Prime
Mwana FA, Dully Syakes walivyokutana na hisia za wana Bongofleva
Muktasari:
- Miguno na zomeazomea vilivyojitokeza katika Tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva vimeibua mjadala, wadau wa siasa wakitaka tafakuri kuhusu hisia za wananchi badala ya kuzipuuza.
Dar es Salaam. Hisia tofauti zilizoonyeshwa na sehemu ya hadhira dhidi ya viongozi wa Serikali na wasanii wakati wa Tamasha la miaka 30 ya Bongo Flava, zimezua mjadala mpana kuhusu tafsiri na athari za tukio hilo katika nyanja za kisiasa na kijamii.
Tamasha hilo liliwakutanisha wasanii wa kizazi cha zamani na cha sasa, waliopanda jukwaani kurejesha kumbukumbu za nyimbo zilizotikisa kwa nyakati tofauti mbele ya maelfu ya mashabiki.
Katika tamasha hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, wasanii 50 wa Bongo Fleva walikusanyika, huku zaidi ya 30 wakitumbuiza mashabiki waliofurika ukumbini.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria Tamasha la miaka 30 ya Bongo Flava Mlimani City.
Tangu mapema, viunga vya ukumbi vilianza kujaa mashabiki waliojitokeza kushuhudia tamasha hilo, ambapo waliokuwa na tiketi waliingia kwa kuskani kadi zao, huku wengine waliowasili bila tiketi wakishindwa kupata nafasi ya kuingia licha ya kuwa tayari kulipia.
Katika matukio yaliyoibua hisia za mashabiki, mojawapo lilimhusu Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), ambaye pia ni msanii, pale alipojaribu kueleza mafanikio ya Serikali kwa kutamka “Serikali ya awamu ya sita...”
Umati ulianza kuzomea na kuguna ili kuzuia hotuba hiyo, jambo lililomfanya abadilishe mada na kuwatuliza wananchi kwa kusema, "Tulieni nyie... nataka kuwaambia kitu kizuri…tunajenga arena," akimaanisha mradi wa ujenzi wa eneo la burudani ya muziki.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA akifurahia wakati wa Tamasha la miaka 30 ya Bongo Flava Mlimani City.
Licha ya kauli hiyo, baadhi ya waliohudhuria waliendelea kupinga kitendo cha kuingiza masuala ya siasa katika tamasha hilo la burudani.
Tukio la pili lilimuhusu msanii Dully Sykes ambaye akiwa jukwaani aliwashukuru kwa kuwataja kwa majina baadhi ya wasanii na alipotaja jina la Makonda, (Paul, Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo), naye alizomewa.
"Basi, basi hiyo mbaya," alisema Dully Sykes na kuacha kuendelea kushukuru watu, akaendelea kutoa burudani.
Matukio hayo yamewaibua wachambuzi wa masuala ya siasa na jamii, wakitoa mitazamo tofautiana, lakini wengi wakikubaliana kuwa tukio hilo hisia hizo za wananachi hazipaswi kupuuzwa.
Msanii Dully Sykes akitumbuiza katika Tamasha la miaka 30 ya Bongo Flava Mlimani City.
Wanasema hisia zilizoonyeshwa na hadhira ni ujumbe unaostahili kutafakariwa na wahusika pamoja na mamlaka husika.
Akizungumzia tukio hilo, mchambuzi wa siasa na mwanahabari, Ezekiel Kamwaga amesema kilichoonekana hakipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa wananchi wanaichukia Serikali, bali ni ujumbe kwamba wananchi hawataki siasa ziingizwe katika shughuli ambazo si za kisiasa.
"Kwenye tamasha watu walinunua tiketi kwa fedha zao na walikwenda kwa ajili ya burudani. Hilo halikuwa tukio la kisiasa. Watanzania kwa sasa hawataki migawanyiko, na siasa za sasa zimekuwa zikiwagawa watu. Ukiziingiza kwenye burudani zinaleta mgawanyiko," amesema.
Kamwaga amesema ushahidi wa hilo ni kwamba baadhi ya viongozi wa Serikali waliopo kwenye tasnia ya muziki, akiwemo Mwana FA, Nick wa Pili na Baba Levo, walishangiliwa walipopanda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza, akisisitiza kuwa zomeazomea zilijitokeza wakati maudhui yalipoelekea kwenye siasa.
"Aliyezomewa pale hakuwa Rais, waliozomewa ni waliozungumza. Walizomewa kuonyesha kuwa walichokuwa wakifanya hakikuwa mahali pake. Hii ni somo kwa viongozi kujua ni mazingira gani yanahitaji siasa na yapi yanahitaji shughuli ziende bila kuingiza siasa," amesema.
Wakati Kamwaga akisema hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie, amesema tukio hilo linaonyesha kuwepo kwa changamoto katika mahusiano kati ya Serikali na wananchi, hasa vijana.
Amesema haikuwa kawaida kwa wapenzi wa sanaa kuonyesha hisia tofauti kila Serikali au baadhi ya viongozi wake walipotajwa, akieleza kuwa kitendo cha baadhi ya viongozi kushangiliwa na wengine kuzomewa, kinaonyesha wananchi wanawatofautisha viongozi kulingana na mtazamo wao.
"Mbali na hayo, hii inaonyesha watu wametulia, lakini wamebeba maumivu moyoni yanayohitaji kuponywa. Serikali ina vyombo vingi; inapaswa kuvitumia kutafuta suluhu kabla hali haijaenea kwenye makundi mengine ya jamii," amesema.
Kwa mtazamo huohuo, Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, kupitia ukurasa wake wa X, pia amesema matukio ya viongozi wa Serikali kuzomewa hadharani hayapaswi kupuuzwa, bali yanapaswa kuchukuliwa kama ishara ya tahadhari kwa walioko madarakani.
"Hasira ya wananchi haijitokezi ghafla; hujengwa na muda mrefu wa kusikilizwa kwa masikio ya uongozi yaliyofungwa," ameandika.
Msigwa amesema heshima ya viongozi haijengwi na madaraka pekee, bali kwa kusikiliza wananchi, kujibu malalamiko yao kwa vitendo na kutatua changamoto zinazowakabili.
"Serikali inayopuuzia dalili za wazi za kutoridhika (kwa wananchi) inajichimbia shimo yenyewe na kuongeza pengo kati yake na wananchi," ameandika, akiongeza kuwa viongozi wanapaswa kutumia matukio kama hayo kujitathmini na kurejesha imani ya wananchi.
Kwa mtazamo mwingine, Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa, Profesa Mohamed Makame amehusisha suala hilo na matukio ya kipindi cha nyuma.
Amesema, hivyo hisia zilizojitokeza zinaweza kuelezwa na mazingira ya kisiasa yaliyowakumba vijana katika kipindi cha uchaguzi na mijadala iliyofuata baada ya hapo.
Amesema baadhi ya wasanii waliowahi kuhusishwa na siasa wamekuwa wakikumbana na kampeni za kutengwa katika mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuwa limechangia mwitikio ulioonekana kwenye tamasha.
Profesa Makame ameungana na wachambuzi wengine, akisema ujumbe mkubwa unaotokana na tukio hilo ni umuhimu wa kutenganisha siasa na shughuli nyingine za kijamii.
Ameshauri Serikali na vijana kujenga majukwaa ya mazungumzo ya mara kwa mara ili kupunguza pengo lililopo.
"Ili kutoka hapa, pande zote mbili zinapaswa kutengeneza maelewano. Serikali iwaheshimu vijana kwa kusikiliza mahitaji yao, na vijana waheshimu mipango ya maendeleo ya Serikali. Mazungumzo ya wazi yataondoa hali ya kutoaminiana inayoonekana sasa," amesema.
Si mara ya kwanza
Mjadala wa namna hii unagusa pia tamasha kama hilo lililofanyika hivi karibuni lililoandaliwa na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa ajili ya kumuenzi msanii mkongwe wa Hip Hop, Profesa Jay.
Msanii Chid Benz akitumbuiza katika Tamasha la miaka 30 ya Bongo Flava Mlimani City.
Katika tamasha hilo, viongozi wa Serikali hawakupanda jukwaani kutoa salamu kama ilivyozoeleka katika baadhi ya matukio ya burudani yenye uwepo wa viongozi, hali iliyoibua maswali kwa baadhi ya wadau kuhusu kutenganisha burudani na siasa bila kuathiri nafasi ya viongozi.
Katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alizuiwa kupanda jukwaani kuzungumza, kwa kilichofafanuliwa na waandaaji kuwa hawakutaka kuligeuza tukio hilo la kisiasa, bali libaki la burudani.