Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hekaya za Mlevi: Vijana wanasingiziwa mengi

Muktasari:

  • Lakini ugomvi ulizinduliwa kwa agizo kwamba binadamu amsigine nyoka kichwani, na nyoka amgonge binadamu kisiginoni. Kwa maelezo ya vitabu, maagizo hayo yalitolewa na Mwenyezi Mungu aliyewaumba nyoka na wanadamu. Mpaka leo agizo hilo linaishi, japo sina hakika kama nyoka analijua na kulifuata kama ilivyo kwa wanadamu. Nasema hivyo kwa sababu hadithi za wanadamu wenyewe zinanichanganya.

Dar es Salaam. Ugomvi wa binadamu na nyoka hautakwisha kirahisi. Ni ugomvi wa asili uliogubikwa na kisasi tangu enzi na enzi. Vitabu vitakatifu vinasema ugomvi ulianza rasmi pale Adamu aliposhawishiwa na Eva, akamkosea Mungu kwa maelekezo ya nyoka. Inasemwa kuwa kwa sababu hiyo, Mungu alibadili mpango wake juu ya Adam na Eva, akamfanya Adamu ale kwa jasho na Eva azae kwa uchungu.

Lakini ugomvi ulizinduliwa kwa agizo kwamba binadamu amsigine nyoka kichwani, na nyoka amgonge binadamu kisiginoni. Kwa maelezo ya vitabu, maagizo hayo yalitolewa na Mwenyezi Mungu aliyewaumba nyoka na wanadamu. Mpaka leo agizo hilo linaishi, japo sina hakika kama nyoka analijua na kulifuata kama ilivyo kwa wanadamu. Nasema hivyo kwa sababu hadithi za wanadamu wenyewe zinanichanganya.

Nimepata kusikia kuwa nyoka ni mwoga sana wa binadamu. Kinachomsababisha amgonge ni kujihami pale akutanapo na miguu ya binadamu inayotembea. Kwa kuwa nyoka hutambaa, huwa kwenye hatari kubwa ya kukanyagwa na miguu hiyo. Hivyo huwa wa kwanza kukigonga kisigino cha mwanadamu kabla hakijatua kichwani pake. Ndio maana inasemwa kuwa nyoka hawezi kumdhuru mtoto, kwani mtoto hawezi kuingia kwenye anga za nyoka.

Sababu ingine ni pale nyoka anapolinda watoto au mayai yake. Mara zote mdudu huyu hutaga vichochoroni, na huyafunika mayai kwa nyasi ama udongo. Baada ya hapo mwenyewe hukaa umbali mfupi akiyalinda dhidi ya wanyama waharibifu. Sasa ilitokea umepita njia hiyo nawe unawekwa kwenye kundi la waharibifu. Atafuatilia hatua zako kabla ya kuuwahi mguu wako usije ukatua kwenye mayai.

Ukitazama kwa undani, binadamu ndiye anayeanza kumrusha roho mwenzie. Kwenye suala la watoto, hata mbuni humfurusha simba pale anapowaingilia wanawe. Unamkumbuka koboko aliyewagonga wanajeshi waliokuwa safarini kwenye lori lao? Yeye alitaga ardhini, kisha akapanda mtini kuweka ulinzi wa mayai yake. Alikuwa tayari kumshambulia yeyote aliyeelekea kuyatimba. Kwa bahati mbaya lori likayakaribia, na koboko akachukua hatua!

Hapa ndipo kisasi kinapochukua nafasi. Mama aliyempoteza mumewe kwenye ajali ya koboko, anapika uji mwepesi na kuubeba mtungini ungali wa moto sana. Koboko akishamwona mama huyu anajua kwamba naye anakwenda kuangamiza mayai. Sasa kwa vile nyoka huyo hushambulia kutokea juu ya mti, anajikunja na kujikunjua kwa kasi akiamini kuwa analenga utosi wa mama. Kumbe anajitumbukiza kwenye jehanamu ya uji wa mtama!

Samaki mmoja akioza, kapu zima linatupwa jalalani. Hivi ndivyo mtazamo wa kisasi ulivyo. Kama mtu kakosana na mwenzake, hata watoto na wajukuu wanahusika. Hivyo nyoka hata asiwe na sumu bado atabeba mzigo ya nyoka muuaji. Kama walivyoimba Sikinde, nyoka na binadamu wanachekeana jino pembe. Kama Sikinde na Msondo, Simba na Yanga, na mimi naongezea: “kama vijana na jamii yao”.

Ni kweli wapo vijana wasiojitambua. Kutokana na matarajio yao makubwa, wanaingia kwenye tamaa za mafanikio ya mapema bila kujua upeo wao mdogo. Kijana anaingia kwenye makundi mabaya na kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu. Mambo yake yanapoharibika, kijana anatafuta faraja ya haraka. Anajikuta akizamia kwenye uraibu wa pombe na dawa za kulevya, bila kujua ndio anaharibu zaidi.

Lakini tusilaumu moto uliochoma soko bila kumtaja yule aliyeuwasha, maana risasi haiui mtu bila kufyatuliwa na mtu. Vijana wasichukuliwe kwa mtazamo hasi bila kutazamwa kilichowafikisha hapo. Kila mmoja alikuwa na tamaa ya kuwa bosi au mfanyabiashara mwenye mafanikio. Na hangeweza kuwa hivyo bila misingi thabiti inayowekwa na wazazi au walezi wake. Kwa maneno mengine tunasema “kijana umleavyo ndivyo akuavyo”. 

Anayetengeneza mtaala wa mtoto ni mzazi. Kijana anaweza kusifiwa au kulaaniwa kutokana na yale aliyoyabeba, au aliyokataa kuyabeba kutoka kwa wazazi na walezi. Akiyabeba mazuri atanyooka lakini akikataa kuyabeba atapinda. Kadhalika akiyabeba mabaya na kuyakataa mazuri atageuka nunda asiyenoga kwenye jamii. Swali la kwanza kwa wazazi: ni mzigo wa aina gani wanaombebesha mtoto wao?

Mtoto anaanza kunusa shida tangu akiwa mdogo. Ghafla mama yake mzazi anatimuliwa, naye anawekwa chini ya uangalizi wa “Mama wa kambo”. Wakati ule ilikuwa kawaida kwa mama wa kambo kumpenda mtoto aliyemzaa mwenyewe, na akamchukia mtoto aliyemkuta kwa baba. Sababu zilikuwa wazi, ni wasiwasi wa mama kukosa mali zitakazorithishwa kwa mtoto aliyemkuta. Sasa mama anapiga darubini kali na kujiona akinyanyasika baada ya mumewe kufariki.

Baada ya kuyaishi mateso, mtoto anaondoka na machungu ya pande zote mbili. Hata kama wanayopitia haya ni wachache, kitu cha kutisha ni kwamba wao ni sehemu ya jamii. Wanaweza kuwaambukiza wengine, au kuchafua taswira ya vijana wote kama ilivyo sasa. Kwa hiyo tunaona jinsi wazazi walivyo na mchango mkubwa kwenye misingi ya maadili ya vijana.

Iwapo wazazi wake wangeitunza ndoa yao kikamilifu, asingeshuhudia mama yake akiburuzwa kutoka nyumbani. Au asingetoroka nyumbani kukwepa vipigo vya mama mkatili, wala asingekutana na makundi ya hovyo yaliyotopea kwenye uraibu wa vilevi. Kijana angelisimamia ndoto zake za mafanikio. Hivyo inafaa wazazi nao kupitia majukwaa yao, wapewe elimu ya kujitambua kama wanayopewa vijana.