Je 2026 ina siri gani kwenye muziki?
Karibu kila redio nchini kwa sasa ina kipindi cha muziki wa zamani, majina ya vipindi hivyo yanaonyesha sura ya vipindi vyenyewe, Zilipendwa, Zama zile, Za kale , Old is gold, Ya Kale dhahabu, Old school na kadhalika. Kwa kawaida watu huita vipindi hivi vya muziki, vipindi vya ‘Zilipendwa’. Neno hili lilizaliwa Radio Tanzania Dar es Salaam likiwa jina la kipindi ambacho kilikuwa kikirushwa Jumamosi usiku na kurudiwa Jumapili asubuhi, kipindi ambacho kilikuwa kikipiga nyimbo za zamani.
Haya tena ndio tunauaga mwaka 2025, kwa sie wengine tuliozaliwa miaka ya 50, tunashangaa na kumshukuru Mungu kwa kuwa hai, maana tulipokuwa wadogo hata kutaja mwaka 1990, ilikuwa ni kama unaongea ndoto ya mbali. Mengi yamepita toka utoto na ujana wetu lakini jambo moja bado linadumu tena kwa afya njema, na jambo hilo ni muziki wa zamani, muziki uliorekodiwa kuanzia miaka ya 1950 mpaka 1990.
Karibu kila redio nchini kwa sasa ina kipindi cha muziki wa zamani, majina ya vipindi hivyo yanaonyesha sura ya vipindi vyenyewe, Zilipendwa, Zama zile, Za kale , Old is gold, Ya Kale dhahabu, Old school na kadhalika. Kwa kawaida watu huita vipindi hivi vya muziki, vipindi vya ‘Zilipendwa’. Neno hili lilizaliwa Radio Tanzania Dar es Salaam likiwa jina la kipindi ambacho kilikuwa kikirushwa Jumamosi usiku na kurudiwa Jumapili asubuhi, kipindi ambacho kilikuwa kikipiga nyimbo za zamani.
Asilimia kubwa ya radio zinapoanza, wakati wa kipindi chake cha majaribio, mara nyingi muziki unaotumiwa ni ule wa zamani. Kwa kupiga muziki huu watu huzoea masafa hayo na radio inapoanza rasmi matangazo yake, msikilizaji anakuwa ameshazoea masafa hayo. Ila cha ajabu kuna vituo vya radio ambavyo huachana na muziki huo wa zamani mara baada ya kuanza rasmi matangazo yake, na baada ya hapo huukwepa muziki huo kama ukoma.
Katika radio nyingi, kipindi cha nyimbo za zamani huwa mara moja tu kwa wiki, pengine hili ni jambo jema kwani wapenzi wa muziki huu huwa na hamu kila wiki kusikiliza kipindi chao. Ni wazi kuwa vipindi hivi vya muziki wa zamani vina wasikilizaji wengi sana kwani watangazaji au watayarishaji wa vipindi wa nyimbo hizi za zamani wengi ni maarufu nchini.
Majina kama Masoud Masoud, Zomboko, Stazo, Churchil, Adam Zuberi na wengineo ni majina maarufu katika anga za wapenzi wa muziki wa zamani. Vipindi hivi vina ladha tofauti kadri ya mpangilio wa mtayarishaji wake.
Kuna watayarishaji wengine hupiga muziki ambao husindikizwa maelezo matamu ya matukio mbalimbali ya enzi hizo, watangazaji wegine ni mahiri kwa kumbukumbu za majina ya wanamuziki wahusika katika nyimbo mbalimbali wanazozipiga, na wengine ni mabingwa wa kupangilia nyimbo za zamani na hivyo bila maneno mengi huhakikisha wasikilizaji wao hawabanduki kwenye kipindi kwa kuwateremshia muziki mtamu mmoja baada mwingine. Lakini pia kuna watangazaji vijana ambao kwao muziki wa zamani ni ule uliopigwa miaka ya 90, hivyo basi nao vipindi vyao vina ladha aina nyingine kabisa ya muziki wa zamani.
Tafsiri ya muziki wa zamani nayo ni pana, unaweza kujiuliza je, muziki wa zamani unaanzia wapi? Mara nyingi mtayarishajiwa kipindi ndie anaekuwa na uamuzi katika kipindi chake juu ya tafsiri ya zamani. Kuna vipindi vinapiga nyimbo hata za miaka ya 50, redio nyingine huanzia miaka ya 60 na kama nilivyosema wengine muziki wa zamani ni ule wa miaka ya 90, kila mmoja ikijinadi kuwa inapiga muziki wa zamani, na hakika hakuna aliyekosea kati ya hao.
Ni nini kinafanya muziki huo uendelee kutamba? Kama umeangalia mimi kamwe sijauita muziki huu ‘zilipendwa’, kwani ni muziki uliopendwa enzi hizo, unapendwa sasa na utaendelea kupendwa. Kwa bahati nzuri mimi ni mwanamuziki wa zamani, na pia niliwahi kuwa naendesha kipindi cha muziki wa zamani, huwa nami najiuliza nini kinafanya nyimbo hizi zilizorekodiwa kwa gharama ndogo sana katika studio duni za miaka ya nyuma sana ziendelee kupendwa kwenye ulimwengu huu wa kidijitali wenye nyimbo zilizorekodiwa kwa ubora wa hali ya juu na gharama kubwa na zikiwa zimeambatana na video zilizotengenezwa kwa mamilioni ya shilingi? Kwa kweli sina jibu.
Nyimbo nilizokuwa nazisikia toka utoto wangu na baadae nikawa mwanamuziki nami nikatunga zangu au kushiriki kutunga za wanamuziki wenzangu wengine, huwa nashangaa pale ninapoona vijana wadogo wakipenda sana nyimbo hizi, wanamuziki vijana wakijaribu kuzirudia na nashangaa kuona wapenzi vijana wakizifurahia nyimbo hizi kama walivyokuwa vijana wenzangu miaka hiyo tulipotunga na kuzipiga nyimbo hizo kwa mara ya kwanza. Nyimbo hizi ambazo hazina video wala promo, ukiingia kwanya mtandao wa youtube unakuta wimbo una ‘viewers’ 200 tu mwaka mzima lakini upo toka miaka ya 80 ulipendwa na unaendelea kupendwa.
Kitu ambacho huwa kinanichekesha ni pale vijana wa kileo wanapojaribu kucheza nyimbo za zamani, staili wanazocheza ni tofauti kabisa na zile tulizokuwa tunacheza wenye nyimbo zetu. Kwa mfano ukipiga wimbo wa twist, wazee wakiingia unakuta wanajitahidi kuchezesha visigino na magoti, bahati mbaya uzee unawanyima uwezo wa kuonyesha umahiri, sasa akiingia kijana hapo anaanza kukata kiuno kama feni, twist haikuwa inachezwa hivyo, hakika mtu angecheza staili hiyo enzi hizo angefukuzwa mtaa kwa kuonekana anavunja maadili.
Zamani kulikuwa na uchezaji tofauti wa wanawake na wanaume, lakini siku hizi kila mtu anacheza roho inavyomtuma, wanaume wakicheza staili ambazo zamani tungeona zinafaa kwa akina dada na akina dada wengine wakicheza ‘kibabe’ zaidi.
Kati ya mambo ambayo nadhani yanafanya nyimbo za zamani ziendelee kupendwa ni maneno matamu yenye maana na mafupi, na kwa kuwa kulikuwa na chujio nyingi hakukuwa na nyimbo zenye lugha chafu. Wimbo wa siku hizi unaweza kukuta ni mrefu kurasa mbili au tatu, ambao ukiufuatilia ndani yake kuna maneno kadhaa ambayo hayastahili kutamkwa hadharani, pia wimbo staili za uimbaji zimekuwa zinafanana kiasi cha kutoweza kutofautisha muimbaji mmoja na mwingine, tofauti na zamani, uimbaji wa Dr Remmy ulikuwa tofauti wa Hassan Bitchuka na tofauti na ule wa Eddy Sheggy, na hakika kila muimbaji alikuwa akijitahidi kuleta utofauti.
Kingine ni mpangilio wa vyombo, hili nadhani nalo ni muhimu sana. Kati ya vitu vilivyokuwa vinasisitizwa katika tungo za zamani ni muafaka wa vyombo. Kila chombo kinachopigwa lazima kiwe na mahusiano na kingine, si mradi kimepigwa tu. Taaluma hii bahati mbaya inapotea hata kwenye nyimbo za muziki wa dansi siku hizi. Je 2026 ina siri gani katika muziki tusubiri tuone Mungu aendelee kutupa uhai.