Huyu hapa mshindi wa Miss Universe Tanzania 2025
Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuvalishwa Taji na kukabidhiwa zawadi ya gari aina ya Hyundai Creta, Naisae ameelezea furaha yake na kusema atatumia ushindi huo kuwainua wanawake wengine kama kaulimbiu ya mashindano hayo isemavyo 'Empower Beyond.'
Dar es Salaam. Usiku wa kuamkia leo Agosti 24, 2025, imefanyika fainali ya mashindano ya Miss Universe Tanzania katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki ambapo mshiriki namba 13, Naisae Yona ameibuka mshindi wa taji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuvalishwa Taji na kukabidhiwa zawadi ya gari aina ya Hyundai Creta, Naisae ameelezea furaha yake na kusema atatumia ushindi huo kuwainua wanawake wengine kama kaulimbiu ya mashindano hayo isemavyo 'Empower Beyond.'
"Siwezi kuamini kama niko hapa lakini nilijua kuwa nitaenda mbali kwenye safari hii , kuanzia siku ya kwanza nilimtanguliza Mungu na nina shukuru sana. Tulikuwa kambini kwa siku 21 lakini tulifurahia na tumejifunza vitu vingi.
"Mimi ni mjasiriamali biashara yangu ya kwanza nilianza nikiwa na miaka tisa nataka kushea maarifa niliyopata kwa wanawake wengine, kila mwanamke anaweza kujitegemea akiwa na biashara yake kwahiyo nitatumia taji langu kuwapa nguvu wanawake wengine," amesema Naisae.
Naisae amesema atahakikisha anawakilisha vizuri Tanzania katika mashindano ya Miss Universe kwa levo ya dunia ambayo yanatarajiwa kufanyikia nchini, Thailand.
"Najiona nikiwakilisha Tanzania vizuri, najiona nikiitangaza nchi yangu kupitia utu, upendo na heshima kama mtoto wa kike najua nitafika mbali nikiingia kwenye Miss Universe katika levo ya dunia" amesema Naisae.
Aidha, amesema muda aliotumia kambini na washiriki wenzeke umekuwa na manufaa ambapo amejifunza kujiamini, kuongea vizuri tofauti na hapo awali.
"Nimejifunza kujiamini, nilivyoingia pale nilikuwa kama samaki aliyetoka kwenye maji unaangalia hapa mtu anajua kutembea. Mwingine anajua kuongea nikasema nitaweza kweli lakini tulipata waalimu wazuri sana, nimefundishwa na waalimu lakini pia na wenzangu, leo nilivyokuja hapa The Superdome nikasema ni mimi nitaweza ni mimi na nitafanya vizuri" amesema.
Hatahivyo mshindi huyo wa Miss Universe Tanzania 2025 amewashukuru washiriki wenzake wote kwa ushirikiano waliokuwanao kambini hapo.
"Nawapenda wote Mungu awabariki mmenisaidia sana kambini nimeweza kuongea na kutembea leo kwasababu yenu mlinisaidia kama wanawake tukiungana mkono kweli tutafika mbali" amesema.
Utakumbuka hii ni mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika Tanzania huku yakiongozwa na mrembo aliyekuwa mshindi wa taji la Miss universe kwa levo ya dunia mwaka 2019, Zozibini Tunzi.