Jennifer Lopez kuvaa vidani vyenye jina la mumewe kwake kawaida
Muktasari:
- Utakumbuka Lopez (54) na Affleck (51) walikuwa na uhusiano mwaka 2002 hadi 2004 walipoachana. Lopez akafunga ndoa na Marc Anthony (2004 - 2014) na kujaliwa watoto wawili, huku Affleck akimuoa Jennifer Garner (2005 - 2018) na walijaliwa watoto watatu.
Marekani.Kuelekea siku ya wapendanao (valentine’s day) Februari 14, staa wa muziki na filamu duniani, Jennifer Lopez (J.Lo) ameongeza mkufu mwingine wenye kidani cha dhahabu chenye jina la mume wake, Ben Affleck.Lopez alionekana kwenye mtandao wa Instagram Jumamosi iliyopita akiwa amevalia mkufu huo mpya katika video (reel) yake ambayo alikuwa anatoa mafunzo ya urembo wa ngozi kuelekea siku ya wapendanao kwa hisani ya chapa yake ya urembo, JLo Beauty.
“Kwa hivyo likizo yangu ya mwaka ninayoipenda zaidi, ni siku ya wapendanao, inakuja na nilitaka kujipodoa vizuri zaidi,” alisema Lopez katika video hiyo, huku akiendelea kuchanganya vipozi vyake mbalimbali.
Utakumbuka Lopez (54) na Affleck (51) walikuwa na uhusiano mwaka 2002 hadi 2004 walipoachana. Lopez akafunga ndoa na Marc Anthony (2004 - 2014) na kujaliwa watoto wawili, huku Affleck akimuoa Jennifer Garner (2005 - 2018) na walijaliwa watoto watatu.
Wawili hao walikuja kurudiana Julai 2021, ikiwa ni miaka 17 ya utengano wao, walichumbiana kwa mara ya pili mnamo Aprili 8, 2022 na walifunga ndoa Las Vegas nchini Marekani Julai 16, 2022 ikiwa ni ndoa ya nne kwa Lopez katika maisha yake.
Kuweka jina la mume wake katika vidani vyake sasa limekuwa ni jambo la kawaida kwa Lopez, aliwahi kuonekana na kilichoandikwa ‘BEN’, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuchumbiana, pia ana kingine cha almasi ‘Mrs. Affleck’ alichokivaa baada ya harusi yao.
Mwimbaji huyo wa kibao maarufu, On The Floor (2011) akishirikiana na Pitbull, pia anamiliki mkufu wa chapa ya Jennifer Zeuner wenye kidani kilichoandikwa ‘Jennifer na Ben’, huu alionekana ameuvaa katika chapisho lake Instagram mnamo Novemba 2022.
Novemba 2022 Lopez katika mahojiano na jarida la Vogue alisema amebadilisha jina lake la mwisho baada ya kuolewa na Ben Affleck, alieleza kuwa watu bado watamuita ‘Jennifer Lopez’ ila jina lake halali kwa sasa ni ‘Mrs. Affleck’.
“Sisi ni mume na mke, ninajivunia hilo na sidhani kuwa hilo ni tatizo. Nina udhibiti mkubwa wa maisha yangu na hatima yangu na ninahisi kuinuliwa kama mwanamke,” alisema Lopez.
“Ni bahati, furaha na fahari kuwa naye, ni hadithi nzuri ya mapenzi ambayo tumeipa nafasi ya pili. Tuna watoto, tunaishi maisha yetu kwa njia ambayo tunaweza kujivunia na watoto wetu kujivunia” alisema Lopez katika siku yake ya kuzaliwa mwaka 2021.
Ikumbukwe kabla ya kukutana na Affleck, staa wa filamu waliyocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), Lopez alikuwa na uhusiano na mtu mwingine maarufu, naye ni Mtayarishaji Muziki, Puff Daddy au Diddy kati ya mwaka 1999 hadi 2001.
J.Lo, aliyejitosa kwenye muziki na albamu yake ya kwanza, On the 6 (1999), uhusiano wake na Diddy ulikuwa na misukosuko mingi, waliwahi kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha na mali za wizi.