Jiongeze: Kabla ya Dully, kuna Marijani Rajabu!
Muktasari:
- Hakuna Mbongo Fleva mwenye nyimbo nyingi za majina ya watu kama Dully. TID anazo mbili Asha na Rahisa, Matonya anazo mbili Julieth na Anitha. Wapo wengine wanazo lakini hawafikii idadi ile ya Prince Dully Sykes.
Dar es Salaam. Dully Sykes ni msanii mwenye sifa za pekee. Moja ya sifa hizo ni kumiliki nyimbo zenye majina ya watu. Julietha, Salome, Baby Candy, Bujour na Maria, hizo ni sehemu ya nyimbo zake za kitambo.
Hakuna Mbongo Fleva mwenye nyimbo nyingi za majina ya watu kama Dully. TID anazo mbili Asha na Rahisa, Matonya anazo mbili Julieth na Anitha. Wapo wengine wanazo lakini hawafikii idadi ile ya Prince Dully Sykes.
Lakini kabla ya Dully, kulikuwapo wa Dully wa kitambo. Huyu siyo Dully tu, bali kwa wanamuziki wa Bongo wote. Hakuna anayefikia idadi ya nyimbo zenye majina ya watu kumziki. Mwamba kabisa na mtu noma.
Namuongelea Jabalí la Muziki, Marehemu Marijani Rajab. Huyu ni kiboko kwa ngoma zenye jina la mtu na zote zilikuwa ‘hits’ jana na leo. Na Marijani utunzi wake uliegemea kuonya, kufunza na kukumbusha zaidi.
Ngoma kama Georgina, Zuwena,
Siwema, Mwanameka, Masudi,
Matilda, Hanifa, Christina, Vicky,
Mwajuma, Baba Anna, Mayasa zingine zitaendelea toleo lijalo. Huyu dingi alikuwa noma na nusu kwenye eneo hili.
Mbali na nyimbo kuzipa majina ya watu. Pia ndiye mwanamuziki mwenye nyimbo nyingi maarufu kuliko yeyote wa sasa na zamani. Nyimbo zake zote ziliwabamba watu zamani na mpaka leo. Huu ni jabalí kweli.
Pia Marijani ana rekodi ya nyimbo zake nyingi kurudiwa na wasanii wa kizazi cha leo. Pengine kuliko wasanii wote. Siwema, Zuwena na Georgina zinaongoza. Nyimbo zake pia zinaongoza kupigwa na bendi za ‘kukopi’.