J Lo maswali kibao kuwa single mother
Muktasari:
- Mrembo huyo aliyetamba kwenye nyimbo nyingi kali alisema bado anajiuliza maswali mengi kichwani mwake kama kuwa single mother ni kitu chenye faida kubwa kwa watoto wake pacha, Max na Emme.
MAREKANI. Nyota wa muziki na filamu, Jennifer Lopez amefichua ana mambo mengi kichwani mwake, kubwa ni kulea watoto wake kama single mother.
Mrembo huyo aliyetamba kwenye nyimbo nyingi kali alisema bado anajiuliza maswali mengi kichwani mwake kama kuwa single mother ni kitu chenye faida kubwa kwa watoto wake pacha, Max na Emme.
Katika mahojiano aliyofanya wakati wa kufanya promosheni ya filamu yake mpya ya Unstoppable, Jennifer ambaye ni maarufu kwa jina la JLo, akiwa na umri wa miaka 55, alizungumzia namba inayofaa kuwalea watoto wake pacha wenye miaka 19 akiwa peke yake kama mzazi wa kike.
“Nimekuwa mzazi pekee wa kike kwenye malezi ya watoto mara nyingi kwenye maisha yangu na nimekuwa nikijiuliza kama nafaa kwenye hilo. Ukweli ni mara zote unahitaji mzazi ambaye atakupenda,” alisema.
JLo na mumewe wa zamani Marc Anthony walifanikiwa kupata watoto hao pacha Max na Emme mwaka 2008. Wawili hao walifunga pingu za maisha 2004 kabla ya Anthony kufungua jalada kutaka waachane mwaka 2012. Ndoa yao ilifika ukomo 2014.
Kutokana na hilo la kuwa mzazi pekee wa kike kwenye malezi ya watoto wake, JLo alitangaza kusitisha shoo yake ya This Is Me...ili kupata muda wa kutosha wa kukaa na watoto wake katika kipindi cha majira ya kiangazi yaliyopita.
“Niliamua kusitisha ile ziara yangu ya kimuziki kwenye kipindi cha majira ya kiangazi ili kuwa nyumbani na watoto wangu,” alisema JLo.
Lopez, ambaye yupo kwenye sakata la kuachana na mumewe mwingine Ben Affleck, alitumikia kipindi hicho cha majira ya kiangazi akiwa na watoto watatu wa Affleck: Violet, 19, Serafina, 15, na Samuel, 12.