umri, kama ilivyo kwa Morani wa Kimasai.


Katika ulimwengu wa leo kila jamii imezama kwenye kiteknolojia. Hapa ndipo tunapotakiwa kuwa makini maradufu tusije tukavuruga badala ya kujenga.

Katika mageuzi makubwa ya teknolojia, tunaweza kusahau mtaala wa maisha na kusema “watoto wa kidigitali”. Lakini maisha yana mfumo wake wa makuzi ya mtoto. Ukimpelekea mtoto teknolojia inayouzidi umri wake, utakuwa umemrusha hatua muhimu atakazolazomika kuzirudia baadaye kwa lazima.


Mara kadhaa tumeona watu wazima wenye mambo ya kitoto. Mtoto anayefungiwa bila kucheza michezo ya utotoni, ukubwani atakuwa na nafasi kubwa ya kuwa “mtu mzima hovyo”. Anaweza kuwa “bosi kitambi” linalotongoza kila mrembo anayeomba kazi. Au mwalimu wa hovyo anayebaka watoto. Haya ni matokeo ya kuruka mtaala wa makuzi, kwani mtoto aliyepita kwenye mapito kiusahihi hawezi kufanya ujinga ukubwani. 


Nilistushwa kidogo hivi majuzi nilipoyasikia yanayoendelea mkoani Mbeya. Kule mamlaka zimechukua hatua ya kuwalinda wanafunzi dhidi ya ajali za barabarani. Safi sana. lakini wanafunzi hao wamewekewa kitufe cha kusimamisha magari wapate kuvuka barabara. Pengine wabunifu wa usalama barabarani, hasa kwenye maeneo ya shule wanastahili pongezi, kwani mara nyingi madereva hasa wa bodaboda na bajaji hawaheshimu haki za watoto na wanafunzi. 


Lakini nikipiga picha ya zoezi hilo likiwa linaendelea, napata kicheko kinachoniumiza tumbo. Namwona mtoto anayetimiza haki yake ya michezo ya utotoni akicheza na kitufe siku nzima. Anakibonyeza na kukimbia huku akicheka. Anafurahi kuliona lori lililopakia shehena ya mzigo linavyohangaika kusimama ghafla. Pengine si kosa lake, hajui kuwa furaha yake inaweza kuzua ajali na uadui baina ya madereva na watoto.
Ilinikumbusha mtoto mwenzetu alipoingia shuleni na bunduki ya baba yake.

Siku hiyo ilibidi masomo yaahirishwe maana Mwalimu Mkuu alipandisha shinikizo la damu. Mtoto alipania kuwatishia watoto wenzake waliokuwa wakimwonea. Lakini alipogundua kuwa wakubwa waliiogopa ile mashine, akaanza kuwakimbiza nayo. Tukio hilo lilimgharimu baadaye, maana alikula bakora mseto za walimu na wazazi, na akaishia kuhamishwa shule.
Mimi nawapongeza sana Mbeya, ila nawasihi wasiwape watoto ukubwa.

Kitendo cha kumpa mtoto mamlaka ya kusimamisha magari kwa kitufe, kinaweza kuongeza ajali badala ya kupunguza. Mamlaka hayo hata kama wangelipewa watu wazima, bado lingekuwa tatizo. Inahitaji elimu ya kutosha ya masuala ya barabara, ndio maana kazi hiyo ikawafaa askari wenye mafunzo maalum. Ni sawa na kumruhusu yeyote atoe hukumu kwenye kiti cha hakimu.


Mimi nadhani kitu cha msingi ni kukazia elimu zaidi kwa watoto. Hivi sasa kuna matukio mengi ya uvunjifu wa sheria za barabarani. Hivyo kuifikisha elimu hiyo kwa watoto linaweza kuwa suluhisho huko mbeleni. Wapatiwe elimu ya nadharia darasani, na katika vipindi vya televisheni kwa njia ya vikatuni. Inaeleweka kuwa huwezi kumtenganisha mtoto na katuni. Ukifika wakati wa elimu ya vitendo basi wasimamiwe na wataalamu. 


Nitoe wito kwa taasisi za elimu kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto kiteknolojia. Tatizo ninaloliona hivi sasa ni namna wenetu wanavyosukumwa na teknolojia kwenye tamaduni za Kimagharibi. Wenzetu wanawatengenezea watoto katuni za vita, uhasama na mauaji. Labda ndio utamaduni wao, kwani si ajabu mtoto wa Kiyahudi akafundishwa kulenga shabaha kwenye picha ya mtoto wa Kiarabu. Sisi tusiuingie mtego huo, bali tuwape wenetu katuni za kujikinga na ajali, maradhi na ufisadi.